Kesi kocha wa makipa Simba, wenzake kupelelezwa upya
Muktasari:
- Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Mwalami Sultan na wenzake, umedai kupatikana kwa taarifa mpya kuhusu kesi hiyo, hivyo wameirudisha katika hatua ya upelelezi.
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultan na wenzake, umedai kupatikana kwa taarifa mpya kuhusu kesi hiyo, hivyo wameirudisha katika hatua ya upelelezi.
Januari 2, 2023 upande wa mashtaka uliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wameshapeleka taarifa katika Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Caroline Matemu amedai hayo leo Januari 16, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kuwa kuna taarifa wamepata kuhusiana na kesi hiyo hivyo wanazifanyia kazi.
"Kutokana na hilo tumeirudisha kesi hii katika hatua ya upelelezi na hatua ya kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu imesitishwa kwanza," amedai Matemu.
Matemu alida taarifa hiyo wanazifanyia kazi na upelelezi bado haujakamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo iahirishe shauri hilo kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2023 kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Sultan washitakiwa wengine ni Mmiliki wa Kituo cha Soka cha Kambiasso Sports Academy, Kambi Seif, Maulid Mzungu, Said Matwiko, John John na Saraha Eliud.
Katika hati ya mashitaka, inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 huko katika eneo la Kivule lililopo ndani ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washitakiwa walikutwa wakisafirisha kilo 27.10 za dawa za kulevya aina ya herione.
Katika shitaka la pili ilidaiwa Novemba 4, 2022 huko Kamegele katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani washitakiwa walikutwa wakisafirisha kilo 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroine.