Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibonde alikwenda kumzika Ruge, hakurudi

Dar es Salaam. Sauti ya makeke kwenye kipindi cha Jahazi, sauti ya uchambuzi wa soka katika televisheni ya Supersport na sauti iliyoongoza mazishi ya Ruge Mutahaba imezima. Ndiyo, haitasikika tena.

Sauti imezima si katika redio ya Clouds FM ya Dar es Salaam, ambako Ephraim Kibonde alikuwa akifanya kazi, haitasikika akiwa hai nchini na hata Afrika Kusini alikokuwa akienda mara kwa mara kuchambua soka.

Kitakwenda vipi kipindi cha Jahazi bila Kibonde? Maisha yanaweza kuendelea namna gani bila sauti yake katika matangazo mbalimbali ya redio hiyo?

Itakuwaje kwa wafanyakazi wa Hoteli ya Oakland Inn ya Afrika Kusini waliozoea kumuona mara kwa mara mwishoni mwa wiki, alipokuwa anakwenda kuchambua mechi za Ligi Kuu England kwa Kiswahili katika studio za televisheni ya Supersport ya Afrika Kusini?

Wafuatiliaji wa mechi za Ligi Kuu England katika chaneli za Supersport, wafanyakazi wa Clouds Media, waliohudhuria msiba wa Ruge Bukoba na Dar, wasikilizaji wake, familia, ndugu na marafiki wote wanalia.

Wanalia kwa sababu hawataisikia sauti ya nyota huyo ambayo ilisikika mara ya mwisho hadharani Jumatatu jioni katika mazishi ya aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba ambaye alifariki dunia nchini Afrika Kusini, Februari 26.

Amemuenzi Ruge? Inaweza kuwa na tafsiri tofauti, lakini siku nne zilizopita Kibonde aliahidi kuwa atamuenzi Ruge Mutahaba kwa kufanya aliyoyahimiza.

“Sisi ambao tumebaki tuendelee kuyafanya yale ambayo alipenda tufanye. Huwezi jua muda gani utafika nawe utaondoka.” Hii ilikuwa kauli ya Kibonde kwa waandishi wa habari siku moja baada ya kifo cha Ruge.

Hajatimiza ahadi hiyo kwani jana asubuhi ilikuwa mwisho wa safari yake ya miaka 47 ya hapa duniani. Kibonde amefariki dunia ikiwa ni siku ambayo wafanyakazi wa Clouds Media ndio walianza kurejea kazini.

Wafanyakazi wengi wa Clouds Media Group ni pigo mara mbili kwani jana ilikuwa siku ya kwanza kazini baada ya kukamilisha mazishi ya Ruge. Ilitarajiwa ingekuwa siku ngumu kazini katika maisha mapya bila kiongozi wao waliyemtegemea na kumwamini katika kila kitu.

Ugumu uliotarajiwa, uliongezwa na machungu mengine baada ya wafanyakazi hao kupokea habari nyingine za kusikitisha za kifo cha Kibonde aliyewaongoza kama ‘MC’ katika shughuli nzima ya mazishi, kuanzia nyumbani Mikocheni, Karimjee na Bukoba.

Katika ofisi za Clouds zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam hali haikuwa ya kawaida, utaratibu ulivurugika na wafanyakazi wengi walikuwa wamekaa katika makundi sehemu ya kuegeshea magari, kila mmoja akiwa na simanzi na wengine wakilia.

Mbali na wafanyakazi, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe naye alifika katika ofisi hizo kujumuika nao ili kujua taratibu zinazofuata.

Kuugua kwa Kibonde

Meneja ubunifu wa Clouds Media, Caesar Redemptus akisimulia kuhusu msiba huo alisema kuwa Kibonde alianza kuumwa ghafla wakati akikaribia kumaliza shughuli ya mazishi ya Ruge katika Kijiji cha Kiziru, Bukoba, Jumatatu iliyopita.

Alisimulia kuwa Kibonde alianza kujisikia vibaya akiwa eneo hilo la msiba na kusaidiwa na watu wa Msalaba Mwekundu waliosaidiana na Dk Isaac Maro, ambaye huendesha kipindi cha Njiapanda cha Redio Clouds kila Jumapili.

Caesar alisema Kibonde aliingizwa ndani ya nyumba ya kina Ruge na kuvuliwa viatu, akalegezwa mkanda kwa kuwa ilionekana kama amepatwa na presha hivyo akapewa huduma ya kwanza akiwa hapohapo nyumbani.

“Baada ya huduma ya kwanza tulimpeleka katika hospitali ya Bukoba kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri hivyo akatibiwa pale na kupata chakula, akarudi katika hali nzuri kidogo,” alisema Caesar ambaye pia ni mtangazaji wa kipindi cha Power Breakfast.

Baada ya Kibonde kupata nafuu, Dk Isaac na wenzake walijadiliana na madaktari wa hospitali ya Bukoba kujua kama Kibonde anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa matibabu zaidi.

“Baada ya majadiliano tulimuuliza Kibonde kama anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa kuwa ndege yetu ilikuwa inaondoka asubuhi ya siku inayofuata. Alituambia anaweza kusafiri na tukakubaliana tukampeleka uwanja wa ndege kwa safari.”

Caesar alisema siku iliyofuata walifika Mwanza kwa ndege na kumweka Kibonde kwenye kiti cha magurudumu (wheel chair) akisaidiwa na Dk Isaac aliyekutana na rafiki yake ambaye ana hospitali Mwanza.

“Baada ya kufika pale tulimwacha Kibonde na Dk Isaac na huyo daktari mwingine ambaye ni rafiki yake, sisi tukaendelea na safari kuelekea Dar es Salaam hadi leo asubuhi (jana) tunapata taarifa kuwa amefariki dunia hivyo ndivyo ilivyokuwa,” alisema Caesar.

Uvimbe tumboni

Samson Kibonde, ambaye ni baba mzazi wa Ephraim Kibonde alisema alitaarifiwa kuwa mwanaye ana uvimbe tumboni, lakini hakuwa na hali mbaya sana.

“Kibonde alikwenda Bukoba kwa ajili ya mazishi ya mfanyakazi mwenzake Ruge, baada ya shughuli akaanza kuumwa na kupelekwa hospitali ya Bukoba, hali ilipozidi zaidi walimpeleka Mwanza, niliwasaliana naye Jumatatu na Jumanne, mganga wa pale akaniambia anaendelea vizuri, mpaka jana walitarajia kurudi leo (jana) asubuhi aletwe hospitali za Dar es Salaam.” alisema baba huyo.

“Lakini usiku alizidiwa na kuhamishiwa Hospitali ya Bugando, jitihada zilishindikana na mauti kumkuta saa 12.30 asubuhi.”

Kibonde, ambaye amewahi kuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha CTN cha Dar es Salaam atazikwa kesho Jumamosi katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam karibu na alipozikwa mke wake mwaka jana. Kibonde ameacha watoto watatu.