ACT Wazalendo yamjibu Rais Samia kuhusu amani, utulivu

Muktasari:
- Chama cha ACT Wazalendo kimesema msingi wa amani na utulivu ni haki.
Shinyanga/Mbeya. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema ili kupatikane amani na utulivu nchini, Serikali haina budi kuzingatia utendaji haki kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Kauli ya Dorothy inajibu kilichoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa hema la Kanisa la Arise and Shine, aliposisitiza kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini.
"Zaidi ya yote, niwasihi tuendelee kuliombea Taifa letu ili lidumu katika umoja, amani, utulivu na mshikamano kama tulivyo," alisema Rais Samia akirejea ripoti ya Global Peace Index iliyoitaja Tanzania kuwa kinara wa amani Afrika Mashariki.
Wakati Dorothy akiyasema hayo, mtia nia ya ubunge wa Shinyanga kupitia chama hicho, Emmanuel Ntobi, amesema jawabu la changamoto zote za haki nchini litapatikana kwa wananchi kufanya uamuzi wa kubadilisha watawala.
Katikati ya hayo, Dorothy amedokeza kuwa chama hicho kimeandaa wagombea bora watakaokwenda kwenye uchaguzi kupigania maslahi ya Watanzania.
Viongozi hao wamesema hayo jana, Jumapili Julai 6, 2025, katika hotuba zao kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wakati wa mkutano wa hadhara, ikiwa ni siku ya saba ya ziara ya Operesheni Majimaji Linda Kura inayofanyika kwa siku 30.
Katika hotuba yake, Dorothy amerejea kauli ya Rais Samia ya Jumamosi, Julai 5, 2025, kwenye uzinduzi wa kanisa hilo, alipotaka amani na utulivu, akisema yote hayo yatapatikana iwapo haki itazingatiwa.
“Sisi tunamwambia Rais Samia, amani haitakuwepo, wala utulivu bila haki. Haki lazima ijengeke na ionekane imetendeka ili kuwepo amani. Ili kuwepo amani lazima kutendwe haki,” amesema.
Kwa upande wa Ntobi, amesema jawabu la changamoto zote za haki na mambo mengine ni wananchi kufanya uamuzi wa kubadili viongozi na kutoa nafasi kwa wagombea wanaotokana na ACT Wazalendo.
Katika msisitizo wa hoja yake hiyo, kada huyo ambaye pia ni Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amegusia aliyoyafanya alipokuwa Diwani wa Ngokolo mkoani humo, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara na huduma, ingawa alikabiliwa na vikwazo lukuki.
Kwa dhamira ileile ya kuwatumikia wakazi wa Shinyanga, amesema ndiyo maana amehama Chadema, ambayo imejitenga kushiriki uchaguzi, na kujiunga na ACT Wazalendo kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.
Ametumia jukwaa hilo kueleza kuwa Tanzania kwa sasa inapita katika nyakati ngumu za kisiasa kutokana na mgawanyiko wa pande tatu, kati ya wanaokubali kushiriki uchaguzi, wanaopanga kuuzuia na wale wasioelewa lolote.
“Hawa wasioelewa wanaona siasa ni ya wanasiasa, wakati siasa ndiyo kila kitu na ndiyo inayotupangia kila kitu. Kwa hiyo siasa ni kwa ajili ya kila mtu wa kila chama,” ameeleza.
Amesema katika nyakati hizi, ni muhimu kwa kila raia ajiulize ni nani atakayemchagua akamwakilishe kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo.
Ntobi amesema ni sawa kwa yeyote aliye katika upande wowote kati ya hizo, ingawa wanaosusa wanapaswa kujiuliza watafanya hivyo hadi lini.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Issihaka Mchinjita, ameeleza kushangazwa na hatua ya Mkoa wa Shinyanga kuwa wa nne kwa kuchangia katika Pato la Taifa, lakini ukiwa miongoni mwa mikoa sita ambayo watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini.
Mchango wa Shinyanga katika Pato la Taifa ni Sh7.5 trilioni, ikiwa chini ya mikoa ya Mbeya, Mwanza, na unaoongoza ni Dar es Salaam.
Mchinjita amesema hatua hiyo ni ithibati kuwa watawala wameshindwa kutimiza ahadi na malengo ya kuwainua wananchi kiuchumi na kujenga ustawi wa jamii.
“Kwa hiyo mchango wenu katika (Pato la Taifa) ni mkubwa lakini ninyi ni kati ya watu maskini sana. Mwaka jana wakati Rais Samia Suluhu Hassan anakuja kuzima mbio za Mwenge, alitangaza mikoa inayoongoza kwa utapiamlo na Shinyanga haikusalimika,” amesema.
Hatua ya kuishi chini ya mstari wa umasikini, amesema, inamaanisha watu hao hawana uwezo wa kupata Sh1,700 kwa siku na wastani wake ni asilimia 30 ya wakazi wa mkoa huo.
Wakati huo huo, Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe aliyekuwa mkoani Mbeya kwa ziara hiyo, amewaambia wananchi wa Mbarali mkoani humo kuwa njia pekee ya kuondokana na mgogoro wa ardhi unaohusisha hifadhi za Taifa, mipaka na wawekezaji ni kuchagua upinzani hususan ACT Wazalendo.
“Sina jipya nitakalolizungumza kwenu. Nimekuja mara kadhaa hapa. Mara ya mwisho mwaka 2024. Nafahamu changamoto kubwa ya watu wa Ubaruku na Mbarali nzima ni ardhi. Tunafahamu changamoto zilizosababishwa na G28 ya mwaka 2008.
“Mgogoro wa ardhi haupo Mbarali pekee yake. Kila sehemu ya nchi kuna changamoto hii. Hii imesababishwa na sera mbovu za chama tawala na kosa kubwa ni kuwepo kwa Bunge la chama kimoja. Hakuna anayewatetea,” amesema Zitto.
Amesema endapo chama hicho kitashika madaraka Oktoba 2025, watahakikisha ardhi yote iliyoporwa na kupewa wawekezaji itarejeshwa kwa wananchi.
“Tutapitia upya mipaka ya hifadhi na vijiji, ikiwemo tatizo lenu la GN. Kazi ya kumaliza mgogoro wa ardhi ndogo sana. Tupeni hii kazi sisi. Tutapitia upya mipaka yote kati ya hifadhi na vijiji, na tutaunda tume itakayopita vijiji vyote ili kuondoa migogoro,” amesema Zitto.