Prime
Kesi ubunge wa Baba Levo kuendelea leo kwa utaratibu mpya
Muktasari:
- Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo. anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.
Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, leo Jumatano Julai 8, 2026 inaendelea na usikilizaji wa kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo.
Baba Levo alitangazwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 imefunguliwa na wapiga kura wanne, Johary Kabourou, Lumu Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wakipinga ushindi wake.
Mbali na yeye, Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za sheria na kanuni za uchaguzi.
Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba mahakama, pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Victoria Nongwa ilianza kusikilizwa ushahidi wa walamikaji Jumatatu ya Julai 6, 2026 kwa utaratibu wa mashahidi kuwasilisha kwanza ushahidi wao wa maandishi, na inaendelea tena leo Jumatano, baada ya mapumziko ya Sikukuu ya Sabasaba jana Jumanne.
Shahidi wa kwanza kufungua pazia la ushahidi huo alikuwa Lumu Mwitu ambaye ni mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo.
Akiongozwa na wakili wa walalamikaji shahidi huyo aliiomba mahakama iupokee ushahidi wake wa maandishi ambao alikwisha kuuwasilisha, na mahakama iliupokea.
Kisha alitoa ufafanuzi wa mambo machache, mawakili wa walalamikiwa walianza kumhoji maswali ya dodoso kuhusiana na yale aliyoyaeleza.
Pamoja na mambo mengine shahidi huyo alieleza wakati wa kampeni za uchaguzi huo alifanya upelelezi na kukusanya ushahidi kuhusu masuala ya rushwa na alikuwa akipeleka taarifa hizo kwa mgombea wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe na Abdul Nondo.
Pia alieleza wakati kampeni zinaendelea Baba Levo akiongozana na kundi la watu katika harusi moja alitoa pesa Sh100,000 akidai ni mchango wake kwa ajili ya harusi hiyo na hapohapo akamuomba kura bibi harusi.
Vilevile alidai katika mkutano mwingine wa kampeni zake Baba Levo alimruhusu msanii wa Muziki wa Bongo Fleva, aliyemtaja kwa jina la Diamond Platnum (Naseb Abdul) kuwagawia watu pesa.
Shahidi huyo alidai katika mkutano mwingine Baba Levo alishuhudiwa akiwagawia watu kofia na nguo kama fulana na khanga huku akiwataka wanaume ambao wake zao hawakuwepo wawapelekee zawadi hizo nyumbani na kuwaomba wakipigie kura chama chake.
Baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake, leo Jumatano mahakama hiyo inaendelea na mashahidi wengine ambao pia maelezo ya ushahidi wao yameshawasilishwa mahakamani.
Huu ni utaratibu mpya wa usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi unaotokana na Kanuni za Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025.
Kwa mujibu wa kanuni hizo mashahidi wanapaswa kuwasilisha maelezo ya ushahidi wao mahakamani kwa Naibu Msajili saa 48, kabla ya tarehe na saa ya usikilizwaji wa shauri husika.
Kisha wakati wa usikilizwaji shahidi hupanda kizimbani kutoa ushahidi wa mdomo, kufafanua baadhi ya hoja katika maelezo yake na kuhojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa upande kinzani.
Hakuna shahidi ambaye maelezo ya ushahidi wake wa maandishi hayajawasilishwa mahakamani ataruhusiwa kutoa ushahidi, kama ilivyo kwa kesi za jinai.
Hii ndio kesi ya kwanza na ya pekee ya ubunge kusikilizwa kwa utaratibu huo mpya, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Kufuatia uchaguzi huo, Chama cha ACT-Wazalendo kupitia kwa wanachama wake kilifungua jumla ya kesi 83.
Katika hizo kilipinga matokeo yaliyowapa ushindi wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kata/shehia na majimbo mbalimbali Bara na visiwani.
Hata hivyo, kesi nyingine zote zilitupiliwa mbali kutokana na hoja mapingamizi mbalimbali yaliyoibuliwa na walalamikiwa.
Kesi hii ya ubunge wa Kigoma Mjini ndiyo kesi pekee iliyofikia hatua ya usikilizaji wa ushahidi baada ya kupenya katikati ya mapingamizi yaliyokuwa yakiibuliwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi