Kesi ya uhaini 1985: Washtakiwa tisa wahukumiwa kifungo cha maisha jela- mwisho

Muktasari:

  • Hatimaye siku ya hukumu ilifika baada ya kesi kusikilizwa mahakamani kwa takribani mwaka mzima.

Hatimaye siku ya hukumu ilifika baada ya kesi kusikilizwa mahakamani kwa takribani mwaka mzima.

Desemba 26 Jaji Kiongozi Nassor Mzavas alianza kutoa maelezo ya hukumu ya kesi ya uhaini kwa kuchambua ushahidi wa pande zote za mashtaka na utetezi hadi alipotoa hukumu Jumamosi ya Desemba 28, 1985.

Baada ya kutumia saa tano Desemba 26 kuchambua ushahidi wa pande hizo, Desemba 27, aliendelea kusoma hukumu hiyo wakati Mahakama ilipoendelea na kikao chake.


Kabla ya kuanza kusoma hukumu, Jaji Kiongozi alieleza msingi alioutumia katika hukumu yake kuwa upande wa mashtaka ndio unabidi udhihirishe wazi kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walikubaliana kutenda kosa la uhaini bila shaka.

Alisema ingawa washtakiwa wote wameshtakiwa kwa kosa la pamoja, ushahidi utatafakariwa kwa kila mmoja peke yake na si kwa wote.

Jaji Kiongozi alisisitiza kuwa, jukumu la kudhihirisha hatia liko upande wa mashtaka na hawawezi kutiwa hatiani kutokana na kushindwa kwao kujitetea vizuri.

Alisema ushahidi wa kula njama ulipaswa kuungwa mkono na ushahidi mwingine peke yake.

Pia, alisema yale maungamo ya washtakiwa wenyewe kuwa walikiri kuhusika na mpango huo na papo hapo wakatajana wao wenyewe, yaliweza kuzingatiwa tu na Mahakama iwapo inaamini maungamo kama hayo yalitolewa na washtakiwa kwa hiari zao wenyewe bila kuteswa.

Kwa upande wa ushahidi wa mazingira, Jaji Kiongozi alisema ili kuiwezesha Mahakama kuzingatia ushahidi wa namna hiyo, upande wa mashtaka uliwajibika kudhihirisha kuwa ushahidi kama huo haukuonyesha kitu kingine bali hatia ya washtakiwa wenyewe.

Katika hukumu yake aliyoanza kuisoma Desemba 27 na kuhitimisha Desemba 28, 1985, Jaji Kiongozi alisema ni kweli kulikuwa na njama za kutaka kuiangusha Serikali kama ilivyodaiwa na upande wa mashtaka.

Hata hivyo, Jaji Kiongozi aliahirisha kikao cha Mahakama na kusema atamalizia kuisoma hukumu yake siku inayofuata.

Wakati Mahakama inaahirisha kikao chake, Jaji Kiongozi alikuwa anaanza kuchambua jinsi upande wa mashtaka ulivyoeleza kuhusika kwa kila mshtakiwa.

Hadi kuahirishwa huko, Jaji alikuwa ameshatumia zaidi ya saa 10 kusoma hukumu hiyo ambayo pamoja na uchambuzi ilichukua siku tatu mfululizo.

Baada ya kuchambua ushahidi wa upande wa utetezi kwa washtakiwa saba waliobaki, maelezo ya mwisho ya upande wa utetezi na maelezo ya mwisho ya upande wa mashtaka, Jaji Kiongozi alielezea maoni ya wazee wa baraza na kuanza kutoa maoni yake.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa, ni kweli kulikuwa na njama. Sasa nitaingia katika maelezo ya upande wa mashtaka,” alisema Jaji Kiongozi.

Akianza kutoa maoni yake, Jaji Kiongozi alisema kuwa sababu za njama hizo za kutaka kuangusha Serikali ni kurekebisha hali mbaya ya uchumi iliyokuwapo na kwamba uongozi ndio uliosababisha hali hiyo.

“Shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Abdallah Mhando ambaye ni dereva teksi alisema katika ushahidi wake kuwa aliambiwa hayo na mshtakiwa wa kwanza, Hatty McGhee,” Jaji Kiongozi alisema.

Pia, alisema shahidi aliambiwa na mshtakiwa wa kwanza kuwa hali ya uchumi nchini ilikuwa mbaya, hakuna chakula, barabara mbaya na uongozi ulikuwa mbaya na kwamba kulikuwa na haja ya kuiangusha Serikali na kumuua Rais.

“Sababu zilikuwa ni zile zile za kiuchumi. Hiyo pia ilielezwa na shahidi Luteni Ndejembi,” alisema Jaji Kiongozi.

