Kesi maofisa wa polisi wanaodaiwa kughushi vibali vya silaha kusikilizwa Julai 27
Washtakiwa wakiwa wanatoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Awali, washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha, lakini kwa sasa watakuwa na mashtaka 32. Na wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Julai 27, 2026 kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kughushi vibali vya umiliki wa silaha inayowakabili watu tisa, wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi.
Uamuzi huo umetolewa leo Julai 13, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, John Msafiri, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya usikilizwaji.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF. 19931 Fredrick Malekela (45)mkazi wa Kilwaroad; E. 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga(54) mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo(54)mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus(47)mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe(46)mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi(30) mkazi wa Kisarawe.
Wengine ambao sio maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59) mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce(60)mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio(29)mfanyabiashara na mkazi wa Tataba.
Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025 yenye jumla ya mashtaka 32, yakiwemo ya kughushi na vibali vya umiliki wa silaha.
Kati ya mashtaka 32 yanayowakabili washtakiwa hao, 15 ni ya kughushi kitabu cha leseni za umiliki wa silaha, 15 ni kutoa nyaraka za uongo, ambazo ni kitabu cha leseni za umiliki wa silaha na mashtaka mawili ni ya kukutwa na mihuri ya kughushi ya Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kinyume cha sheria.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo, kinyume na kifungu namba 333 na 335A na kifungu 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Inadaiwa katika mashtaka yao, wanadaiwa kuwa vibali au leseni hizo, zilitolea kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo kitabu cha leseni ya kumiliki silaha cha Desemba 5, 2024 chenye jina la Ahmed Ally, wakati wakijua kuwa sio kweli.
Vile vile mashtaka mengine kuanzia shtaka la pili, hadi la 13, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024 na mwaka 2025 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, walighushi na kutengeneza vitabu vya leseni za kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim.
Shtaka la 14 hadi 30, washtakiwa wanadaiwa mwaka 2025 katika mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kitabu cha leseni ya kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed na wengine, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Shtaka la 31 na 32, washtakiwa kwa pamoja na kwa nia ya makusudi na kinyume cha sheria walikutwa na mihuri ya kughushi ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Julai 28, 2025 na kusomewa mashtaka hayo, ambayo waliyakana na wapo nje kwa dhamana.