Kikwete atoa neno kwa Dk Biteko

Muktasari:

  • Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema mdomo umeumbwa kusema, akimshauri Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko kuchapa kazi.

Chalinze. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amemweleza Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko kwamba uteuzi wake katika nafasi hiyo ni uamuzi sahihi na kwa wakati ulio sahihi.

Amemshauri iwapo atasikia minong’ono kutoka kwa baadhi ya watu kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amevunja Katiba kumteua, alale usingizi kisha afanye kazi zake vizuri.

Kikwete amesema hakuna atakayekwenda mahakamani kwa ajili ya uteuzi huo, hivyo Dk Biteko achape kazi.

Amesema hayo kwenye mkutano wa wanachama na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Chalinze uliopokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Kikwete amehudhuria mkutano huo uliofanyika leo Jumatano Oktoba 11, 2023 akiwa mgeni mwalikwa.

Amesema Rais Samia amemuamini kwa kuwa amemuona anafaa, hivyo anampongeza kwa chaguo zuri.

"Nawapongeza mawaziri, mbunge wa Chalinze na wa Bagamoyo na wengine kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Nawaomba muendelee kufanya kazi na kumsaidia Rais kwa uadilifu,” amesema.

Amesema, “Mwisho lakini si mwisho kwa umuhimu nampongeza Naibu Waziri Mkuu Biteko kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo. Anastahili kwa utendaji wake wa kazi uliotukuka. Midomo imeumbiwa kusema, hivyo wapo baadhi wanaosema Rais kavunja Katiba, hakuna iliyovunjwa.”

Kikwete amesema viongozi wanaotajwa kwenye katiba ni Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu, hivyo kama Rais Samia angesema anaweka Waziri Mkuu wa pili hapo angekiuka Katiba.

Dk Biteko aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo; mbali ya kusifia utekelezaji wa ilani ya CCM amewaasa wanachama na viongozi kufanya siasa za maendeleo.

Amesema wananchi watawapima kwa kazi wanazofanya na si maneno mengi ya jukwaani.

"Wana-Chalinze nimepokea taarifa yenu mnakwenda vizuri katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ya maendeleo," amesema.

Amesema ili kuendeleza utendaji kazi wenye mafanikio, wanapaswa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano.

Awali, mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema wamefikisha asilimia 96 ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM jimboni humo kwa kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi.

Amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri nchini, ikiwamo ya Chalinze.

Ridhiwani ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ya barabara, umeme na vituo vya afya.