Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kifo cha Jenerali Moses chakumbusha vita vya Kagera

Muktasari:

  • Jana Jumamosi, Julai 18, 2026, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alitangaza kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe aliyehudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya jeshi na serikalini.



Dar es Salaam. Kifo cha Jenerali mstaafu Moses Ali (87) kinaacha historia kubwa katika siasa na Jeshi la Uganda na Afrika Mashariki.

Anakumbukwa kama mmoja wa washirika wa karibu wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin Dada, na kamanda mwandamizi wa jeshi ambaye, muda mfupi kabla ya kuzuka kwa Vita vya Kagera mwaka 1978, alitofautiana na Amin, akafukuzwa serikalini na kuvuliwa nyadhifa zake za kijeshi.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametangaza kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alifariki dunia jana Jumamosi, Julai 18, 2026, saa 10 jioni katika Hospitali ya Nakasero, Kampala, alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Alisema taifa limepoteza “ndugu na mtumishi wa muda mrefu” aliyechangia katika kulinda amani, kujenga maridhiano na kuimarisha utawala wa Uganda kwa miongo kadhaa.

Kifo chake kinahitimisha safari ya zaidi ya miongo sita ya utumishi katika jeshi, siasa na uongozi wa umma, na alihudumu chini ya tawala tofauti na kuwa mmoja wa viongozi waliodumu kwa muda mrefu zaidi nchini Uganda.


Alivyotamba kwenye mitandao

Jenerali Moses Ali alikuwa akivutia mijadala mitandaoni katika siku za hivi karibuni kutokana na umri wake mkubwa, huku wasaidizi wake wakionekana mara nyingi wakimsaidia na kuwa karibu naye wakati wa kutekeleza shughuli zake za kikazi na za umma.

Miezi kadhaa kabla ya kuondolewa katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu wa Pili wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Jenerali Moses alikuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kutokana na hali yake ya uzee iliyokuwa ikionekana wazi katika shughuli za umma.

Video na picha zilizosambaa kwa kasi zilimuonesha akiwa akitembea kwa mwendo wa taratibu na, katika baadhi ya matukio ya hadhara, akisindikizwa kwa karibu sana na wasaidizi wake.

Wasaidizi hao walionekana wakibaki pembeni yake ili kumsaidia wakati wa kutembea, kupanda na kushuka ngazi au kuelekea katika maeneo ya mikutano rasmi.

Taswira hizo zilisambazwa kwa wingi kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mpana kuhusu umri wa viongozi wanaoendelea kushika nyadhifa za juu serikalini.

Baadhi ya wachangiaji walieleza wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kuendelea kutekeleza majukumu mazito ya Serikali, huku wengine wakisisitiza kuwa alistahili heshima kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa na kwamba changamoto za uzee hazikupaswa kufuta historia yake ya utumishi.

Muda mfupi baadaye, Rais Museveni alimwondoa Jenerali mstaafu Moses katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu wa Pili na Naibu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyolenga kuimarisha utendaji wa Serikali.

Nafasi yake ilichukuliwa na Dk Crispus Walter Kiyonga, mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Waziri wa Ulinzi.

Kuondolewa kwa Jenerali Moses kulikuwa sehemu ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Rais Museveni, ambapo mawaziri wengine 28 pia waliondolewa katika awamu hiyo.


Hakushiriki vita vya Kagera

Licha ya kuwa mmoja wa makamanda waandamizi na washirika wa karibu wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin Dada, Jenerali mstaafu Moses Ali hakushiriki Vita vya Kagera vya mwaka 1978–1979 kati ya Uganda na Tanzania, baada ya kufukuzwa serikalini miezi kadhaa kabla ya vita hivyo kuanza.

Moses Ali alikuwa miongoni mwa wanajeshi waliomuunga mkono Idi Amin wakati wa mapinduzi ya mwaka 1971 yaliyomwondoa madarakani Milton Obote.

Baada ya mapinduzi hayo, alipanda vyeo kwa haraka katika Jeshi la Uganda na kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ikiwemo Waziri wa Tawala za Mikoa na baadaye Waziri wa Fedha.

Hata hivyo, mwaka 1978 uhusiano wake na Idi Amin ulivunjika baada ya kutofautiana kuhusu uendeshaji wa Serikali na masuala ya kifedha.

Kutokana na mgogoro huo, Amin alimfukuza kazi, akamvua vyeo na heshima zake za kijeshi, hatua iliyomlazimu Moses Ali kukimbilia eneo la West Nile kujinusuru baada ya kuripotiwa kuwepo kwa vitisho dhidi ya maisha yake.

Kutokana na kuondolewa kwake serikalini kabla ya kuzuka kwa Vita vya Kagera mwezi Oktoba 1978, Moses Ali hakuwa sehemu ya vikosi vya Uganda vilivyopambana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wapiganaji wa Uganda walioungana kupambana na utawala wa Idi Amin.


Mtu wa maridhiano

Mwaka 1988, Jenerali Moses Ali aliweka historia kwa kusaini makubaliano ya amani na Serikali ya Rais Museveni.

Hatua hiyo inatajwa kuwa haikuwa tu njia ya yeye kurejea serikalini, bali ilikuwa msingi mkuu uliochangia kurejesha utulivu, usalama na imani ya wananchi katika eneo lote la West Nile lililokuwa limekumbwa na machafuko kwa muda mrefu.

Kupitia ushawishi wake, alifanikiwa kuwashawishi wapiganaji wengi wa zamani kuweka silaha chini na kujumuika katika ujenzi wa taifa, na hivyo kujenga taswira yake kama nembo ya ustahimilivu na maelewano ya kitaifa.

Baadaye, mwaka 1986, Moses Ali alifikia makubaliano ya amani na Serikali ya Rais Yoweri Museveni.

Chini ya makubaliano hayo, yeye pamoja na wapiganaji wake waliunganishwa katika mfumo wa Serikali na vikosi vya usalama, hatua iliyomwezesha kurejea katika maisha ya kisiasa na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ikiwemo nafasi ya Naibu Waziri Mkuu wa Pili.

Mbali na siasa na jeshi, Moses Ali alijulikana kama mtetezi wa maendeleo katika eneo la Adjumani na West Nile.

Alisimamia miradi ya maendeleo katika elimu, afya, miundombinu na huduma za kijamii, huku akisisitiza umoja wa kitaifa na maridhiano kati ya jamii zilizowahi kuathiriwa na migogoro.

Kwa zaidi ya miaka 30 akiwa mbunge, aliendelea kuwa sauti ya wananchi wa Adjumani West na mmoja wa wanasiasa waliodumu kwa muda mrefu zaidi nchini Uganda.

Kifo cha Jenerali Moses Ali kinafunga ukurasa muhimu wa historia ya Uganda.

Alikuwa mmoja wa viongozi wachache waliohudumu katika vipindi tofauti vya kisiasa vya nchi hiyo, kuanzia enzi za Idi Amin, kipindi cha mapambano ya waasi hadi Serikali ya Rais Yoweri Museveni.