Kesi ya wanaodaiwa kuvujisha mitihani kusikilizwa siku nne mfululizo

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga siku nne mfululizo kuanzia April 23 hadi 26, 2024 kusikiliza kesi ya kuvujisha na kusambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Telegram, inayowakabili watu 12 wakiwemo walimu.



Hadija Jumannne, Mwananchi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga siku nne mfululizo kuanzia April 23 hadi 26, 2024 kusikiliza kesi ya kuvujisha na kusambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Telegram, inayowakabili watu 12 wakiwemo walimu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Ajali Milanzi, amepanga tarehe hizo leo Machi 18, 2024 kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Jahnson Ondieka (37), Patrick Chawawa, Theresia Chitanda, Elinami Sarakikya, Joyce Nyanyakila na Gladius Roman.

Wengine ni Dorcas Muro, Alcheraus Malinzi, Lloyd Mpande, Ronald Odogo, Jacob Adagi na Joel Ngome.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kuvujisha mitihani na kutengeneza nyaraka za uongo.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi amedai iliitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji lakini leo ndiyo amepewa jalada la kesi, hivyo akaomba kulipitia kwanza ndipo waendelee na usikilizwaji.

"Mheshimiwa hakimu, jalada la kesi lilikuwa linaendeshwa na wakili mwingine, leo hii ndiyo nimepewa hivyo naomba muda ili niweze kulipitia kabla ya kuendelea na usikilizwaji," ameomba Mbilingi.

Hakimu Milanzi amekubaliana na ombi hilo na kupanga kesi kusikilizwa kwa siku nne mfululizo kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Aprili 23 hadi 26, 2024.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi.

Miongoni mwa mashahidi hao, ni Meneja Uendeshaji Mitihani, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Vonensia Sanga, ambaye alieleza jinsi Serikali ilivyopata hasara ya zaidi ya Sh40 milioni baada ya kuvuja kwa mtihani wa darasa la saba mwaka 2022.

Pia ameeleza jinsi alivyopata taarifa ya kuvuja kwa mtihani na hasara ambayo Serikali imepata kutoka na kitendo alichodai kilifanywa na washtakiwa hao.

Sanga ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, alitoa ushahidi Novemba 16, 2023 mahakamani hapo.

Amedai taarifa ya kuvuja kwa mtihani aliipata kutoka kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji Mitihani Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania, Edger Kasuga.

Alidai Oktoba 13, 2022 saa tatu asubuhi aliitwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa na Edger Kasuga na kutaarifiwa kuwa mtihani ambao ulifanyika Oktoba 5 na 6 ulikuwa umevuja.

Shahidi huyo amedai baada ya kuelezwa hayo, aliagizwa kwenda kwa Mhasibu Mkuu wa baraza hilo kwa ajili ya kupata jumla ya gharama zilizotumika katika maandalizi ya mtihani huo ili zikasaidie kutoa maelezo polisi.

Sanga alidai alifika kwa mhasibu na kutajiwa gharama ya Sh40,460,623 ambazo zinajumuisha gharama za utunzi, uchapaji, ufungaji, usambazaji, usimamizi na usahihishaji.

Alidai alimfikishia Mkurugenzi taarifa ya gharama na baadaye alienda Polisi kutoa maelezo.

Alidai kitendo cha mtihani huo kuvuja, Serikali imepata hasara ya Sh40,460,623 pamoja na baadhi ya wazazi kupata usumbufu kwa vijana wao kurudia mtihani baada ya baraza kufuta matokeo ya vituo 24 vya mitihani.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa Malinzi anadaiwa kati ya Oktoba 2, 2022 na Oktoba 12, 2022 sehemu isiyojulikana akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo za mtihani wa somo la uraia la darasa la saba akijifanya mtihani huo ni halali na umeandaliwa na Necta

Pia, tarehe hiyo na sehemu isiyojulikana Malinzi akiwa na nia ya kudanganya anadaiwa alitengeneza nyaraka za uongo za mtihani wa maarifa ya jamii wa darasa la saba wa mwaka 2022, alionyesha kuwa mtihani huo umeandaliwa na Necta.

Katika shtaka tatu, Adagi na Ngome wanadaiwa kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba, kinyume cha sheria.