Kesi ya Sabaya kuendelea leo

Muktasari:

  • Sabaya na wenzake wanadaiwa kutenda kosa la kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo imepanga kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.

Juzi, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wa Serikali waandamizi, Felix Kwetukia, Ofmed Mtenga na Wakili wa Serikali Neema Mbwana, mbele ya Hakimu Patricia Kisinda.

Upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Fridolin Gwemelo, Edmund Ngemela na William Alexander.

Juzi, akitoa ushahidi Philemon Kazibila (64) aliiambia Mahakama kuwa vijana wawili waliokuwa na Sabaya walifika ofisini kwake na kujitambulisha kuwa ni maofisa usalama.

Kazibila ambaye ni shahidi wa nne wa Jamhuri alisema hayo wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili Ofmed Mtenga.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la kwanza la kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha na washtakiwa wote wanadaiwa kujipatia Sh90 milioni huku wakijua kuwa kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, la tatu na la nne linalomhusu Sabaya pekee, anadaiwa kujihusisha na rushwa.

Pia, anadaiwa kuchukua Sh90 milioni na kufanya kosa la matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.