Kikwete aonya ajira kutoweka mwaka 2050, aeleza nini kifanyike

Kikwete aonya ajira kutoweka mwaka 2050, aeleza nini kifanyike

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kutokana na utoaji hafifu wa elimu nchini kuna hatari ya nusu ya ajira zilizopo kutoweka ifikapo mwaka 2050.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kutokana na utoaji hafifu wa elimu nchini kuna hatari ya nusu ya ajira zilizopo kutoweka ifikapo mwaka 2050.

Ameyasema hayo leo Jumanne Mei 18, 2021  wakati akizindua kongamano la elimu linalojadili ufadhili wa elimu lililoandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) jijini Dar es Salaam.

Akieleza utafiti uliofanywa na tume ya kimataifa ya elimu ambayo yeye ni mjumbe, amesema elimu inayotolewa barani Afrika ilitolewa miaka 50 hadi 70 iliyopita kwa nchi zilizoendelea.

"Sisi bado tunatumia chaki, wakati wenzetu wanatumia tablets. Tuliona kuwa kuna watu zaidi ya milioni 263 waliotakiwa kuwa shule lakini hawapo, kati yao milioni 100 wapo Afrika. Kwa waliopo shule wengi hawamalizi shule. Wengi wanaishia njiani. Asilimia 67 wamemaliza shule, asilimia 33 ni idadi kubwa," amesema  Kikwete.

Amesema kutokana na utoaji hafifu wa elimu na maendeleo ya teknolojia kuna janga la ukosefu wa ajira linakuja.

"Ifikapo 2050 asilimia 50 ya kazi zitafutika, kwa sababu ya matumizi ya mashine. Kutakuwa na magari yasiyotumia dereva. Unataka usafiri, unaita Uba, unatumia simu yako inakuja inakupeleka sehemu husika labda Ubungo Plaza au Millennium Tower," amesema.

Amesema mbali na ukosefu wa ajira, idadi ya watu barani Afrika itafikia watu bilioni mbili, “kama watu hao hawana ujuzi unafanya nini? Sijui itakuwaje. Kutakuwa na athari kubwa za kiuchumi na kijamii."

Akisisitiza matumizi ya teknolojia, Kikwete ameshauri kuwepo na uwekezaji katika elimu ili vijana wa Afrika wasiwe watazamaji, wawe washiriki wa uchumi.

"Kunatakiwa kuwepo na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ufundishaji. Kila shule inatakiwa kuunganishwa na intaneti," amesema.

Huku akitoa mfano wa janga la corona, Kikwete amesema limethibitisha jinsi ukosefu wa teknolojia unavyoathiri ufundishaji.

"Tumeona wakati wa corona, moja hatua zilizochukuliwa ni kufunga shule. Wanafunzi wetu hawakusoma, wanacheza rede, lakini nchi zilizoendelea shule zilifungwa na watoto wakaendelea kusoma.”

"Nilipokuwa Rais tulianzisha matumizi ya intaneti katika ufundishaji, tuliwekeza sana kwenye mkongo wa Taifa. Lengo langu lilikuwa ni kuhakikisha kila shule, hospitali ziunganishwe na intaneti. Mwalimu mmoja wa hisabati afundishe nchi nzima,” amesema.

Kuhusu Elimu jumuishi ameitaka Serikali na wadau kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa kukosa elimu.

"Wengine wanadhani msichana ni wa kubaki jikoni. Wengine wameachwa nyuma kutokana sababu za kisiasa.

Tunatakiwa kuhusisha mashirika yasiyo ya kiserikali kuchangia elimu," amesema.

Awali akimkaribisha Kikwete mwenyekiti wa Tenmet, Dk John Kalage ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi ya HaliElimu amesema kongamano hilo litajadili kwa kina njia za ufadhili wa elimu nchini.