Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema kujibu madai kesi ya rasilimali Julai Mosi

Viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kesi hii ni mwendelezo wa kesi kama hiyo iliyofutwa awali kutokana na kasoro za kisheria ambayo imerejeshwa tena baada ya wadai kurekebisha kasoro hizo zilizobainishwa na Mahakama.

Dar es Salaam. Mchakato wa usikilizwaji wa kesi ya madai ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa ndani ya  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya Tanzania Bara na Zanzibar umeanza baada ya kesi hiyo kutajwa kwa mara ya kwanza leo Jumatatu, Juni 15, 2026.

Kesi hiyo ya madai namba 13832 ya mwaka 2026 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar, Said Issa Mohamed, na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Wadai wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Madai mengine ni ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo pamoja na mambo mengine wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Kesi hiyo ambayo imepangwa kusikilizwa na Jaji Awamu Mbagwa, imetajwa leo Juni 15, 2026 kwa mara ya kwanza tangu ilipofunguliwa, kwa ajili ya kuangalia kama ubadilishanaji nyaraka umeshakamilika na mahakama kutoa maelekezo muhimu.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Shaban Marijani ameieleza mahakama kuwa tayari wameshawapatia wadaiwa nyaraka za kesi hiyo ingawa bado hawajawasilisha majibu yao dhidi ya madai ya wadai.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa, Dk Rugemeleza Nshala amekiri ni kweli  wameshapatiwa nyaraka za kesi hiyo na  bado hawajawasilisha majibu yao dhidi ya madai.

Hata hivyo wakili Nshala amesema bado wako ndani ya muda wa siku 21 ambazo watakiwa kuwasilisha majibu hayo kwa mujibu wa sheria, ambazo amesema zinaisha Julai Mosi, 2027, tarehe ambayo ndio waliyopanga kuwasilisha majibu yao.

Kwa kuwa upande wa wadai haukuwa na pingamizi, Jaji Mbagwa amekubaliana na hoja hiyo na akaelekeza wadaiwa wawasilishe majibu yao Julai Mosi, 2026 kama walivyoomba.

Kisha Jaji Mbagwa amepanga kesi hiyo itajwe kwa mara nyingine Julai 8, kwa ajili ya amri muhimu za mahakama kuhusiana na utaratibu wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Kesi hii ni mwendelezo wa kesi kama hiyo iliyokuwa imefunguliwa awali kabla ya kufutwa na Mahakama.

‎Awali, kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo na Mohamed, Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa), ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Chadema kutoka Zanzibar dhidi ya wadaiwa hawa wa sasa.

‎Hata hivyo, kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ambayo awali ilisikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, ilifutwa na Jaji David Ngunyale Mei 28, 2026, kabla ya kuisikiliza madai ya msingi kufuatia pingamizi la awali ambalo liliibuliwa na wadaiwa.

Mahakama ilikubaliana na hoja za pingamizi la Chadema kuwa hati ya madai ina kasoro za kisheria kutokana na kutokubainisha kuwa mambo yaliyokuwa yamelalamikiwa na wadai yalianza lini. kinyume na Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC).

Jaji Ngunyale alisema kuwa kutokana kasoro hiyo ya hati ya madai kutobainisha dhahiri kuwa mambo wanayoyalalamikia yalianza lini kwa mujibu wa Sheria ya Ukomo, kunaifanya mahakama ishindwe kuamua kama ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo au la.

"Katika mazingira hayo, mahakama hii inaona kuwa hati ya madai ina kasoro za kisheria na hivyo inaitupilia mbali," alisema Jaji Ngunyale akihitimisha uamuzi huo na kuelekeza kila upande ubebe gharama zake za uendeshaji kesi hiyo.

Hata hivyo, siku chache tu baada ya kesi hiyo kufutwa wadai hawa wawili walirudi mahakamani hapo ambapo walifungua upya kesi hiyo baada ya kurekebisha kasoro za kisheria zilizobainishwa na mahakama, huku madai yakibakia yaleyale kama yanayosomeka katika kesi ya sasa.

Hata hivyo wakati kesi hii ya sasa ikisubiriwa kusikilizwa, tayari Chadema Zanzibar kimeshatangaza kumvua uanachama Mohamed.