Kesi inayomkabili mke wa bilionea Msuya kuendelea leo

Muktasari:

Kesi ya mke wa Bilionea Msuya kuendelea leo, ambapo Shahidi wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi anatarajia kutoa ushahidi wake.

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella inatarajia kuendelea leo, ambapo shahidi wa pili wa upande wa mashtaka anatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 103/2018 wakidaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni, Dar es Salaam.

Kesi hiyo ndogo inatokana na mshtakiwa wa kwanza Miriam Mrita, kupinga maelezo yake ya onyo yasipokelewe mahakamani kama ushahidi akitoa sababu mbalimbali ikiwemo kuteswa wakati wa kumchukuliwa maelezo hayo.

Mawakili wa utetezi Nehemia Nkoko na Omary Msemo jana waliwasilisha pingamizi hilo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Edwin Kakolaki, ambapo Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda aliiomba mahakama kufanyika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.


Mawakili hao wa utetezi walipinga maelezo hayo baada ya shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi ya msingi WP 4707 Sajenti Mwajuma (42) kuiomba mahamaka kupokea maelezo hayo ili yatumike kama ushahidi.

Akitoa sababu za kupinga maelezo hayo, Wakili Msemo alidai yalichukuliwa nje ya muda kinyume na kifungu cha 50 (1) a cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai CPA kama ilvyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 inayotaka mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo ndani ya saa nnd tangu anapokamatwa.

Alidai mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Mrita, alikamatwa Agosti 5, 2016 na maelezo kumchukulia Agosti 7, 2016 ambapo kifungu cha 51 kinataka muda wa nyongeza kuongezwa endapo maelezo yatakuwa hayajakamilika.

Wakili Msemo alidai, sababu ya pili ya kutaka maelezo hayo yasipokelewe ni baada ya mshtakiwa huyo kudai maelezo hayo aliyatoa baada ya kuteswa.

"Suala mshtakiwa kudai aliteswa lilijitokeza kuanzia mahakama ya Kisutu wakati washtakiwa wakisomewa maelezo ya mashahidi (Committal proceeding) na kudai kuna baadhi ya sehemu zake za mwili wake zilikuwa na makovu, alidai

Alieleza sababu nyingine, wakati mshtakiwa anachukuliwa maelezo hakupewa haki zake kisheria kinyume na kifungu cha 53(c) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai CPA.


"Haki hizo ni pamoja na kuwa na mwanasheria, ndugu au rafiki hivyo mshtakiwa hakupewa haki hii tunapinga kupokelewa kama ushahidi katika kesi hii,"

Naye Wakili Nkoko alidai mpelelezi wakati anamuhoji mtuhumiwa lazima ajue amekamatwa lini ili kujua kama maelezo ya nachukulia ndani ya muda na kama yatakuja nje ya muda ipo haja ya kupeleka maombi mahakamani ili kuongeza muda.

Alidai sababu nyingine ya kuomba mahakama isipokee maelezo hayo, wakati Shahidi anatoa ushahidi wake hakueleza maelezo hayo yalichukuliwa kituo gani.