Kesi ya kina Sabaya yaahirishwa tena

Aliyekua Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imeahirisha tena kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne kutokana na upelezi kutokamilika.

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imeahirisha tena kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne kutokana na upelezi kutokamilika.

Sabaya na wenzake leo Julai 4, 2022 wamefikishwa kwa mara ya nne katika mahakama hiyo kujibu tuhuma zinazowakabili katika kesi namba 2 ya uhujumu uchumi ya mwaka 2022 lakini kesi hiyo imeahirishwa tena.

Kesi hiyo inayoendeshwa na wakili wa upande wa Jamuhuri, Kasimu Daudi pamoja na Sabitina Mcharo imehairishwa hadi hapo Julai 14, 2022 kutokana na upelezi wa kesi hiyo kutokamilika.

Wakili wa Serikali Kasimu Daudi ameieleza mahakama hiyo kuwa bado upelelezi haujakamilika na pia wanasubiri hati ya kuipa mahakama hiyo uwezo wa kuisikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP.

Sabaya na wenzake wanne wanakabiliwa na mashitaka mbalimbali likiwemo ya uhujumu uchumi na kijipatia Sh30 milioni kutoka kwa mfanyabiashara wa Bomang'ombe wilayani Hai, Alex Swai ambaye alidai kukwepa kodi.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.

Hata hivyo  wakili upande wa washtakiwa Heleni Mahuna amesema hana pingamizi na ahirisho hilo na kuwataka upande wa Jamuhuri kulichukulia suala hilo kwa uzito ili washtakiwa wajue ni nini hatma yao na haki iweze kupatikana.

"Washtakiwa wanaendelea kuteseka rumande bila kufahamu ni lini shtaka lao litasikilizwa na hatma ya maisha yao, tunaomba upande wa Jamuhuri walichukulie suala hilo kwa uzito." amesema  wakili wa Mshatikiwa Helen Mahuna.

Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo, Salome Mshasha amesema amesikiliza hoja za pande zote na kuwataka upande wa Jamuhuri kuharakisha upelezi wa kesi hiyo.

"Shahuri hilo lipo chini ya Serious offences, tuendelee kusisitiza upande wa Jamuhuri kukamilisha upelelezi, na kwa leo pia tunahairisha kesi hii hadi hapo Julai 14 mwaka huu" amesema Hakimu Salome.