Luteni Ndejembi alikuwa shahidi wa tatu upande wa mashtaka.

Jaji Kiongozi alisema Luteni Ndejembi alieleza aliwahi kuambiwa sababu hizo na mshtakiwa wa tisa, Luteni Badru Rwechungura Kajaja, walipokutana Novemba 1982. “Luteni Ndejembi aliambiwa kuwa baada ya Serikali kuangushwa, maduka yatajaa bidhaa katika muda wa miezi mitatu tu,” alisema Jaji Kiongozi.

Katika maelezo yake hayo ya hukumu, Jaji Kiongozi alisema hata ushahidi wa shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, Luteni Iddi Stambuli, ulikuwa unahusu sababu za hali ya uchumi.

“Shahidi huyo alisema aliambiwa na mshtakiwa wa pili, Kapteni Christopher Kadego kuwa kulikuwa na mpango wa kuiangusha Serikali kwa kuwa hali ya uchumi ilikuwa mbaya, askari wanakula chakula bila mafuta, hawana nguo, spea za magari hakuna,” alisema Jaji Kiongozi.

“Ilionyesha kuwa nia ilikuwa ni hali mbaya ya uchumi, ushahidi wa shahidi wa 46 wa upande wa mashtaka, Kapteni Suleiman Mape, ulizungumzia hali hiyo.”

Mapema Jaji Kiongozi alikumbusha maoni yaliyotolewa na wazee wa baraza ambao waliona washtakiwa kadhaa wana hatia na baadhi yao hawana hatia.

Jaji Kiongozi alisema washtakiwa ambao mzee wa tatu wa baraza, Anne Kirundu aliwaona wana hatia ni saba wa mwanzo na mshtakiwa wa nane, Kapteni Zacharia Hans Poppe na wa tisa, Luteni Kajaja (kwa kosa la kujua njama na kutotoa ripoti).

Hata hivyo, mshtakiwa wa 11, Luteni John Chitunguli; mshtakiwa wa 13, Christopher Pastor Ngaiza, wa 15 Luteni Otmar Haule, wa 16 George Banyikwa; mshtakiwa wa 17 Zera na mshtakiwa wa 19 Livinus Maximillian Rugaimukamu walionekana na Anne Kirundu kuwa hawana hatia.

Ilipofika Jumamosi ya Desemba 28, 1985, Jaji Kiongozi Mzavas akawahukumu Watanzania tisa, wakiwamo maofisa wanane wa jeshi na rubani wa ndege za ATC, vifungo vya maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kupanga njama za kuipindua Serikali miaka mitatu iliyokuwa imepita.

Washtakiwa wengine sita, pamoja na Christopher Ngaiza, ambaye alikuwa mshauri wa zamani wa Rais Julius Nyerere, waliachiwa huru.

Wakati akitoa hukumu yake, Jaji Nassor Mnzavas alisema nia ya washtakiwa hao wa njama za uhaini ilikuwa kurekebisha kile walichofikiria kuwa ni hali mbaya ya kiuchumi isiyo na matumaini inayosababishwa na uongozi duni wa Serikali ya Kijamaa, “lakini siwezi kufumbia macho ukweli kwamba ikiwa mapinduzi yangefanyika, watu wengi wangepotea,” alisema Jaji Kiongozi, Nassor Mzavas.

Waliohukumiwa kifungo cha maisha ni Luteni Eugene Maganga, Kapteni Metusela Suleiman Kamando, Kapteni Zacharia Hans Pope na Kapteni Vitalis Gabriel Mapunda.

Wengine ni Kapteni Dietrich Oswald Mbogoro, Luteni Badru Rwechungura Kajaja, Hatibu Gandhi au Hatty McGhee na Kapteni Christopher Kadego.

Kwa jumla washtakiwa 19 waliofikishwa mahakamani kujibu shtaka la uhaini ni Hatty McGhee, Kapteni Christopher Kadego, Luteni Eugene Maganga na Suleiman Kamando, Kapteni Vitalis Mapunda, Kapteni Roderic Roberts, Paschal Chaika, Luteni John Chitunguli, Luteni Mark Mkude, Kapteni Oswald Mbogoro na Kapteni Zacharia Hans Pope.

Wengine ni Luteni Badru Kajaje, Christopher Ngaiza, Luteni Gervas Rweyongeza, Luteni Otmar Haule, George Banyikwa, Zera Banyikwa, Luteni Nimrod Faraji na Livinus Rugaimukamu.

Hata hivyo, baada ya wengine wanne kuachiwa huru Agosti 1985 na kubaki 15, siku ya hukumu wengine waliachiwa huru wakati wenzao wakihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.