Prime
Mahakama yatoa uamuzi pingamizi la Baba Levo
Muktasari:
- Hii ni kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, ambayo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi leo, lakini Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameibua mapingamizi mengine.
Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, imetupilia mbali mapingamizi yaliyoibuliwa na walalamikiwa katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo.
Baba Levo alitangazwa mbunge wa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wamefungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakipinga uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 wadai hao ambao wanajitambulisha wapigakura katika jimbo hilo wanadai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.
Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa ushahidi wa walalamikaji leo, Jumatatu, Juni 6, 2026.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kusikilizwa ushahidi huo, walamakiwa wameibua mapingamizi wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali.
Mapingamizi hayo yameibuliwa na mawakili wa walalamikiwa wakidai kuwa walalamikaji wameshindwa kuwasilisha maelezo ya maandishi ya mashahidi wao kwa mujibu wa kanuni na amri ya mahakama.
Hata hivyo hoja hizo zimepingwa vikali na wakili wa walalamikaji, John Seka ambaye ameieleza mahakama changamoto ya Mfumo wa Mahakama wa Uwasiliahaji Mashauri Kielektroniki na kueleza hatua alizozichukua ikiwa ni pamoja na mawasiliano na Msajili ambaye alimpa ruhusa ya kuwasilisha maelezo hayo kwa njia mbadala ya barua pepe.
Uamuzi
Jaji Nongwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake amekubiana na hoja za Wakili Seka na kusema kuwa hakubaliani na hoja kuwa walalamikaji walipuuza amri ya mahakama.
Hivyo, Jaji Nongwa baada ya kurejea changamoto alizozieleza Wakili Seka na jitihada za mawasiliano alizozichukua amesema kuwa haoni kama walalamikaji wanaweza kulaumiwa kwani kulikuwa na tatizo hilo la mfumo.
"Nakubaliana na hoja kwamba hakuna kiapo cha kuelezea changamoto hiyo. Kwa maoni yangu hatua zilizochukuliwa na walalamikaji zinaonesha kuwa walichukua hatua stahiki," amesema Jaji Nongwa.
"Tumesomewa email (baruapepe) ya Naibu Msajili (Masjala Ndogo Kigoma) kuwa maelezo hayo yamepokewa kwa wakati," amesema Jaji Nongwa na kusisitiza Naibu Msajili ndiye msimamizi wa mashauri.
"Kwa kuzingatia haya ninakataa pingamizi lililoibuliwa na walalamikiwa na ninalitupilia mbali," amesema Jaji Nongwa.
Baada ya uamuzi huo Jaji Nongwa ameelekeza kesi hiyo iendelee kusikilizwa na tayari shahidi wa kwanza wa upande wa walalamikaji katika kesi hiyo ameshaitwa na kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake.