Prime
Mitihani mitano kwa kocha mpya Yanga

Muktasari:
- Yanga imemaliza msimu na pointi 82, ikishinda mechi 27, sare moja na kupoteza miwili kati ya 30 iliyocheza, ikitwaa taji la 31, la Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku likiwa ni la nne mfululizo kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025.
Dar es Salaam. Mabosi wa Yanga kwa sasa wako katika mchakato wa kusaka kocha mpya atakayeinoa timu hiyo kwa msimu ujao, baada ya Miloud Hamdi aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, kuondoka na kujiunga na Ismaily SC ya Misri.
Yanga imemaliza msimu na pointi 82, ikishinda mechi 27, sare moja na kupoteza miwili kati ya 30 iliyocheza, ikitwaa taji la 31, la Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku likiwa ni la nne mfululizo kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025.
Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa huku akiwa na leseni A ya UEFA, alitua nchini kujiunga na Singida Black Stars, Desemba 30, 2024, ingawa hakuiongoza hata mechi yoyote hadi Yanga ilipoinasa saini yake rasmi, Februari 4, 2025.
Kocha huyo, alitambulishwa Yanga baada ya kuondoka kwa Mjerumani, Sead Ramovic aliyejiuzulu mwenyewe, Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, tangu atambulishwe kikosini humo Novemba 15, 2024, akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini.
Sasa wakati Hamdi akiondoka, mabosi wa Yanga wameanza mchakato wa kusaka mbadala wake huku ikielezwa wanaiwinda saini ya Kocha, Mfaransa Julien Chevalier anayemalizia mkataba wake na kikosi cha ASEC Mimosas ya Ivory Coast ili kutua nchini.
Mwingine ni Rhulani Mokwena aliyezifundisha, Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates na Chippa United zote za Afrika Kusini na Wydad Casablanca ya Morocco, japo atakayekabidhiwa kibarua hicho kati ya makocha hao atakabiliwa na mitihani mizito.
Kutetea makombe
Moja ya mtihani mkubwa utakaomkabili kocha mpya wa Yanga ajae, ni pamoja na kuchukua mataji mbalimbali kama ilivyofanya msimu wa 2024-2025, ilipochukua Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la (FA) na Kombe la Muungano la mwaka 2025.
Shauku ya Yanga ni kuona inaendelea kufanya vizuri katika michuano ya ndani kwa kuteta mataji yake yote iliyochukua kwa msimu ujao, jambo linaloonyesha wazi kocha atakayekabidhiwa pia kikosi hicho atakuwa na kazi kubwa ya kufanikisha hilo.
Ubabe kwa Simba
Licha ya kutwaa mataji hayo, ila jambo lingine ambalo mashabiki wa Yanga wanajivunia kwa sasa ni kuendeleza ubabe kwa wapinzani wao wakubwa hapa nchini Simba, kitu ambacho kocha ajaye atapimwa pia kupitia pambano hilo la 'Kariakoo Derby'.
Katika Ligi Kuu Bara, Yanga imeshinda mechi nne mfululizo dhidi ya Simba, ambapo pambano la mwisho la Juni 25, 2025, la msimu huu, ndilo lililoipa ubingwa wa 31, tangu mwaka 1965, hivyo kusubiriwa kuona kocha mpya ajaye ataendeleza au laah!
Ushindani
Mtihani mwingine kwa kocha mpya wa Yanga ni kupambana na makocha wenzake wazoefu, ambaye mbali na Fadlu Davids wa Simba, ila wengine ni aliyekuwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi atakayeifundisha Singida Black Stars na Florent Ibenge wa Azam FC.
Fadlu ameiongoza Simba kumaliza Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa ya pili na pointi 78, ikishinda 25, sare tatu na kupoteza miwili, huku akiifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kukosa ubingwa mbele ya RS Berkane ya Morocco.
Kocha huyo ameifikisha Simba fainali baada ya miaka 32, tangu iliposhiriki mwaka 1993 michuano ya CAF, ambapo msimu huu, ilichapwa jumla ya mabao 3-1, kufuatia kupoteza ugenini 2-0, Mei 17, 2025, kisha marudiano ikatoka sare ya 1-1, Mei 25, 2025.
Kwa Gamondi ni kocha mzoefu aliyerejea tena kujiunga na Singida Black Stars baada ya kuondoka Yanga Novemba 15, 2024, huku akiipa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, Kombe la Shirikisho la (FA) na Ngao ya Jamii mwaka 2024.
Mwingine ni Ibenge aliyetambulishwa Azam FC Julai 5, 2025, akichukua nafasi ya Rachid Taoussi raia wa Morocco, ambapo Mkongomani huyo amejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, baada ya kuondoka Al Hilal ya Sudan.
Katika kipindi cha misimu mitatu aliyoitumikia Al Hilal, Ibenge ameiongoza kwenye jumla ya mechi 91, ambapo kati ya hizo ameshinda 55, sare 20 na kupoteza 16, huku kikosi hicho kikifunga mabao 158 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 62.
Ibenge ameiwezesha Al Hilal kushinda taji la Ligi Kuu ya Sudan, Kombe la Ligi 'Sudan Super League' na ubingwa wa heshima wa Ligi Kuu ya Mauritania iliyoshiriki msimu huu wa 2024-2025, kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyokuwepo kwao Sudan.
Uzoefu wa makocha hao, unazidi kuongeza ushindani msimu ujao wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mashindano yote ya ndani, jambo linaloongeza mvuto na msisimko mkubwa, kutokana na wasifu waliokuwa nao na ubora wa wachezaji wa timu hizo.
Ligi ya Mabingwa
Licha ya Yanga kufanya vizuri michuano ya ndani na kutwaa mataji yote, ila msimu wa 2024-2025, imefanya vibaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kikosi hicho kushindwa kutamba kufuatia kutolewa mapema tu kwenye hatua ya makundi.
Msimu huu wa 2024-2025, Yanga ilipangwa kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo ilimaliza ya tatu na pointi nane, nyuma ya Al Hilal iliyofundishwa na Ibenge aliyetua Azam FC, aliyeiongoza hadi robo fainali na kutolewa na Al Ahly ya Misri.
Ibenge aliiongoza Al Hilal kumaliza kinara wa kundi hilo na pointi 10, nyuma ya MC Alger ya Algeria iliyoshika nafasi ya pili na pointi tisa, huku TP Mazembe ya DR Congo ikiburuza mkia na pointi tano, jambo linaloipa Yanga mtihani mwingine.
Kikosi bora
Kipindi hiki kumekuwa na wachezaji mbalimbali wanaohusishwa kuondoka Yanga na wengine kuingia, ingawa kocha mpya ajaye atakuwa na kazi kubwa ya kufanya, ili kutengeneza kikosi bora kitakachoweza kuleta ushindani katika michuano tofauti.
Miongoni ni mshambuliaji, Clement Mzize anayetajwa huenda pia akaondoka baada ya kufanya vizuri msimu huu akifunga mabao 14 ya Ligi Kuu Bara, akiwa ni mzawa aliyefunga mengi zaidi, huku hatima ya Stephane Aziz KI ikiwa bado ni kitendawili.
Aziz KI aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco hivi karibuni, inaelezwa alijiunga na kikosi hicho kwa mkopo na ikiwa mabosi watamuhitaji watabidi kuilipa Yanga hadi mwisho Julai 10, 2025, bali ikishindikana atarejea nchini kuendelea nao.
Kiungo huyo mshambuliaji aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2023-2024, baada ya kufunga mabao 21, amekuwa ni nguzo muhimu ya Yanga, hivyo kama hatorudi itakuwa kazi kwa mabosi wa timu hiyo kusaka mbadala atakayevaa viatu vyake.
Licha ya uwepo pia wa nyota wengi wanaoweza kuziba nafasi yake wakiwemo, Clatous Chama na Pacome Zouzoua, ila hadi sasa bado hakuna muafaka uliofikiwa kama watabakia tena msimu ujao, baada ya mikataba yao kumalizika msimu huu wa 2024-2025.
Msikie kocha aliyeondoka
Baada ya kuondoka Yanga, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miloud Hamdi alinukuliwa akisema malengo yake makubwa yalikuwa ni kubakia msimu ujao, japo bado anaamini kikosi hicho kitafanya vizuri kutokana na ubora wa wachezaji aliowaacha kikosini.
"Naamini Yanga inaweza kufanya vizuri msimu ujao kwa sababu ya wachezaji waliopo, wanakupa kila unachohitaji kama kocha kwa sababu wanatambua malengo ya timu kubwa ni kutwaa mataji, sina wasiwazi wowote kutokana na hilo," anasema Miloud.