KESI YA UHAINI 1985: Mtoto wa Ngaiza atoa ushahidi, aeleza uhusiano na Lugangira-40

KESI YA UHAINI 1985: Mtoto wa Ngaiza atoa ushahidi, aeleza uhusiano na Lugangira-40

Muktasari:

  • Shahidi huyo alionyeshwa moja ya karatasi mbili alizodai kuwa mojawapo aliikuta ikiwa ni anwani za nchi za nje na akatakiwa aseme ikiwa karatasi hiyo ilikuwa na anwani ya Marekani na aliposhindwa kuiona hiyo anwani ya nje, aliulizwa: “Hapo kuna neno MZA, kwani hiyo ndiyo USA kwa mawazo yako?”

Shahidi huyo alionyeshwa moja ya karatasi mbili alizodai kuwa mojawapo aliikuta ikiwa ni anwani za nchi za nje na akatakiwa aseme ikiwa karatasi hiyo ilikuwa na anwani ya Marekani na aliposhindwa kuiona hiyo anwani ya nje, aliulizwa: “Hapo kuna neno MZA, kwani hiyo ndiyo USA kwa mawazo yako?”

Konstebo James: Sioni.

Alipojibu hivyo, Jaji Kiongozi Nassor Mzavas alimuuliza: Je, unajua kusoma?

Konstebo James: Ndiyo.

Jaji Kiongozi: Umesoma mpaka (darasa) la ngapi?

Alipojibu kuwa amesoma mpaka darasa la saba, Jaji Kiongozi alimtaka asome karatasi hiyo lakini hakuweza kufanya hivyo na kusema “siwezi.”

Tarimo: Na umeiambia mahakama kuwa mlipokuwa kweye hiyo nyumba hapo Mkwajuni saa 1:30 usiku wa Januari 7, mtu mmoja alitaka kupita kwenye nyumba hiyo na Mfalingundi alimkamata. Ya kweli hayo?

Konstebo James: Ndiyo. Alikamatwa wakati alipokuwa amekaribia nyumba yenyewe.

Tarimo: Lakini nikikwambia kuwa mtu huyo alikamatwa si kwa vile alisogelea nyumba yenyewe bali alikuwa akijipitia zake, utasema nini?

James: Kimya

Baada ya Konstebo James kukaa kimya bila kujibu, Jaji Kiongozi aliingilia kati na kusema: “Lakini natumaini mtu sahihi wa kujibu swali hilo ni Mfalingundi mwenyewe.”

Hata hivyo, baada ya Wakili Tarimo kudai kuwa Konstebo James alipaswa kujibu swali hilo kwa vile alidai aliona wakati mtu huyo akitiwa mbaroni, Jaji Kiongozi aliruhusu swali hilo kujibiwa na Konstebo James ambaye alisema: “Mtu huyo alikamatwa wakati aliposogelea nyumba hiyo lakini sikusikia mazungumzo yaliyokuwa kati yake na Mfalingundi kwa vile nilikuwa mbali kidogo.”

Tarimo: Je, ulipata kumwona mtu huyo tena popote pale baada ya hapo?

Konstebo James: Hapana.

Tarimo: Mpaka hivi sasa hujamwona?

Konstebo James: Ndiyo.

Akiulizwa na Sekule tena, Konstebo James alitakiwa aeleze kama alijua kusoma na kuandika na alisema kuwa alikuwa amemaliza darasa la saba na hivyo alijua kusoma na kuandika.

Sekule: Tayari umeshasema kuwa baada ya kumkamata Metusela na kumpekua, moja ya karatasi ulizozikuta mfukoni mwake ilikuwa ni anwani ya nchi za nje kama vile USA. Sasa hebu tazama karatasi hii (akionyeshwa hiyo karatasi) unaweza kusoma kilichoandikwa hapo?

Konstebo James: Nashindwa kusoma.

Sekule: Lakini wewe unasema unajua kusoma. Sasa imeandikwa A.B.C.D...?

Konstebo James: Imeandikwa Sweden.

Sekule: Sasa Sweden ni nini?

Konstebo James: Ni nchi.

Sekule: Iko wapi? Ni sehemu ya nchi gani hiyo Sweden?

Konstebo James: Ni nchi ya ng’ambo. Haiko hapa Tanzania.

Sekule: Wakili mwenzangu Mkude alikuuliza nini maana ya RTD kama ilivyoandikwa kwenye ile karatasi nyingine. Je, ulielewa lile neno ‘TO’ lililokuwa limeandikwa baada ya mshale lilikuwa na maana gani?

Konstebo James: Ndiyo. Ninaelewa maana ya hilo ‘TO’ (lakini hakueleza maana yake kwa Kiswahili).

Sekule: Na kama wakili mwenzangu Mkude alivyokuuliza, unadhani karatasi kama hiyo inaweza kuandikwa barabarani?

Konstebo James alipokubali kuwa iliwezekana kuwa hivyo, Sekukle alimuuliza, “lakini umeelewa swali langu?”

