Prime
Kifo cha mfungwa kilivyomsotesha gerezani mkuu wa gereza, wasaidizi wake kwa siku 1,110

Mtwara. Mahakama ya Rufani nchini, imewaachia huru mkuu wa Gereza la Kipule Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Mrakibu wa Magereza (SP), Girbet Sindani na maofisa wake wawili, waliokuwa wakitumikia kifungo cha miaka 17 gerezani.
Kwa mahesabu, tangu SP Sindani na Sajini Yusuph Selemani mwenye namba B.4048 na Koplo Fadhil Mafowadi mwenye namba B.74114 wakamatwe Juni 2022 hadi kuachiwa huru jana Juni 30,2025, walishakaa mahabusu gerezani kwa siku 1,110.
Lakini tangu wahukumiwe kifungo hicho Desemba 19, 2024 hadi wanaachiwa huru, vigogo hao wa zamani wa magereza wametumikia kifungo kwa siku 193 na kwa hukumu hiyo wana haki ya kurejeshwa kazini na kulipwa stahiki zao zote.
Awali vigogo hao walikuwa wameshtakiwa kwa makosa mawili likiwamo la mauaji ya kukusudia ya mfungwa na kosa la pili lilikuwa ni kujaribu kumuua mfungwa mwingine, ambaye waliteswa pamoja na marehemu ndani ya gereza.
Hata hivyo, Desemba 19, 2024 Mahakama Kuu kanda ya Mtwara iliyosikiliza shauri hilo chini ya Jaji Rose Ebrahim ilifikia hitimisho kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa umeshindwa kuthibitishwa mashitaka hayo kwa viwango vinavyokubalika.
Badala yake, ikawatia hatiani kwa kuua bila kukusudia na kuwahukumu kifungo cha miaka 17 na miezi sita jela na kifungo cha miaka minne na miezi sita jela kwa kosa la kusababisha madhara makubwa ya kimwili kwa mfungwa mwingine badala ya kosa la kujaribu kuua.
Hawakuridhishwa na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani ambapo jopo la majaji watatu, Ignas Kitusi, Abraham Mwampashi na Paul Ngwembe, limebatilisha hukumu ya awali na kufuta adhabu na kuwaachia huru.
Katika hukumu yao, majaji hao wamesema upande wa mashitaka haukuthibitisha mashitaka ambayo Mahakama Kuu iliwatia nayo hatiani, na kulikuwa na mkanganyiko wa ushahidi ambao haukutatuliwa na mashahidi.
Tukio la mauaji lilivyokuwa
Kulingana na mwenendo wa shauri hilo, Juni 2022 wafungwa katika Gereza la Kipule walikuwa katika shughuli mbalimbali ikiwamo kuvuna mahindi ambapo katika kazi hiyo kulijitokeza wizi wa mahindi yaliyokuwa yamevunwa.
Baadhi ya wafungwa walishukiwa kuhusika na wizi huo na uongozi wa gereza ulifanya uchunguzi ambapo walioshukiwa waliitwa na kuhojiwa na maofisa magereza na miongoni mwao ni Abdalah Ngatumbala na Sihaba Mswaki.
Katika mahojiano hayo, wafungwa hao wawili waliteswa ili wataje mahali yalipo mahindi yaliyoibwa na wahusika ni akina nani ambapo waliumizwa vibaya mwili kutokana na mateso hayo na kupelekwa hospitali.
Hata hivyo, Abdalah Ngatumbala alifariki dunia wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake, kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata, lakini mwenzake, Sihaba Mswaki alipona baada ya kulazwa na kupatiwa matibabu.
Uchunguzi ulianzishwa ambapo maofisa hao watatu wa magereza walishukiwa kutenda ukatili huo na kukamatwa na kufunguliwa kesi mwaka 2022 wakituhumiwa kwa mauaji ya kukusudia na kosa la kujaribu kuua mfungwa.
Ushahidi ulivyokuwa
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi saba ambapo shahidi wa kwanza na wa nne ndio walioshuhudia tukio hilo ambapo shahidi wa kwanza alisema yeye alishuhudia mchakato wote wa mahojiano na mateso kwa wafungwa hao.
Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa maofisa hao ndio waliohusika na shughuli nzima ya kuwahoji na kuwatesa wafungwa hao, lakini shahidi wa nne ambaye ni mfungwa anayedaiwa kuteswa pamoja na Abdalah, alikuwa na hadithi tofauti.
Yeye aliiambia mahakama kuwa maofisa hao sio ambao waliwatesa bali ni maofisa wengine kabisa ambao hawajashtakiwa, na bahati mbaya upande wa Jamhuri haukumdodosa wala kutamka kama shahidi aliyeigeuka Jamhuri.
Namna walivyojitetea
Katika utetezi wake, SP Sindani kama alivyokuwa, alikanusha mashitaka dhidi yake na kueleza kuwa amebambikiwa makosa hayo kwa vile hakuwa na mahusiano mazuri na shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye hata hivyo hakutajwa kwa jina.
Mkuu huyo wa zamani wa Gereza la Kipule alieleza mahakama kuwa siku ya tukio, alipokea taarifa kutoka kwa maofisa walio chini yake, wakimjulisha juu ya wizi wa mahindi uliotokea na tayari wafungwa wawili wameshahojiwa.
Alisema baada ya kupewa taarifa hiyo, aliwaagiza maofisa hao kufanya uchunguzi wa kina wa suala hilo na kuwafungulia mashitaka wafungwa kwa kosa la wizi.
Baada ya hapo aliondoka ofisini kuelekea Lindi lakini akiwa katika mji wa Liwale akienda Lindi, alijulishwa na maofisa wake kuwa mmoja wa wafungwa alikuwa na hali mbaya na kuagiza apelekwe hospitali ambapo naye alikwenda kukutana nao.
Anaeleza kuwa maofisa wake walitafuta fomu ya polisi namba tatu (PF3) ambapo wafungwa wote walipelekwa hospitali lakini baadaye alipokea taarifa kuwa mfungwa mmoja, Abdalaha Ally Ngatumbala alifariki dunia hospitalini hapo.
Sajini Selemani kwa upande wake, alikanusha mashitaka yaliyokuwa yakimkabili na kueleza kuwa Juni 7, 2022 alikuwa akijihusisha na kuchanja chanjo ng’ombe kazi ambayo alikuwa akiifanya kwa kushirikiana na wafungwa watatu.
Alimaliza kazi hiyo ya chanjo saa 4:00 asubuhi na ng’ombe wakapelekwa malishoni na alipokuwa anarudi kwenye saa 7:00 mchana alipita katika shamba lililokuwa linavunwa mahindi na kukuta mifuko 60 ya mahindi yakiwa tayari yamevunwa.
Ilipofika saa 10:00 alasiri wakati anarudi alikuta mifuko minane au tisa na mingine iliyokuwa na mahindi ilikuwa imeibwa ambapo alimjulisha bosi wake, aitwaye Japhet ambaye alikuwa na cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, ASP Japhet alimwambia kuwa alikuwa na taarifa juu ya wizi huo na tayari washukiwa wawili wameshabainika hivyo akaendelea na shughuli zake Juni 8, 2022 aliendelea na shughuli za ng’ombe.
Ilipofika saa 2:00 asubuhi, alipokea simu kutoka kwa Japhet akimtaka aripoti kwake, ambapo aliwarudisha wafungwa aliokuwa akishirikiana nao na kwenda jengo la utawala.
Alipofika hapo aliwakuta wafungwa wanne, wawili wakiwa wamesimama na wawili wakiwa wamekaa sakafuni ambao ni Abdalah na Mswaki, ambapo afande Japhet alimwamuru asafiri na mkuu wa gereza kwenda Lindi alipokuwa na kikao Juni 9.
Alijiandaa kwa safari hiyo na kuungana na mkuu wa gereza lakini walipokuwa eneo la gereji, bosi wake alipokea taarifa juu ya wafungwa wale wawili.
