Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli Bunge sio chombo cha machawa yazua majibizano

Muktasari:

  • Mjadala umeibuka baada ya kauli ya Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kutaka bunge liheshimiwe na sio kuwa chombo cha machawa.

Bariadi. Mnyukano wa hoja umeibuka, baada ya kauli ya Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliyetaka bunge lisidogoshwe kwa kuonekana ni chombo ambacho hata machawa na wachekeshaji wanapaswa kwenda kukitumikia.

Kauli hiyo imemuibua Mchekeshaji, Clayton Chipando maarufu Babalevo aliyesema Zitto ametoa kauli hiyo kwa sababu amemwona amechukua fomu ya kuwania ubunge Kigoma Mjini kwa tiketi ya CCM.

Babalevo ambaye aghalabu hujinasibisha na uchawa, amekwenda mbali zaidi na kusema, Zitto anasema hayo kwa sababu amekosa mazuri ya kuzungumza kwani alipopewa nafasi ya ubunge wa Kigoma Mjini, hakuna jema alilofanya.

Hoja za wawili hao, zimemuibua Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo aliyemshukia Babalevo, akimtaja kuwa mwanasiasa anayetaka nafasi asiyoistahili na kusisitiza, hilo linathibitika na uongozi wake alipokuwa Diwani wa Mwanga Kaskazini mkoani Kigoma, aliwatelekeza wananchi na kwenda kuishi Dar es Salaam.


Ilivyoanza

Yote hayo, yalianzia na kauli ya Zitto ya Julai 3, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Tabora, alipotahadharisha bunge kudogoshwa kiasi cha kwamba hadi machawa na wachekeshaji wanaona ni mahala pa kwenda.

"Bunge linadogoshwa, kwamba limekuwa eneo la machawa au la wachekeshaji, au ni la mtu yeyote anayetaka kwenda," alisema Zitto katika hotuba yake mbele ya wananchi wa Tabora.

Msisitizo wa Zitto katika hoja hiyo ni Bunge kupewa hadhi yake, kwa kuwa ni chombo cha kutunga sheria na kinawawakilisha wananchi, lisichukuliwe kuwa chombo ambacho kila mmoja anaweza kufanya anavyotaka.

"Uliofanyia utani bunge utakuwa umefanyia utani uhai wa Taifa, ili kuhakikisha mihimili huu haufanyiwi utani, watu wa Tabora pamoja na hasira mlizonazo, machungu mliyonayo au kukata tamaa, pigeni moyo konde twendeni kwenye uchaguzi, mkachague watu sahihi," amesema.

Hayo yamemuibua Babalevo, aliyejirekodi katika kipande cha picha jongefu, akisema anajua maneno yote yanayosemwa ni kwa sababu amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania ubunge Kigoma Mjini kupitia chama chake cha Mapinduzi (CCM).

"Mtasemwa sana (wachekeshaji na machawa) haitoishia hapo, mimi nawaomba radhi na Mungu akijaalia nitawanyooshea huyu mtu (Zitto). Huyu mtu yeye ndio chawa kuliko sisi wote na nina ushahidi wa kutosha," amesema.

Babalevo amedai aliwahi kuambatana na Zitto kwenda kufanya uchawa kwa matajiri zaidi ya 13 kwa ajili ya kupewa fedha za kufanyika mikutano na mafuta kwenye magari.

"Ningemwambia yeye ndugu yangu, angeenda kwenye mikutano ya hadhara kuelezea namna alivyopewa miaka mitano na chama chake kuongoza Kigoma Mjini, alifanya nini. Angeenda kufika Tabora anawaambiwa nilifanya moja, mbili tatu.

"Na sio mchekeshaji, sio mburula kwamba hajasoma, amesema na mashahada, alifanya nini alivyopewa nafasi kwenye Jimbo la Kigoma Mjini, ndiyo maana anahaha," amesema.


Nondo aibukia

Akiwa katika Kijiji cha Sapiwi Sokoni wilayani Bariadi katika Mkoa wa Simiyu, leo, Jumamosi, Julai 5, 2025, Nondo amemjibu Babalevo akisema, amekosa hata uhalali wa kuzungumza maneno hayo kwa kuwa hana anachojua kuhusu nafasi anayoiomba.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo

"Hatuwatengi wachekeshaji wala (Zitto) hakuwa na maana kwamba wachekeshaji hawawezi kuwa viongozi, wanaweza. Lakini wachekeshaji gani, wale wenye mizaha hawafai," amesema.

Amesema hilo linathibitishwa na kile alichofafanua, Baba Levo hata alipokuwa diwani, hakuna alichokifanya kwa sababu aliwatelekeza wananchi wake kwa kukimbilia kuishi Dar es Salaam.

"Alipokuwa diwani hakuwa anafanya chochote zaidi ya kuwakimbia wananchi wake, alikuwa diwani katika Kata ya Kigoma, lakini anaishi Dar es Salaam, anautaka ubunge atauweza?" amehoji Nondo.

Sambamba na hilo, Nondo amesema Babalevo amesikika hata katika moja ya chombo cha habari akishindwa kujibu baadhi ya maswali ya msingi kuhusu uongozi, jambo linalothibitisha hana uwezo wa kuongoza.

"Anaulizwa kuhusu mihimili ya nchi, anasema Mahakama, Bunge na Baraza la Mawaziri, badala ya Serikali, huyu ataweza kuwa Mbunge?" amehoji.

Amesema kwa namna anavyoona, hadhani hata mamlaka zinazopitisha wagombea ndani ya CCM watampitisha kwa kuwa hana vigezo vya kuwa Mbunge hasa wa Kigoma Mjini.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kuhusiana na alichokisema Nondo, Babalevo amesema kwa kuwa si kazi ya mbunge kujibu maswali, hana sababu ya kujua vile vinavyodaiwa kuwa amekosea.

Amesema anachojua kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi wa jimbo atakalochaguliwa, kuhakikisha wanapata maendeleo.

"Hivi anajua kazi ya mbunge huyo? Si kazi ya mbunge kujibu maswali ya maana ya muswada, kazi ya mbunge ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wake na naiweza," amesema.



Ntobi azungumza

Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa chama hicho, Emmanuel Ntobi amesema uamuzi wake wa kujiunga na chama hicho, umetokana na kujua kuwa kipo mstari wa mbele wa kuendesha mapambano ya kuwapigania Watanzania.

Amesema ameachana na Chadema kwa sababu kimejiondoa kushiriki uchaguzi ilhali ndilo jukwaa ambalo chama cha siasa kinapaswa kupambana.

"Niwaombe kwa kipindi kilichobaki, njooni tuunganishe nguvu tuwaondoe CCM madarakani," amesema.

Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Peter Madeleka amesema wanaodai chama hicho kimesaliti kwa kushiriki uchaguzi, wamekosa hoja.

Amesema ni muhimu kushiriki uchaguzi kwa kuwa Tanzania ina matatizo mengi na wakati wote wamekuwa wakipambama kuyakabili bila kususa.