Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kina Mdee wafungua kesi, wadai kutishwa Chadema

Muktasari:

  • Hatimaye wabunge 19 wa viti maalumu waliokuwa wanachama wa Chadema, wamefungua shauri kupinga kuvuliwa uanachama huku miongoni mwa hoja zao ni kutokupewa haki ya kusikilizwa na vitisho.

Dar es Salaam. Hatimaye wabunge 19 wa viti maalumu waliokuwa wanachama wa Chadema, wamefungua shauri kupinga kuvuliwa uanachama huku miongoni mwa hoja zao ni kutokupewa haki ya kusikilizwa na vitisho.

Wabunge hao, wakiwamo Halima Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo jana Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kuwavua uanachama.

Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, wabunge hao wanaowakilishwa na mawakili Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashi, wanaiomba mahakama ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza kisha itoe amri tatu.

Amri hizo ni kutengua mchakato na uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama, kukilazimisha Chadema kutimiza wajibu wake kisheria, yaani kuwapa haki ya kuwasikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua mpaka malalamiko yao yatakapoamuliwa.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu Chadema ulitokana na rufaa walizozikata wabunge hao kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu, Novemba 27, 2020 iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama.

Katika shauri hilo, pamoja na mambo mengine wabunge hao wanadai mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki, wakidai hawakupewa haki ya kusikilizwa.

Kwa mujibu wa kiapo cha Mdee ambacho kwa asilimia kubwa kina maelezo na taarifa zinazofanana na za wengine 18, anadai baada ya kula kiapo cha ubunge, Novemba 24, 2020, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alimtaja yeye na wenzake kama wasaliti.

Anadai Mnyika alikwenda mbali alipowaalika wanachama wa Chadema na umma kwa jumla kutoa mapendekezo kuhusu vikwazo dhidi yao na hata kabla hajapewa barua au maelezo ya makosa yake na nafasi ya kusikilizwa na Kamati Kuu, kitendo kilichojenga uadui dhidi yake na kuhatarisha usalama wake.

Mdee anadai Novemba 25, 2020 Chadema walimtumia barua ya maelezo ya makosa yake kupitia mtandao wa Whatsapp na kumtaka ahudhurie kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika Novemba 27, 2020, ikiwa ni taarifa ya siku mbili tu.

Kwamba kutokana na hasira na vitisho vya usalama wake kutokana na kauli za Mnyika kwa umma, matokeo yake wanachama wa Chadema walianza kutoa vitisho kwa kiwango cha kushutumiwa na hata kuitwa Covid-19. Mdee anadai kutokana na hayo aliingiwa na hofu ya kushambuliwa na wanachama wa Chadema waliochochewa na kauli za viongozi wa Chadema, akiwemo Mnyika.

Hivyo anadai kutokana na hofu hiyo, aliiandikia Kamati Kuu akiomba ahirisho la kikao hicho na kuongezewa muda.

Mei 12, wabunge hao walikwenda kufungua maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiomba kibali cha kufungua kesi ya kupinga kufukuzwa kwao, lakini ilitupiliwa mbali kutokana na kasoro za kisheria.