Kibao chamgeukia ‘Hausigeli’ tuhuma za mauaji ya Aneth

Dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya wakati wa uhai wake

Dar es Salaam. Mawakili wa utetezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, Bilionea Erasto Msuya, maarufu Miriam Steven Mrita na mwenzake, wamemsukumia zigo la tuhuma za mauaji mtumishi wa kazi za ndani wa marehemu Aneth Msuya.

Mawakili hao Peter Kibatala, anayemtetea mjane huyo ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Nehemia Nkoko anayemtetea mshtakiwa wa pili, Revocatus Muyella maarufu Ray, jana walimwangushia tuhuma hizo msichana wa kazi, Getruda Mfuru wakati wakiwasilisha hoja za mwisho.

Kwa nyakati tofauti, waliiomba Mahakama ione kwamba kwa mazingira ya kesi hiyo na kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo binti huyo aliyekuwa mtumishi wa ndani wa marehemu Aneth ndiye anayehusika na tuhuma za mauaji ya mwajiri wake.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji, wakidaiwa kumuua Aneth Elisaria Msuya, ambaye alikuwa wifi yake (Miriam).

Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Jana kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya mawakili wa pande zote, kuwasilisha hoja zao za mwisho baada ya usikilizwaji wa ushahidi wa pande zote kufungwa Novemba 10, mwaka huu.

Katika hatua hiyo, kila upande uliwasilisha hoja za kuishawishi Mahakama ikubaliane nao kwa ama kuwaona washtakiwa kuwa wana hatia (upande wa mashtaka) ama hawana hatia (upande wa utetezi).

Novemba 6, baada ya Mahakama kufunga usikilizwaji wa ushahidi wa pande zote iliamuru mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao za mwisho kwa njia ya maandishi ifikapo au kabla ya Novemba 27, mwaka huu na ikapanga kesi hiyo itajwe jana Desemba 4, kwa ajili ya taratibu nyingine.

Hivyo jana ilipoitwa mawakili wa pande zote walitoa muhtasari wa hoja zao walizoziwasilisha kwa njia ya mdomo ili wazee wa Baraza katika kesi hiyo wapate fursa ya kusikia kile walichokiwasilisha mahakamani hapo kwa maandishi kabla ya kutoa maoni yao kama washtakiwa wana hatia au hawana hatia.

Upande wa mashtaka ndio ulikuwa wa kwanza kutoa muhtasari wa hoja zake za maandishi na ulihitimisha kwa kuieleza mahakama kuwa umeweza kutimiza wajibu wake wa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa kwa kiwango kinachotakiwa yaani bila kuacha mashaka.

Hivyo uliieleza mahakama kuwa japo kesi imejengwa katika ushahidi wa kimazingira kwa kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia tukio la mauaji hayo, lakini kupitia mashahidi wake 25 waliowaita pamoja na vielelezo mbalimbali walivyoviwasilisha, umethibitisha kuwa washtakiwa hao ndio waliohusika na mauaji hayo.

Miongoni mwa Mashahidi hao ambao upande wa mashtaka uliegemea ni wa shahidi wake wa 25 ambaye ni msichana wa kazi za ndani wa marehemu Aneth ambaye aliyeibeba kesi hiyo.

Walieleza namna alivyosimulia kuwa alikutana na washtakiwa hao mara tatu kwa siku tofauti huko Kigamboni Kibada na kwamba, walimtishia na kumtaka siku hiyo ya tukio asiwepo nyumbani hapo na alipoondoka ndipo baadaye akapata taarifa za mauaji hayo ya mwajiri wake.

Baadhi ya vielelezo ambavyo upande wa mashtaka uliviegemea kuwa kupitia hivyo, wamethibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa ni pamoja na maelezo ya mshtakiwa wa kwanza, Miriam ya onyo (aliyoyaandika Polisi akidaiwa kukubali kosa) na ya ungamo (kukiri kosa mbele ya Mlinzi wa Amani- Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo).

Vingine ni ripoti ya uchunguzi wa kitabibu wa chanzo cha kifo (postmortem report) na ripoti ya uchunguzi wa vinasaba waliyodai kuwa unamuunganisha mshtakiwa wa pili.

Hata hivyo mawakili hao wa utetezi kwa upande wao walichambua kwa ufupi udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka na kuhitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria yaani bila kuacha mashaka yoyote.

Katika uchambuzi wake Wakili Kibatala aliieleza mahakama kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umeacha mashaka makubwa na maswali mengi kuliko majibu huku akibainisha kuwa kuna mashaka na maswali 33 ambayo yanahitaji majibu.

Pamoja na mambo mengine wakili Kibatala alidai kuwa katika kesi za mauaji nia ovu ni kigezo muhimu sana katika kuthibitisha mashtaka na akaeleza kuwa ingawa upande wa mashtaka wakidai kuwa mjane huyo wa Bilionea Msuya alitenda kosa hilo kwa kuwa alikuwa na mgogoro wa mali na marehemu Aneth lakini wameshindwa kuthibitisha mgogoro huo.

