Kila saa moja watu 30 wanakufa kwa kuzama majini
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Jamii yatakiwa kuungana kupunguza vifo vya kuzama kwa asilimia 35 ifikapo 2035.
Dar es Salaam. Zaidi ya watu 300,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuzama majini duniani, sawa na wastani wa watu 30 kila saa, huku karibu robo ya vifo hivyo vikiwahusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi hiyo ni ongezeko kutoka watu 236,000 vilivyorekodiwa mwaka 2024.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, WHO imetumia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vifo vya Kuzama Majini, inayoadhimishwa Julai 25 kila mwaka, kuhimiza serikali, jamii na wadau mbalimbali kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kaulimbiu ya mwaka 2026 ni "Unite to Turn the Tide" (Tuungane Kubadili Mwelekeo), ikisisitiza kuwa kila mtu ana nafasi ya kuchangia kupunguza ajali za kuzama.
WHO inaeleza kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana katika miaka ya karibuni, kuzama bado ni miongoni mwa sababu 10 zinazoongoza kusababisha vifo kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 14 duniani.
Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na kuzama hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambapo watu wengi huzama kwenye mito, maziwa, visima, matenki ya kuhifadhi maji, vyombo vya kuhifadhia maji majumbani na mabwawa ya kuogelea.
Watoto na vijana wanaoishi maeneo ya vijijini ndio wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wa tatizo hilo.
WHO kupitia mkakati wa kimataifa wa kuzuia vifo vya kuzama imeweka lengo la kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 35 ifikapo mwaka 2035, ikisisitiza kuwa mafanikio hayo yatapatikana ikiwa sekta zote na jamii kwa ujumla zitashiriki.
Kwa mujibu wa WHO, wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanasimamiwa kila wanapokuwa karibu na maji, kufunika au kuweka uzio kwenye mabwawa na vyanzo vya maji majumbani, kuwafundisha watoto kuogelea pamoja na usalama wa majini, na kujifunza huduma ya kwanza ya kufufua moyo na mapafu (CPR), pamoja na mbinu salama za uokoaji.
Shirika hilo pia linazitaka shule kujumuisha elimu ya usalama wa maji katika mitaala na kuwapatia wanafunzi maarifa ya kujikinga na ajali za kuzama.
Kwa wafanyakazi wanaofanya kazi karibu na maji, WHO inapendekeza matumizi ya jaketi za kuokoa maisha, mafunzo ya usalama kazini na kuripoti mazingira yoyote yasiyo salama.
Waajiri wanashauriwa kuhakikisha wanatoa vifaa vya usalama, mafunzo stahiki na kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama mahali pa kazi.
Viongozi wa jamii wanahimizwa kutambua maeneo yenye hatari ya kuzama, kuendesha mafunzo ya kuogelea na uokoaji pamoja na kuimarisha mifumo ya tahadhari dhidi ya mafuriko.
Kwa upande wa serikali, WHO inataka kuwepo kwa sheria zinazolinda usalama wa wananchi wanapokuwa karibu na maji, kuongeza uwekezaji katika programu zilizothibitishwa kupunguza vifo vya kuzama na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali.
Dunia imepiga hatua,
lakini kazi bado ipo
WHO inakumbusha mwaka 2021, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilitangaza rasmi Julai 25 kuwa Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vifo vya Kuzama Majini, likitambua tatizo hilo kuwa kipaumbele cha afya duniani.
Tangu mwaka 2000, kiwango cha vifo vinavyotokana na kuzama duniani kimepungua kwa asilimia 38, lakini WHO inaonya kuwa maelfu ya maisha bado yanapotea kila mwaka kutokana na ajali zinazoweza kuzuilika.
Shirika hilo linasisitiza kufikia lengo la kupunguza vifo kwa asilimia 35 ifikapo mwaka 2035 kutategemea ushiriki wa kila mtu.