Kilichofanya John Malecela aheshimike madarakani, baada ya kung'atuka

Mzee John Malecela akiwa katika Kanisa la Anglikana la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) mjini Dodoma, aliposhiriki ibada ya kutoa shukrani kwa Mungu kwa kutimiza umri wa miaka 90 leo Aprili 21, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Malecela aliyezaliwa Aprili 19, 1934 ametimiza miaka 90, sifa zake kuu zatajwa

Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amesheherekea kutimiza miaka 90 ya kuzaliwa, ikielezwa weledi wake umemfanya aheshimike akiwa madarakani na hata baada ya kung'atuka kwenye nafasi za uongozi.

Malecela aliyezaliwa Aprili 19, 1934, leo Aprili 21, 2024 ametoa shukrani kwa Mungu aliposhiriki ibada katika Kanisa la Anglikana la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) mjini Dodoma.

Ibada hiyo iliambatana na sherehe ya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi.

Katika maisha yake, Malecela amewahi kuhudumu kwenye nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, mbunge wa Mtera, waziri kwenye wizara mbalimbali, waziri mkuu na makamu wa Rais.

Pia amewahi kushika nafasi za uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo ya makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara.


Ukombozi Bara la Afrika

Katika hafla hiyo, Rais Mwinyi amemwelezea Malecela kuwa mbali ya kushika nafasi hizo za uongozi nchini amehusika kwa sehemu kubwa kuzikomboa nchi za kusini mwa Bara la Afrika, alipokuwa waziri wa Mambo ya Nje.

"Sote tunatambua na kuthamini mchango mkubwa wa mzee wetu katika nafasi mbalimbali za uongozi na utumishi kwenye Taifa letu.

Katika nafasi hizo alisema Mzee Malecela amekuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kusimamia na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.

Amesema alikuwa miongoni mwa watu saba wenye busara walioteuliwa na Jumuiya ya Madola kuongoza mazungumzo dhidi ya makaburu wa Afrika Kusini, yaliyowezesha kuachiwa kwa, Nelson Mandela na baadaye kuipatia nchi hiyo uhuru.

Dk Mwinyi amesema Malecela alijituma na kujitoa kwa CCM, jambo lililokifanya chama hicho kuona haja ya kumteua kuwa makamu mwenyekiti wake Tanzania Bara, nafasi ambayo kwa sasa inashikwa na Abdulrahman Kinana ambaye pia alihudhuria hafla hiyo.


Sifa tatu za Malecela

Akimzungumzia mzee huyo, Kinana amesema ana sifa kuu tatu ikiwamo ya uzalendo.

Amesema ikiwa atakuwa na jambo lake na likatokea linaloihusu nchi, basi Malecela angeachana na lake na kufanya la Tanzania.

"Jambo la pili, ni mzee mwenye busara katika Taifa hili, ukiachana na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Ali Hassan Mwinyi, kiongozi pekee nchi hii aliyepata uongozi wa juu katika Taifa hili, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Afrika na duniani mpaka akawa mtu mashuhuri, si kwa kutaka bali kwa kuteuliwa na Jumuia ya Madola, ni mmoja tu, Mzee Malecela," amesema Kinana.

Kinana aliyesema amefunzwa uongozi na Malecela, ametaja sifa yake ya tatu kuwa ni uvumilivu na anayejua kupima ni wakati gani wa kuchukua hatua gani na ni wakati gani wa kuchukua uamuzi gani, jambo lililomfanya kuheshimika kwenye uongozi wake na hata baada ya kustaafu.

"Chama cha Mapinduzi kinatambua mchango wako mkubwa katika kukijenga chama hiki na katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa na imani na chama hiki," amesema.


‘Mtumieni kama hazina’

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amemwelezea Malecela kuwa ameishi miaka 90 ya umri wake vizuri.

Akitumia msemo wa Mzee Mwinyi kuwa maisha ni kuandika historia ili utakapokufa watu waisome historia yako nzuri, Sumaye amesema Malecela ameandika historia nzuri na ya kupendeza.

