Kilichotokea kesi ya rasilimali za Chadema
Viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Haya ni maombi ya zuio la muda dhidi ya Chadema kufanya siasa na kutumia mali zake, yanayotokana na kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya chama hicho baina ya Bara na Zanzibar.
Dar es Salaam. Jopo la mawakili wa makamu mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Mohamed, pamoja na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Ahmed Khamis, limeiomba Mahakama iwapatie siku saba kujibu hoja mpya zilizoibuliwa na Chadema katika shauri la madai la mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama hicho baina ya Bara na Zanzibar.
Jopo hilo la mawakili waandamizi, Mulamuzi Byabusha, Shaaban Marijani na Alvan Fidelis, limefikia hatua hiyo leo, Jumatatu Julai 6, 2026, mbele ya Jaji Awamu Mbagwa katika shauri la maombi madogo ndani ya kesi ya msingi ya kutaka itolewe amri ya Chadema kutojihusisha na shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama.
Shauri hilo namba 13832/2026 limefunguliwa dhidi ya Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho (wadaiwa), kwa madai kuwa kuna upendeleo katika mgawanyo wa rasilimali ndani ya chama hicho.
Ndani ya shauri hilo, wadai waliwasilisha maombi madogo ya kuomba zuio la muda la chama hicho kutojihusisha na shughuli za kisiasa, ambapo leo yalitakiwa kusikilizwa baada ya upande wa wadaiwa kuwasilisha viapo kinzani vya Katibu Mkuu huyo na wajumbe wa bodi hiyo.
Nje ya Mahakama:
Marijani, akiwa nje ya Mahakama, alisema leo, Jumatatu Julai 6, 2026, ilikuwa siku ya kusikilizwa kwa maombi hayo, lakini Ijumaa walipokea viapo kinzani kutoka kwa mdaiwa wa kwanza na wa pili vilivyoambatanishwa na pingamizi la awali lenye hoja takribani tisa.
"Leo tulikuwa kwa ajili ya kusikiliza shauri, lakini tumeomba muda wa kupitia kwa undani viapo hivyo ili kuweza kujibu pingamizi zao za awali ambazo wameziwasilisha ndani ya muda mfupi. Mahakama ikaruhusu na ikatupa amri ya kuyasikiliza pingamizi hayo kwa njia ya maandishi, tukapewa kalenda ya kujibizana kwa njia hiyo," alisema Marijani.
Vilevile alisema kulikuwa na viapo kinzani na baada ya kuona viapo hivyo vya mjibu maombi wa kwanza na wa pili, walibaini kuwa kuna mambo mapya yaliyokuwa yameibuliwa, hivyo wakaona kuna haja ya wateja wao kupata fursa ya kuyajibu ili kuiwezesha Mahakama kufanya uamuzi sahihi kuhusu maombi hayo.
"Hivyo, tukaiomba Mahakama itupatie muda ili kuweza kuandaa viapo vya kujibu viapo kinzani vya wadaiwa kwa mambo ambayo yameanzishwa. Kwa hiyo tukapewa ratiba ya kujibizana katika viapo hivyo. Kesi imepangwa kutajwa Agosti 5, 2026," aliongeza Wakili Marijani.
Kwa upande wa mawakili wa Chadema, wakiongozwa na Dk Rugemeleza Nshala na Hekima Mwasipu, alisema majibu yao waliyawasilisha Julai 2, 2026, yakiwa ni viapo kinzani vya Katibu Mkuu wa Chadema na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, na wakawapatia pia upande wa wadai.
"Wenzetu wameomba ruhusa ya siku saba ya kuwasilisha majibu yao juu ya viapo hivyo kinzani, ambapo Mahakama imewakubalia. Kwa hiyo watawasilisha majibu yao Julai 13, 2026," alisema Dk Nshala na kuongeza:
"Pingamizi letu la awali, ambalo tumeliwasilisha, litasikilizwa kwa njia ya maandishi. Kila upande umepewa siku 10. Sisi tutaeleza kwa nini tunafikiri pingamizi tulizoweka zina msingi, na wao waliomba wapatiwe siku saba kwa ajili ya kujibu," alisema Dk Nshala.
Hata hivyo, alisema Mahakama imeamua majibu yao yawasilishwe Julai 16, 2026, na wadai watajibu Julai 23, 2026, huku wao wakipewa siku saba nyingine za kujibu majibu hayo, ambayo watayawasilisha Julai 30, 2026.
"Mahakama itakutana na sisi Agosti 5, 2026, kwa ajili ya kuangalia kama wametekeleza amri ambazo imetoa kikamilifu, saa tano asubuhi," alisema Dk Nshala.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Madai mengine ni ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yenye nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo, pamoja na mambo mengine, waliomba Mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na itoe zuio la kudumu la matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Kwa mara ya kwanza, kesi hiyo ilitajwa Juni 15, 2026.