Mshtakiwa wa tatu, Koplo Fadhili Mafowadi, yeye alieleza kuwa siku ya tukio alipangiwa kuwa na wafungwa 21 kwa ajili ya kujenga baadhi ya majengo.
Ilipofika saa 1:30 alipokea maagizo kutoka kwa Sajenti Abdalah kwamba akamchukue mfungwa aitwaye Sihaba Mswaki ampelekea gerezani lakini wakati anampeleka mfungwa huyo, alishangaa kumuona anachechemea.
Alimsindikiza mfungwa huyo hadi kwa ASP Sabasaba Mselem ambapo alimuona pia ASP Mwaijande akiwa na wafungwa wengine watatu, wawili wakiwa wamesimama lakini Abdalah Ngatumbala (marehemu) akiwa amekaa sakafuni.
Baadaye alirudi kwa mkuu wake wa kazi na kuendelea na majukumu yake.
Pamoja na utetezi wao huo, Mahakama Kuu iliwatia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia na kosa la kusababisha madhara mabaya mwilini ambapo kwa kosa la kuua walihukumiwa miaka 17 na miezi sita na la majeraha miaka minne na miezi sita.
Rufaa yao ilivyokuwa
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa yao, maofisa hao waliwakilishwa na wakili Rainery Songea wakati Jamhuri ikiwakilishwa na wakili wa Serikali mkuu, Wilbard Ndunguru ambaye alisaidiana na Godfrey Mramba kuitetea Jamhuri.
Akijenga hoja za rufaa hiyo na kwa nini wateja wake waachiwe, wakili Songea alisema shahidi wa kwanza na wa nne wa Jamhuri ndio walishuhudia tukio hilo, lakini walijikanganya kana kwamba hawakuwa pamoja katika eneo la tukio.
Shahdi wa kwanza alieleza kuwa ni warufani ndio waliofanya tukio hilo lakini shahidi wa nne akiwa chini ya kiapo alisema maofisa hao waliopo kizimbani hawakuhusika na tukio hilo na kumtaja Mselem kuwa ndio muhusika.
Wakili huyo akasema pamoja na Mselem kutajwa, hakuitwa kutoa ushahidi wala mpelelezi wa kesi hiyo naye hakuitwa kutoa ushahidi wake ili angalau kuisaidia Jamhuri kurekebisha au kuweka sawa kuhusu mkanganyiko uliojitokeza.
Kutoitwa kwa Mselem kuliibua mashaka juu ya ushahidi wa Jamhuri kuhusu nani hasa alimuua Abdalah Ngatumbala na nani aliyemsababishia majeraha Mswaki.
Wakili huyo alisema wala mahakama haikumtamka shahidi wa nne kama shahidi aliyegeuka (hostile witness) hivyo mahakama haikustahili kutouzingatia ushahidi wake huo, wakati inatoa hukumu na kuwatia hatiani warufani.
Mkanganyiko ulioletwa na shahidi wa nne dhidi ya ushahidi wa shahidi wa kwanza, wote wakiwa ni mashahidi wa Jamhuri ni mkubwa na mahakama ilipaswa kuwapa faida washitakiwa na kuwaona hawana hatia na kuwaachia huru.
Wakili Ndunguru kwa upande wake, alipinga vikali rufaa hiyo akisisitiza upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka hayo pasipokuacha mashaka, na hivyo kutiwa kwao hatiani na kuhukumiwa vifungo walivyopewa ilikuwa ni sahihi.
Kuhusu mkanganyiko wa shahidi wa kwanza na wa nne, wakili huyo alisema haikugusa mzizi wa shauri hilo la mauaji huku akisema hakukuwa na haja ya kuita mashahidi zaidi kwani ushahidi wa shahidi wa kwanza uliziba mashimo yote.
Wakili huyo alisema ushahidi wa shahidi wa nne unaweza kuwa ulishawishiwa na mambo mbalimbali lakini mashahidi wengine wote walikuwa imara, na Mselem aliyetajwa hakuitwa kutoa ushahidi kwa kuwa hakupatikana.
