Kikosi Kazi champa hofu Profesa Lipumba

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza wakati wa kuzindua mradi wa kuimarisha ushiriki wa vijana katika michakato ya kisiasa na chaguzi, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Ukimya wa siku 146 bila taarifa za upatikanaji wa ripoti ya maoni ya wadau wa demokrasia nchini, umeibua hofu ya ucheleweshaji unaoweza kuathiri mahitaji ya tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Dar es Salaam. Ukimya wa siku 146 bila taarifa za upatikanaji wa ripoti ya maoni ya wadau wa demokrasia nchini, umeibua hofu ya ucheleweshaji unaoweza kuathiri mahitaji ya tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Hofu hiyo imeelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD), Profesa Ibrahim Lipumba, aliyedai ripoti ya kikosi kazi cha ukusanyaji wa maoni hayo, ndio msingi utakaotoa mwelekeo wa kuanza uandaaji wa tume hiyo.

Msingi wa kauli hiyo aliutoa juzi wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya kuimarisha ushiriki wa vijana katika michakato ya kisiasa na chaguzi nchini chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa vijana katika chaguzi na ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Tangu kuanza kwa kikosi kazi, kuanzia Aprili 27, mwaka huu vyama vya siasa na makundi mengine, walipendekeza kuwapo kwa tume huru kabla ya uchaguzi.

“Tusipokamilisha mapema tutaendaje kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa? tutapata wapi muda wa kushiriki mikutano ya hadhara?,” alisema Lipumba.

Lipumba alitoa kuli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuahidi Serikali itatoa ufafanuzi siku chache zijazo huku akiwataka wadau kusubiri mapendekezo ya kikosi kazi.

Alipongeza juhudi za Rais kurejesha matumaini kupitia kikosi hicho kinachoshughulikia hoja ya mikutano ya hadhara ya kisiasa, uchaguzi, mfumo wa maridhiano, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi, elimu ya uraia rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na Katiba mpya.

Mjumbe wa Kamati Kuu ACT -Wazalendo, Ismail Jussa alishauri mageuzi ya mfumo huo wa uchaguzi kupitia tume za uchaguzi na mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.


Hofu ya vijana

Katika hatua nyingine, baadhi ya vijana waliotoa maoni yao katika jukwaa hilo jana chini ya uwakilishi wa vyama ambavyo ni wanachama wa TCD, walieleza wasiwasi katika uhamasishaji wa vijana kushiriki kwenye chaguzi na nafasi za uongozi kupitia vyama vya upinzani.

Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT- Wazalendo, alisema kwa uzoefu wake kumekuwa na wimbi la hofu ya vijana wengi kuingia katika ushiriki wa siasa za mageuzi kutokana na vitisho.

“Kuna dhana kwamba kijana ukiingia upinzani ndio utakuwa umejifungia kupata ajira serikalini,” alisema Nondo bila kudhibitisha tuhuma hizo.

Hata hivyo, Fahami Matsawili, mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana CCM Taifa, alishauri vyama vingine kama ilivyo CCM kutenga idadi maalumu ya vijana wanaotakiwa kushiriki katika Bunge.

Pia, alishauri vyama kuwa na mpango mkakati wa kuwezesha vijana kushika hatamu za uongozi.