"Wazee kama hawa si wengi, kwa hiyo tunachotakiwa hasa ninyi ambao ni vijana-vijana wale ambao mna uwezo wa kumfikia Mzee Malecela mna bahati kubwa, wewe Mkuu wa Mkoa, Rosemary Senyamule, viongozi wa chama hata asubuhi wakati wa kunywa chai unamwambia mama unaomba uje ukanywe chai nyumbani kwa mzee upate busara za kuongoza nchi na kuongoza chama," amesema.

Amemwelezea Malecela kuwa ni hazina kubwa kwenye Taifa, na licha ya kuonekana kama vile amezeeka, lakini kuna mambo mengi yanayohusu Taifa ambayo anayajua.

Sumaye amesema ni mtu aliyekuwa tayari muda wote akitumwa.


Mke na begi uwanja wa ndege

Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amesema Malecela ni mtu ambaye Taifa litaendelea kumuenzi kwani ameshika karibu nafasi zote na ni mtu ambaye akiingia mahali anafanya kwa uadilifu na uaminifu bila kujali ataathiri vipi wale waliopo karibu naye.

"Nakumbuka kwenye vita hivi vya Afrika, John alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na alitumwa nafikiri kwenda Uganda, alipoenda huko akarudi tukaitwa baraza lote la mawaziri na yeye alivyotua tu akaja kwenye baraza,” amesema.

“Tulivyomaliza tu pale akatumwa tena kwenda Somalia kuonana na Rais wa nchi hiyo na alikuwa ameshatuma begi lake nyumbani," amesema Msuya.

"Alimwambia mke wake alete begi uwanja wa ndege na sisi tuliomsindikiza tukaona kweli mke wake alivyokuja akawa analia, wewe umekuwa mtu wa kusafiri tu kila siku na mimi nakuletea mabegi uwanja wa ndege, hii ni ndoa gani hii," ameeleza.

Msuya amesema Malecela alikuwa mtu wa kujitoa na kuweka masilahi ya Taifa lake mbele, akisalia kuwa hazina kubwa kwenye Serikali na Taifa kwa ujumla.


Alivyowakilisha Dodoma

Spika mstaafu wa Bunge, na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amesema Malecela amewakilisha vyema wana - Dodoma na Tanzania katika maeneo mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Marry Chatanda amempongeza Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambaye ni mke wa Malecela kwa kumtunza vyema mzee huyo hadi kufikisha umri huo.


Kujitoa kwa familia

Profesa Secelela Malecela ambaye ni mtoto Malecela amemwelezea baba yake kuwa ni mtu aliyejitoa kwa familia.

Amesema kuna wakati alitumwa Ujerumani na baada ya kutoka huko alienda kwenye sherehe za watoto wake kwenye shule tatu kwenye mikoa mitatu tofauti.

"Nakumbuka kulikuwa na kama kongamano hivi la kupiga kinanda kila mtoto alikuwa anakuja na wazazi wake anapiga kinanda, hivyo mimi nikaja na karatasi nikampa, akaniambia  nitakuwepo kwenye shughuli yako kwa hiyo tukawa tunafanya mazoezi wote. Sasa kukatokea mkutano wa FAO (Shirika la Chakula na Kilimo Duniani) nchini Ujerumani, sasa baba ikabidi aende, mimi nikakata tamaa hatakuwepo, lakini alitoka Ujerumani akiwa amevaa nguo za joto akaja nazo mpaka kwenye kongamano shuleni, akiwa anatokwa jasho, hakujali alikuwepo," ameeleze Profesa Secelela.


Utani kwa Anne Kilango

Wakati wa sherehe iliyofanyika nyumbani kwake leo, akitoa neno la shukrani, Malecela amewavunja mbavu waliohudhuria alipomsimamisha mke wake Anne na kumwambia, kwa jinis anavyompenda, akimsikia anamsemea maneno mabaya mahali, basi aelewe atakuwa amelewa.