Kikwete: Mambo ya birthday kwa umri wetu ni mapya

Muktasari:
- Kikwete aeleza jinsi watoto walivyomzoesha kuesherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Dar es Salaam. Wakati leo akitimiza miaka 72 Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kwake sherehe hiyo sio jambo kubwa kwake na wakati mwingine huwa anasahau hadi akumbushwe na watoto wake.
Kikwete amesema analazimima kuzoea utaratibu huo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa kuwa hajakulia katika misingi hiyo.
“Haya mambo ya birthday kwa watu wenye umri wangu ni mapya, nimezaliwa kijiji hapa hakuna mtu anayekumbuka kila mtu anaendelea na shughuli zake, hawa vizazi vya siku hizi ndio wanakumbuka.
“Nakumbuka binti yangu Mwanaasha alipokuwa mdogo siku yake ya birthday alitegemea keki, mimi sikuwa na mawazo hayo aliniuliza kama nimemletea nikamwambia sijaleta, akanikasirikia sana,” amesema Kikwete.
Kikwete amesema binti huyo alimwambia wazi kuwa amekasirika na hataki kuzungumza naye, ujumbe huo ulimfanya atoke kwenda kutafuta keki.
“Nikaona eeh, makubwa haya nikamwambie dereva twende tukatafute, tukaenda kwenye maduka huko tulipata niliporudi nikamwambia nilichelewa kuifuata ila niliandaa, akafurahi sana na ugomvi ukaisha,” amesema Kikwete.
Mke wa Rais huyo mstaafu, Salma Kikwete akampa salam zake za pongezi, “Namtakia kila la heri mume wangu, mpenzi wangu na rafiki yangu wa karibu. Miaka 72 sio kitu kidogo.”