Kesi ya Malkia wa meno ya tembo yapigwa kalenda

Muktasari:

Watuhumiwa watatu wanadaiwa kupanga na kutekeleza biashara hiyo


Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66), anayedaiwa kuwa ni malkia wa Pembe za Ndovu, imeshindwa kuendelea na ushahidi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Leo Jumatano Septemba 5, 2018 wakili wa Serikali,  Mwanamina Kanakomba amedai mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe fupi ili iweze kuendelea na ushahidi.

“Kesi hii ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa terehe nyingine ili iweze kuendelea na ushahidi , hivyo tunaomba mahakama ipange terehe fupi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi” amedai Kanakomba.

Baada ya maelezo hayo  wakili wa utetezi, Jeremia Mtobesya amekubaliana na upande wa mashtaka na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe fupi  kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, 2018 itakapoendelea na ushahidi.

Mbali na malkia wa tembo, washtakiwa wengine ni Salvius Matembo na Philemon Manase, wanadaiwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo ya thamani ya Sh13 bilioni, kinyume cha sheria.

Tayari mashahidi zaidi ya kumi wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.

Wanadaiwa  kati ya Januari Mosi, 2000  na Mei 22, 2014 walijihusisha na biashara  ya nyara za Serikali.

Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889 zenye thamani ya Sh 5.4 bilioni  bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014  kwa makusudi raia wa China, Yang Feng Glan aliongoza na kufadhiri vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 706 vya Meno ya Tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Pia, washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za Serikali kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno ya tembo kwa nia ya kujipatia faida.

Imedai kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za Serikali.

Soma Zaidi: