Kikwete: Wanawake mnaupiga mwingi

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Jakaya Kikwete akiwatunuku Digrii ya Awali ya Usanifu Majengo wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye mahafali ya 53 ya chuo hicho jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Nderemo na vifijo vimeibuka katika duru la tatu la mahafali ya 53 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya Mkuu wa Chuo hicho ambaye ni Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete kutoa pongezi kwa wahitimu wanawake kwa kuhitimu kwa idadi kubwa ya asilimia 57.2.

Katika mahafali hayo ya awamu ya tatu wanafunzi takribani 2,609 wametunukiwa shahada za awali na astashahada kati yao wanawake ni 1,492 huku wanaume wakiwa 1,117.

"Hongereni wahitimu wanawake mnaupiga mwingi," amesema Kikwete kauli ambayo iliibua shangwe na vigeregere miongoni mwa washiriki wa mahafali hayo.

Akizungumza katika mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kuleta ushawishi chanya katika jamii huku akiwakumbusha kuwa elimu waliyoipata ni mali ya umma hivyo ni lazima ilete faida kwa Watanzania.

"Elimu haiwezi kuleta faida na kuwa chachu ya mabadiliko yaliyokusudiwa kama haitatumika katika kutatua matatizo ya jamii,"amesema.

Pia, amewataka kuwa wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi kuliko kusubiri ajira serikalini au katika sekta binafsi.

"Muwe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate, jambo ambalo si rahisi kutokea katika dunia ya leo ambayo ni kijiji chenye ushindani mkubwa.

"Mtakapokuwa mnatekeleza wajibu wenu wa kujitafutia maisha mazuri na kuendeleza nchi yetu, muwe na hulka ya kuthubutu mambo ambayo yanaonekana ni magumu," amesema.

Vilevile amewakumbusha wahitimu kuwa wazalendo kwa nchi kudumisha tunu za amani, umoja, mshikamano wa nchi.

Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Balozi Mwanaidi Maajar amesema baraza hilo linafahamu na linatambua madhara mbalimbali yanayosababishwa na uzembe wa wanafunzi kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Amesema baraza linaendelea kuwasisitiza wazazi na walezi kusimamia misingi bora ya malezi kwa watoto haswa katika kipindi hiki cha utandawazi kwani bila kufanya hivyo kutakuwa na kizazi tegemezi ambacho hakiwezi kuwajibika ipasavyo.

"Ninaisihi jamii na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini, kurudi kwenye misingi bora ya malezi kwa kuliangalia suala hili kwa jicho la kipekee ili kulinusuru taifa letu la kesho na madhara yatokanayo na kizazi kisichowajibika," amesema Maajar