Kikwete aitaka Afrika kubadili ahadi za afya kuwa utekelezaji
Muktasari:
- Mkutano huo umewakutanisha wakuu wa nchi, mawaziri wa afya, watunga sera, viongozi wa taasisi za kikanda na wadau wengine.
Accra. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amezitaka nchi za Afrika kuhamisha mjadala wa afya kutoka kwenye matamko na ahadi za kisera kwenda kwenye utekelezaji unaoambatana na bajeti, uwajibikaji na ubunifu.
Amesema bara hilo linakabiliwa na changamoto katika sekta ya afya, licha ya kuwepo kwa mikakati, maazimio na ahadi nyingi zilizotolewa kwa miaka kadhaa katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Mathalan, amesema takribani wanawake 260,000 hufariki kila mwaka duniani kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua, huku karibu asilimia 70 ya vifo hivyo hutokea katika nchi za Afrika.
Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), ametoa kauli hiyo jana, Julai 20, 2026, katika mjadala wa sera nchini Ghana, pembezoni mwa mkutano maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu afya.
Rais Samia Suluhu Hassan pia, leo, Jumanne, Julai 21, 2026, anasafiri kwenda nchini Ghana kuhudhuria mkutano huo, utakaowakutanisha wakuu wa nchi, mawaziri wa afya, watunga sera, viongozi wa taasisi za kikanda na wadau wengine.
Kikwete amesema umefika wakati Afrika kujenga mifumo imara ya afya inayotegemea zaidi rasilimali zake za ndani badala ya misaada.
Mazingira ya sasa, amesema, yanaonesha wazi kuwa mfumo wa kutegemea misaada ya nje hauwezi kuendelea kuwa nguzo kuu ya huduma za afya barani Afrika.
“Kupungua kwa misaada ya maendeleo kutoka kwa washirika wa kimataifa kunazifanya Serikali za Afrika kutafakari upya namna ya kugharamia sekta hii muhimu,” amesema.
Aidha, ongezeko la madeni ya umma katika mataifa mengi ya Afrika, amesema, limepunguza uwezo wa Serikali kuongeza matumizi ya huduma za kijamii, ikiwamo afya.
Ameeleza kuwa wakati changamoto hizo zikiendelea, mahitaji ya wananchi ya kupata huduma bora za afya yanaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya mifumo ya magonjwa.
“Ujumbe kutoka Eswatini hadi Accra ni mmoja. Afrika lazima izidi kugharamia, kuzalisha na kulinda mustakabali wake wa afya,” amesema Kikwete.
Afya ya mama, mtoto
Amesema eneo moja linalohitaji hatua za haraka zaidi ni afya ya mama na mtoto, ambayo bado inaonesha viashiria vinavyotia wasiwasi katika sehemu nyingi za Afrika.
Ameeleza kuwa takribani wanawake 260,000 hufariki kila mwaka duniani kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.
Karibu asilimia 70 ya vifo hivyo, amesema, hutokea katika nchi za Afrika, jambo linaloonesha ukubwa wa changamoto iliyopo.
Amesema dunia tayari ina maarifa, wataalamu, dawa, vifaa tiba na teknolojia zinazoweza kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya kina mama na watoto.
Kwa sababu hiyo, amesema changamoto iliyopo si ukosefu wa suluhisho, bali kushindwa kuyafikisha suluhisho hayo kwa wananchi wanaoyahitaji.
“Mama anaporudi nyumbani salama, ni kwa sababu fedha, ushahidi wa kisayansi na utoaji wa huduma vimefanikiwa kukutana,” amesema.
Amesema wauguzi, wakunga na wahudumu wa afya ya jamii ndio wanaobeba jukumu kubwa la kuokoa maisha kila siku na wanapaswa kupewa mazingira bora zaidi.
Akizungumzia Tanzania, Kikwete amesema imepiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito vinavyotokana na matatizo ya ujauzito na kujifungua.
Kikwete amesema kiwango hicho kimepungua kutoka zaidi ya vifo 550 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai hadi vifo 104.
Amesema maendeleo hayo yanaifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kufikia lengo la maendeleo endelevu la kupunguza kiwango hicho hadi vifo 70 ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, ameonya kuwa mafanikio hayo hayatadumu bila kuendelea kuwekeza katika mifumo ya afya na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote.
Amesema mjadala wa afya haupaswi kuishia kwenye kiasi cha fedha kinachotengwa pekee, bali uangalie matokeo yanayopatikana kwa wananchi.
“Swali si tunatumia kiasi gani katika afya. Swali ni kama uwekezaji wetu unawafikia wananchi wanaouhitaji zaidi,” amesema Kikwete.
Amebainisha kuwa wananchi hupima mafanikio ya sekta ya afya kwa upatikanaji wa dawa, wataalamu na vifaa tiba badala ya takwimu za bajeti pekee.
Kikwete amesema uwajibikaji unapaswa kuwa msingi wa kila uwekezaji wa afya ili kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaleta thamani inayokusudiwa.
“Uwajibikaji lazima sasa uwe nguzo ya ufadhili wa afya, kwa sababu tukiepuka ubadhirifu, tunaweza kufanya mengi zaidi kwa fedha chache,” amesema.
Katika hatua nyingine, ameitaka Afrika kuongeza uwezo wa kuzalisha dawa, vifaa tiba na chanjo ndani ya bara.
Amesema kwa sasa Afrika inaagiza kutoka nje kati ya asilimia 80 na 100 ya dawa zake, huku zaidi ya asilimia 99 ya chanjo zikitoka nje ya bara.
Hali hiyo, amesema, inaweka mifumo ya afya katika hatari wakati wa migogoro ya kimataifa au kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji.
Amehimiza nchi wanachama kuunga mkono Wakala wa Dawa wa Afrika na kutumia fursa za biashara ya kikanda kuimarisha usalama wa afya.
Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii, Balozi Amma Twum-Amoah, amesisitiza umuhimu wa matokeo.
Amesema mafanikio ya sera za afya yanapaswa kuonekana katika maisha ya wananchi badala ya kubaki kwenye nyaraka na ripoti za utekelezaji.
“Vipaumbele vyetu lazima vionekane katika utekelezaji, na maendeleo yetu yapimwe kwa maboresho yanayopatikana katika maisha ya kila siku ya watu wetu,” amesema.
Ameeleza kuwa Afrika haina upungufu wa ahadi, mikakati wala ubunifu wa kuboresha sekta ya afya.
Amesema changamoto iliyobaki ni kuhakikisha ahadi hizo zinageuzwa kuwa bajeti, bajeti kuwa programu na programu kuwa matokeo yanayoboresha maisha ya wananchi wa bara hilo.