Kigwangala awapa siku 40 wanakijiji kuondoka ndani ya pori la Akiba Kijereshi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala

Muktasari:

Alikuwa katika ziara ya kutembelea hifadhi hiyo

Busega.Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala, amewataka wananchi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Pori la Akiba la Kijereshi (Busega Mkoani Simiyu) kuondoka ndani ya siku 40 kuanzia leo.

Wananchi hao ni wale walioweka makazi na kufanya shughuli za kijamii kwenye eneo la mitaa 500 za pori hilo.

Akizungumza leo Julai 19, Dk Kigwangala alimwagiza Meneja wa Hifadhi hiyo Diana Chambi kuhakikisha kabla ya siku hizo 40 kwisha, awaandikie barua za kutoka kwenye eneo hilo wote waliovamia hifadhi hiyo.

Alimtaka kuanza kuweka alama za kutambua mwisho wa hifadhi.

Dk kigwangala alitoa agizo hilo jana Julai 18, wakati wa ziara yake  ya kutembelea hifadhi hiyo, ambapo alishangaa kuona idadi kubwa ya wananchi wakiwa wamejenga  nyumba za kudumu ndani ya pori hilo, ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

Akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo, wakiwamo watumishi wa halmashauri hiyo, Waziri huyo alisema kuwa ikiwa wananchi hao watashindwa kuondoka wenyewe ifikapo Agosti 31, mwaka huu, nguvu itatumika kuwaondoa kwa lazima.

" Muda huo ukiisha kazi inaanza mara moja, hapa hakuna utani, hii ni hifadhi tayari kwa hiyo lazima itunzwe na kulindwa, tukiwaacha hawa wataendelea na ujangili pamoja na kuchungia mifugo, tarehe 1, Septemba operesheni inaanza kwa mtu atakayegoma kuondoka," amesema Kigwangala.

Katika hatua nyingine Waziri Kigwangala ameitaka kampuni ya Kijereshi Tented Camp iliyowekeza kwenye pori hilo ndani ya muda wa miezi mitatu, kurejesha mara moja kwa msajili wa ardhi hati ya eneo lenye ekari 1160 lililoko ndani ya hifadhi pori hilo kutokana na kupewa kimakosa.

Amesema kuwa Mwekezaji huyo alipewa hati ya kumiliki eneo hilo ndani ya hifadhi ya serikali, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria, na kumtaka arejeshe ili aanze kuomba upya kwa kufuata taratibu zilizowekwa na serikali.

" Hifadhi hii imeanza rasmi mwaka 1994, lakini huyu mwekezaji hii hati aliipata mwaka 1995 wakati tayari hifadhi tumeishapa hati tayari, sasa hakuna sharia ambayo inasema kupata hati juu ya hati, hiyo lazima urejeshe hiyo hati Mara moja ndani ya miezi mitatu, kisha aanze kuomba upya kwa kufuata taratibu," Alisema Kigwangala.

Awali  Meneja wa Pori hilo Diana Chambi alisema kuwa wananchi waliovamia hifadhi ya pori hilo ni kutoka kwenye vijiji vya Lukungu, Mwabayanda, mwakiloba, kijirishi pamoja na Igwata, ambao alieleza waliomba kupewa muda mpaka mwezi Agosti mwaka huu wavune mazao waliyolima ili waondoke kwa hiari kwenye eneo la hifadhi hiyo.