Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya kina Mdee yapangiwa Jaji, tarehe

Muktasari:

  • Kesi ya waliokuwa wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18, ya kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho imepangwa kusikilizwa na Jaji Cyprian Mkeha.

Dar es Salaam. Kesi ya waliokuwa wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18, ya kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho imepangwa kusikilizwa na Jaji Cyprian Mkeha.

Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kuwavua uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).

Walifungua kesi hiyo Julai 21 mwaka huu siku 13 baada ya kupata ridhaa ya mahakama hiyo.

Wakili wa kina Mdee Ipilinga Panya, amelieleza Mwananchi leo Jumanne, Julai 26, 2022 kuwa wamepokea hati ya wito wa kufika mahakamani Ijumaa Julai 29, 2022 huu kwa ajili ya maelekezo muhimu.

“Kwa hiyo kesho tutawa-serve (tutawapelekea- hati ya wito) respondents (wadaiwa) yaani Chadema, AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na (Tume ya Taifa ya Uchaguzi)Nec.”, amesema wakili Panya.

Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, Mdee na wenzakeo wanaowakilishwa na mawakili  Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashi, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza  kisha itoe amri tatu.

Amri hizo ni ya kutengua mchakato na uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama (certiorari order),  kukilazimisha Chadema kutimiza wajibu wake kisheria (mandamus), yaani kuwapa haki ya kusikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitokana na rufaa walizozikata kina Mdee kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu, Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, bila ridhaa ya chama.