Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo: Mapambano hayahitaji kutundika daruga

Muktasari:

  • Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hakioni sababu ya kususia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, lakini kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi.

Mbeya. Chama cha ACT-Wazalendo kimesisitiza kuwa mapambano dhidi ya watawala si ya muda mfupi, bali ni safari ya muda mrefu inayohitaji uvumilivu na msimamo thabiti.

Kimevitaka vyama vya upinzani kutokata tamaa wala kutolegeza juhudi, bali kuendelea kushikamana na kuendeleza mapambano hadi pale haki, usawa na demokrasia ya kweli vitakapopatikana.

Hayo yamebainishwa na kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Zitto na viongozi wengine wa ACT Wazalendo wapo kwenye ziara ambayo jana imeingia siku ya nne yenye lengo la kuwajengea uwezo wananchi kuhusu ‘operesheni majimaji linda kura' itakayodumu kwa siku 15. Katika ziara hiyo, ACT Wazalendo inaueleza umma  sababu za kushiriki uchaguzi mkuu.

"Haya ni mapambano ambayo wewe utayafanya kwa wakati wako, kisha wengine ili lile lengo mlilokusudia lifikiwe. Hii ndio kazi ambayo ACT Wazalendo tunaifanya ya kuwaunganisha na kuwahamasisha Watanzania mkapige kura.

"Kura yako ina thamani lakini kuna wenzetu wameteswa na saikolojia ya kwamba CCM haiwezi kuondoka madarakani au haiwezi kushindwa majimbo au kata, wanaona ni bora kuacha," amesema Zitto.

Zitto amesema ACT Wazalendo kinawaambia wananchi wa Tukuyu, Mbeya na Watanzania kuwa ni dhambi kususia uchaguzi mkuu bali kushiriki na kuendeleza mapambano ili kuhakikisha kuwa siku moja tutafanikiwa.

"Mwananchi wa Rungwe, Tukuyu, Mbeya na Mtanzania kura yako ina thamani na uwezo wa kumchagua kiongozi unayemtaka kuanzia mwenyekiti wa kijiji, mtaa,  kitongoji, diwani, mbunge hadi Rais.

"Hakuna uchaguzi ambao mpinzani ameshinda ubunge au udiwani kirahisi ni mapambano, marufuku kukata tamaa twendeni tukashiriki uchaguzi tuondoe CCM," amesema Zitto ambaye amewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini kwa miaka 15.

Mwanasiasa huyo, amedai kuwa CCM kwa kutumia mbinu mbalimbali kimefikisha mahala ambapo watu wanasalimu amri, kwamba upinzani hauwezi tena kushinda uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Zitto amewataka wananchi wa Tukuyu kukiunga chama hicho mkono kuanzia katika udiwani, ubunge na urais ili kutatua changamoto zinawakabili za bei ya zao la chai, kahawa na huduma za kijamii.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma  na Waziri Kivuli wa Fedha wa chama hicho, Kiza Mayeye amesema ni wakati wa mwafaka wa Watanzania kuiweka CCM pembeni ili kutoa fursa kwa upinzani kuongoza nchi.

"Hatukuja hapa kushangilia la hasha bali siasa ni maisha, wananchi wanahitaji huduma bora za jamii. Hatusemi kwa sababu tunawachukia CCM, bali wameshindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, tuungeni mkono ili tukasimamie maisha ya Watanzania," amesema Mayeye.

Mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo, Halima Nabalang'anya amewaambia wananchi Mbeya, "twendeni tukapige kura msikate tamaa, msisikilize manenomaneno kwamba hata mkipiga kura watashinda... tukapige kura tusisuse...," amesema Nabalang'anya.

Naibu Katibu wa ACT Wazalendo (Bara), Ester Thomas amesema chama hicho kimejikita katika msimamo wa masilahi ya wote na si wachache, ndio maana inatoa fursa ya watu wa makundi mbalimbali kwenye nafasi za uongozi.