Akijibu hoja ya mzee wa pili wa baraza, Lawrence Shelukindo Saguti, ikiwa baada ya Metusela Kamando kutiwa mbaroni alitoa kitambulisho chake yeye mwenyewe, Konstebo James alijibu hapana. “Tuligundua kitambulisho chake baada ya kumpekua na hizo karatasi mbili.”

Baada ya hapo alifuata Shahidi wa 43 wa upande wa mashtaka, Oscar Ngaiza, mtoto wa Chrisopher Ngaiza (mshtakiwa wa 13), alianza kutoa ushahidi wake akieleza jinsi Pius Lugangira alivyoomba kutumia nyumba yao ya Masaki kwa mikutano ya biashara na wateja wake wakati baba yao akiwa safarini Kigali, Rwanda.

Alisema alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1982/83 akisoma masomo ya uhandisi katika Kemia, alikuwa kila akipata likizo yake ya miezi mitatu anaishi kwenye nyumba ya baba yake iliyoko Barabara ya Chole, Masaki, nyumba namba 1127.

Alidai kuwa alikwenda kuishi hapo nyumbani kwa baba yake Desemba 18, 1982 baada ya kupata likizo yake. Na hapo alikuta baba yake akiwa safarini Kigali, Rwanda kwa shughuli za kikazi. Na yeye pamoja na mama yake na ndugu zake wawili waliondoka kwenda Bukoba kabla ya sikukuu ya Krismasi kwa mapumziko.

“Mimi pamoja na mdogo wangu mwingine (hakumtaja jina) tulirudi kwa ndege Desemba 27 na nilimwacha baba na mama wakiwa wanaendelea na mapumziko yao huko Bukoba,” alisema Oscar ambaye wakati kesi ikiwa mahakamani alikuwa akifanya kazi kwenye Kampuni ya Kioo.

Aliongeza, “wakati baba na mama yetu walipokuwa hawapo nyumbani, nilibaki mimi pamoja na ndugu zangu wengine, Flora Lugangira, Stephen Buberwa, Winfred Bogi na mdogo wangu mwingine (hakumtaja jina).

Baada ya kusema hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Johnson Mwanyika, aliuliza: “Unamfahamu mtu mmoja aitwaye Pius Lugangira?

Oscar: Ndiyo. Namfahamu.

Mwanyika: Umemfahamu tangu lini?

Oscar: Nimemfahamu tangu utoto wangu kwa vile ni ndugu yangu wa karibu sana katika ukoo. Mimi humwita kaka yangu.

Mwanyika: Je, mwezi Desemba 1982, ulipata kumwona huyo Pius Lugangira?

Oscar: Ndiyo. Nilimwona.

Mwanyika: Ulimwona wakati gani?

Oscar: Baada ya kurejea kwangu kutoka Bukoba.

Mwanyika: Unakumbuka ilikuwa ni lini?

Oscar: Tarehe 29 Desemba 1982.

Mwanyika: Ilikuwaje mpaka ukamwona?

Oscar: Baada ya kupiga simu kutoka hotelini kwake Motel Agip alifika nyumbani asubuhi kwa ajili ya kuoga kwa vile alisema maji hotelini kwake yalikuwa hayatoki.

Mwanyika: Halafu ilitokea nini baada ya hapo?

Oscar: Alikaa kidogo na hatimaye aliondoka na kwenda zake.

Mwanyika: Ni lini ulipomwona tena?

Oscar: Tarehe 30 Desemba 1982. Siku iliyofuata alikuja nyumbani majira ya asubuhi na siwezi kukumbuka ilikuwa saa ngapi.

Mwanyika: Je, alikuja kuoga tena?

Oscar: Hapana. Alikuja kunifahamisha kuwa alikuwa akikusudia kukutana na wateja wake hapo nyumbani kwa mazungumzo ya kibiashara.

Mwanyika: Na ni kwanini hasa Pius Lugangira alikuambia juu ya huo mkutano?

Oscar: Ni kwa sababu tu alitaka mkutano huo aufanyie hapo nyumbani.

Mwanyika: Halafu kilitokea nini?

Oscar: Alinipa Sh500 au zaidi, siwezi kukumbuka kwa sasa, ili nikanunue bia na pia aliniambia kuwa angenipa fedha nyingine kwa ajili ya chakula.

Alisema baada ya kwenda kununua bia na kurudi nyumbani, alikuta hali ya kawaida wakati Pius Lugangira alipokuwa akizungumza na wenzake kwenye sebule.

Mwanyika: Je, kulikuwamo na watu wangapi kwenye hiyo sebule?

Oscar: Kati ya saba na nane pamoja na Pius mwenyewe.

Alisema yeye hakupata kusikia kile walichokuwa wakizungumza na baada ya kuwaletea vinywaji, yeye alikwenda kusabahiana nao na aliondoka na kuwaacha wakiendelea na mazungumzo yao.

Oscar alisema kuwa aliitwa kwenye gwaride la polisi karibu mara tano au sita ambapo alitakiwa kuwatambua wale ambao walifika nyumbani na kufanya hiyo mikutano pamoja na yule mgeni aliyefika nyumbani kumtafuta Pius Lugangira na aliweza kumtambua kuwa alikuwa ni Kapteni Roderic Rousham Roberts.

Nini kiliendelea? Tukutane toleo lijalo.