Prime
Kikongwe wa miaka 115 ajiandalia mazishi

Patrick Kimaro maarufu Sabasita, alijichimbia kaburi ikiwa ni sehemu ya kujiandalia maisha yake ya baadaye baada ya kuondoka duniani, sasa yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha jeneza lake na wosia.
Mwingine ni mkazi wa Arusha, Ndelekwa Ayo (103) ambaye amejiandalia kaburi nyumbani kwake na ameelekeza azikwe katika eneo hilo ambalo amekuwa akiishi kwa muda mrefu.
Pia mwaka 2020, mkazi mmoja wa kijiji cha Wangama mkoani Njombe, Anthony
Mwandulami alijiandalia kaburi lake pamoja na wake zake saba, hali iliyoelezwa si utamaduni wa wakazi wa mkoa huo.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni kwenye mahojiano maalumu, Chipita alisema amejiandalia vifaa vya kumzikia siku ya kifo chake kwa kuhifadhi vifaa vyote vitakavyotumika na shughuli nzima ya kumsindikiza kwenye nyumba yake ya milele.
Chipita amejiandalia vifaa kama vile sanda, kitanda, taa, sabuni pamba na vifaa vya kuchimbia kaburi ambavyo amevitunza ndani kwa miaka mitano sasa, huku kitanda atakachooshewa ndicho anacholalia kwa sasa.
Kikongwe huyo mwenye watoto watano, wajukuu 30 na vitukuu 40, alisema kufa kupo na hawezi kuogopa na anafanya maandalizi hayo kwa kuwa Mungu amemuamuru kufanya hivyo akiamini kila mtu atakufa.
“Wanangu hawana neno, wanajua wamejiandaa hawatakosa kufanya mambo yao, kulala matanga na mengineyo, wafanye tu mengine. Nimewasaidia ili wasipate shida kutafuta pesa za kuninunulia vifaa hivyo.
“Hata kaka yangu mkubwa alijinunulia mwenyewe, akajisomea hitima kisha akaviweka sandukuni akisubiri kufa. Akifa ndiyo atafanyiwa hitima, hata jirani yangu nyumba ya pili ameweka pia, si ajabu,” alisema.
Chipita ambaye anaishi kwa mtoto wake wa mwisho, alijitengenezea “benki ya dharura” kwa kuhifadhi fedha kwenye kopo ndani ya nyumba yake. Alisema benki hiyo haikauki fedha, hata wanae hukopa na kurejesha na fedha hiyo ndiyo itatumika kununua vitu kwenye mazishi yake.
Akizungumzia jambo hilo, Esha Chipita ambaye ni mtoto wa tatu wa mzee huyo, alisema baba yake alikwenda mwenyewe kununua na aliwajulisha kuwa amenunua vifaa kwa ajili ya kumzikia siku akifariki.
“Kiukweli hii mimi naogopa, siwezi kuthubutu, yaani niandae tena nitunze kwenye sanduku ndani kwangu vifaa vingine vya mazishi, siwezi hata kama umri umeenda. Naogopa sana, yaani mzee hapo amejishukuru mjue.
“Mzee kaweza, hata baba mkubwa alikuwa anaweza, mimi siwezi kabisa. Unaweza kununua leo ukashangaa kesho unakufa. Mimi siwezi kufanya hivyo, ikitokea (nimekufa) itokee tu, lakini hatuombei,” alisema Esha.
Naye Aziza Chipita, mtoto wa tano wa mzee huyo ambaye ndiye anamtunza nyumbani kwake, alisema mzee amejiandalia vifaa vyake kutokana na fedha aliyoipata wakati akitengeneza pombe ya kienyeji, baadaye aliacha na fedha aliyopata aliitumia kujinunulia vifaa vyake.
“Mzee amejaaliwa na hatuna kipingamizi juu ya hilo kwa kuwa amefanya uamuzi mwenyewe wala hatukuona kama ni uchuro. Nikiwa na uwezo nitajinunulia na kuvitunza, sioni kama ni tatizo,” alisema.
Kwa upande wake, Ally Amilongo, mkwe wa Chipita alisema; “Nilikuwa naishi mbali na yeye, lakini baadaye nilipata tatizo la macho, kwa sasa sioni. Mke wangu alinichukua na kunileta hapa nyumbani ili kuleta urahisi wa kunihudumia mimi na baba yake (mkwe) ambapo mimi nilikuta amenunua vifaa hivyo.
“Nilikuta ameshaweka vifaa vyake ndani, yaani amenunua hadi shoka la kukatia miti na mbao zake mbili, marashi, pamba, jembe la wima, tezo na kitanda kipya na ana mkeka wake ametunza na amejiandaa hata asipochangiwa anaweza kuondoka.
“Kufarahisha zaidi, ana kibenki chake ambacho ametunza pesa ambayo ni kwa ajili ya kununua vitu vidogo vidogo vitakavyohitajika wakati wa msiba wake. Hicho kibenki huwa tunajikopesha na baadaye tunalipa, hili kwetu ni funzo, sio uchuro, hata mimi nimejifunza kitu,” alisema.
Alisema mzee huyo hakufanya mambo ya ajabu wakati wa ujana wake, ni mtu wa kawaida, hanywi pombe, havuti sigara, anatumia asali ambayo anaiweka kwenye kila chakula anachokula, anatafuna bamia,” alisema.
Jirani yake, Asha Salum alisema jambo hilo kwa miaka ya hivi karibuni ni la ajabu, hata mtu akifanya hivyo anakuwa anaogopeka kwa kuwa sio jambo la kawaida.
“Niliposikia niliogopa nikapata hofu sana, unaanzaje kwenda kuchagua vifaa eti utakavyozikwa navyo siku ukifa, unajua ni jambo gumu? Nimesikia wapo waliochimba mpaka makaburi yao wakisubiri kufa, huo ni uchuro,” alisema Asha