Hukumu ya jopo la majaji
Katika hukumu yao waliyoitoa jana Juni 30,2025 walisema hakuna ubishi kuwa ushahidi wa shahidi wa nne wa Jamhuri ambaye ni mwathirika wa mateso yaliyosababisha kifo cha Abdalah ulikuwa tofauti na shahidi wa kwanza.
Majaji hao walirejea ushahidi huo na kueleza kuwa shahidi wa kwanza alisema Juni 8,2022 alishuhudia maofisa hao wakiwapiga wafungwa hao wawili, Abdalah Ngatumbala (marehemu) na Sihaba Mswaki kwa kutumia fimbo.
Kulingana na shahidi huyo, SP Sindani ndiye alikuwa akiwapiga kwa fimbo na baadaye alitoa amri kwa Sajini Selemani na Koplo Mafowadi kuendelea kuwapiga wafungwa hao na walitii amri hiyo na kuendelea kuwapiga mbele ya SP Sindani.
Kwamba wakati yote hayo yanatokea, sajini Sababa na ASP Nicholaus Mselem walikuwepo, lakini shahidi wa nne alikuwa miongoni mwa wafungwa waliopigwa, lakini yeye anasema walipigwa Juni 7 na sio Juni 8 na warufani sio waliowapiga.
Majaji hao walisema Mahakama Kuu katika kupima ushahidi wa mashahidi, waliona ushahidi wa shahidi huyo wa nne unatofautiana na mashahidi wengine, hivyo Jaji alihitimisha kwa kusema kuwa shahidi huyo alikuwa hasemi ukweli.
Walisema kitendo cha Jamhuri kushindwa kutumia haki yake kwa shahidi huyo wa nne kwa kuomba kibali cha mahakama kumdodosa (cross examine) shahidi huyo au kumtamka kama “hostile witness” kulifanya ushahidi wake ubakie jaladani.
Kulingana na majaji hao, kubakia kwa ushahidi huo kulifanya uwe sehemu ya ushahidi wa Jamhuri ambao kwa hitimisho ilikuwa na mkanganyiko mkubwa na haukupaswa kutozingatiwa tu, bali ulitakiwa upatiwe ufumbuzi kisheria.
“Pale mkanganyiko usipopatiwa ufumbuzi unakuwa ni faida ya mshitakiwa”, walisema majaji hao lakini katika kesi iliyopo mbele yao, Jaji alitumia kanuni ya kumuamini shahidi mmoja na kutomwamini mwingine kufikia hitimisho.
“Katika kesi hii, Mahakama Kuu ilimuondolea sifa shahidi wa nne badala ya kuchambua ushahidi wake kwa kuegemea jaribio la uaminifu kwa kuuhusianisha na ushahidi wote wa mashitaka kwa ujumla wake,”walisema.
“Hii inatupeleka hoja ya pili. Shahidi muhimu ASP Mselemu hakuitwa kutoa ushahidi. Mashahidi muhimu wa Jamhuri na wale wa utetezi wanamnyooshea kidole na hata shahidi wa nne anakana si washitakiwa waliowatesa bali ni Mselem.”
“Kwa kuuzingatia ushahidi wa kesi hii hususan mashuhuda ambao wamejikanganya wenyewe kuhusu nani hasa waliwatesa, ASP Mselemu alikuwa shahidi muhimu sana wa Jamhuri wa kutegua kitendawili hicho.”
Majaji hao walisema jaribio la Jamhuri kujitetea kuwa ASP Mselem hakuitwa kwa kuwa hakupatikana haina maana yoyote katika hatua ya rufaa kwa kuwa kumbukumbu zinaonyesha hakuwa ameorodheshwa kama shahidi.
Kutokana na uchambuzi wao huo, majaji hao wamesema huwezi kusema hata mashitaka waliyofungwa nayo yalithibitishwa pasipo kuacha mashaka, kwa sababu ilikuwa ni lazima Jamhuri ithibitishe ni nani waliowapiga wafungwa hao.
Ni kutokana na msingi huo, majaji hao wamebatilisha kutiwa kwao hatiani na kufuta adhabu waliyopewa na kuamuru waachiliwe huru mara moja.