"Hakuna hata ndugu mmoja aliyekuja kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na mgogoro wa aina yoyote ile na mshtakiwa wa kwanza. Shahidi wa 22 David Mhanaya (mpelelezi mkuu wa kesi hiyo) hata kesi za mirathi alikuwa hazijui,” alidai.

Aliikumbusha Mahakama kuwa shahidi wa tatu wa utetezi, Kelvin Erasto Msuya aliieleza mahakama alivyosimamia mirathi mpaka ikapangwa na aliwasilisha mahakamani hapo mwenendo wa mahakama katika kesi hizo za mirathi.

Pia alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza alijitetea vizuri akaeleza alivyoishi na marehemu vizuri mpaka sehemu ya mirathi akamgawia pamoja na dada wa marehemu Bilionea Msuya wengine licha ya kutokuwa wanufaika.

Wakili Kibatala alidai shahidi wa 25 (msichana wa kazi) ndiye mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akaondoka na kutokomea kusikojulikana kwa miezi miwili na kwamba, mashahidi kadhaa wa Polisi walikiri kutompata katika simu zake lakini yeye alisema alikuwa anapatikana.

"Binti aliondoka bila kuaga na wao wanaendelea na shughuli zao nyingine tu bila kuchukua hatua thabiti za kumpata huyu shahidi wa 25, haiingii akilini kwa akili ya kawaida tu mtu amekufa kifo kisicho cha kawaida,” alidai Kibatala na kuongeza:

"Sasa jumlisha swali hilo na miezi miwili yote hiyo. Shahidi wa 25 anasema alikuwa anapatikana, lakini muda wote mashahidi wanasema walimtafuta bila mafanikio, nini kimejificha hapo?"

Pia wakili Kibatala alidai mashahidi wawili wa upande wa mashtaka ambao ni maofisa wa polisi walipingana na waliwasilisha vielelezo viwili vinavyopingana kuhusu kukamatwa na kuhojiwa kwa binti huyo wa kazi.

Alibainisha kuwa shahidi mmoja anadai kuwa binti huyo alikamatwa na kuhojiwa kama mtuhumiwa lakini shahidi mwingine anadai kuwa binti huyo hakuwahi kukamatwa na kuhojiwa.

"Sasa vielelezo vyote vinatoka katika Jeshi la Polisi vinapingana nini kimejificha hapa Mheshimiwa Jaji na waungwana wazee wa baraza? --Kwa nini Jeshi moja liwe na vielelezo 2 vinavyopingana?", alihoji na kusisitiza:

"Pia kuna mashaka ambayo lazima yajibiwe kwamba inawezekanaje huyu binti miezi miwili hajakamatwa na baadaye anafuatwa kirahisi tu kama shahidi. Bila kuwakosea upande wa mashtaka kesi hii imeletwa bila kujipanga."

Kwa upande wake wakili Nkoko alidai kuwa hati ya mashtaka ina kasoro kwani inapingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani akibainisha kuwa tarehe, muda na eneo lililotokea tukio vinatofautiana baina ya hati ya mashtaka na ushahidi uliowasilishwa. Pia alibainisha kuwa hata majina ya mshtakiwa wa pili ni tofauti na majina yake halisi na kwamba alishayakana tangu wakati wa usikilizwaji wa awali lakini upande wa mashtaka haukuchukua hatua kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka kwa mujibu wa sheria.

Huku akirejea uamuzi wa Mahakama katika kesi mbalimbali alidai kuwa katika mazingira hayo mahakama inapaswa kuifuta hati hiyo na kuwaachia huru washtakiwa.

"Katika kesi za ushahidi wa mazingira mtu wa kwanza kuhisiwa kuwa muuaji ni yule wa mwisho kuonekana na marehemu na kwa ushahidi huu, wa mwisho ni PW25 (shahidi wa 25 upande wa mashtaka yaani housegirl)", alidai Wakili Nkoko na kusisitiza:

"Hivyo mahakama hii ione kuwa mshtakiwa wa pili hakuhusika na mauaji ya Aneth Elisaria Msuya kwa kukodishwa na Miriam Steven Mrita (mshtakiwa wa pili) na hiyo inakwenda pia kwa mshtakiwa wa pili."

Alihitimisha kwa kusema; 'Hivyo kwa hayo tuliyoyawasilisha kwa mdomo na hoja zetu za maandishi tunaomba mahakama hii iitupilie mbali hati ya mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa."

Jaji Kakolaki baada ya kupokea hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Desemba 11, mwaka huu kwa ajili ya majumuisho ambapo atasoma muhtasari wa ushahidi wa pande zote kisha atatoa nafasi kwa wazee wa baraza kutoa maoni yao kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la, kisha atapanga tarehe ya hukumu.