Kesi jengo lililoporomoka Kariakoo kutajwa leo
Muktasari:
- Leondela na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wamiliki watatu wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, itatajwa leo Desemba 12, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa katika kesi hiyo, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala.
Mdete na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia, katika mahakama hiyo.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa leo mahakamani hapo na kuangalia iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au la.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Novemba 29, 2024 na kusomewa kesi ya kuua bila kukusudia.
Siku hiyo walisomewa mashtaka yao na mawakili watatu waandamizi wa Serikali, Adolf Lema, Grace Mwanga na Erick Kamala, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini.
Wakili Kamala alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alieleza kuwa shtaka la kwanza hadi la 31 ni ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungo hicho.
Alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao kwa pamoja Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.
Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusabisha vifo vya Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.
Pia wanadaiwa kusababisha vifo vya Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.
Wakili Kamala alidai kuwa katika siku na eneo hilohilo, washtakiwa kwa pamoja isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusabisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.
Hata hivyo, siku upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo ulikuwa bado unaendelea, hivyo uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa, ambayo ni leo.