Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyefukuzwa Chadema apinga, wenyewe wapigilia msumari

Muktasari:

  • Amesema bado anajiona mwanachama halali wa Chadema kwa kuwa hakuitwa kujibu tuhuma wala kupewa nafasi ya kujitetea kama inavyotakiwa na taratibu za chama hicho kabla ya kufikia uamuzi huo.



Dar es Salaam. Siku moja baada ya kufutwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Issa Mohammed amesema hatua hiyo ni ya kihuni na haikufuata taratibu za chama, huku akiweka msimamo bado ni mwanachama halali anayelindwa na katiba ya Chadema.

Taarifa ya Said kufutwa uanachama ilitolewa jana Jumapili, Juni 7, 2026, kwa uamuzi wa Kamati tendaji ya Kanda ya Pemba uliofikiwa katika kikao cha dharura kilichofanyika Juni 6, 2026, Chake Chake, Pemba.

Hatua hiyo ilitokana na ushiriki wake katika kufungua shauri la madai Na. 8323 la mwaka 2025 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama.

 Katika shauri hilo, yeye pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (sasa ni marehemu), walidai kuwapo kwa mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hata hivyo, Mei 28, 2026, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kubaini kasoro za kisheria katika hati ya madai, ikiwemo kushindwa kuainisha tarehe ya kuanza kwa ukiukwaji uliodaiwa. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Juni 8, 2026, Said amesema hakuwahi kupewa taarifa rasmi wala nafasi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wa kumfukuza kufikiwa.

“Mwanachama wa chama si kama wakijiwe, mwanachama wa chama analindwa na kanuni, maadili na katiba ya chama. Ili mwanachama afukuzwe uanachama, utaratibu lazima ufuatwe. Mimi sijapewa taarifa yoyote rasmi, nimeona tu taarifa hizo zikisambaa kwenye mitandao,” amesema.

Amesema bado anajiona mwanachama halali wa Chadema kwa kuwa hakuitwa kujibu tuhuma wala kupewa nafasi ya kujitetea kama inavyotakiwa na taratibu za chama hicho.

“Katiba ya chama inaeleza wazi haki za mwanachama. Anapotuhumiwa, anatakiwa kuitwa katika kikao halali, kupewa tuhuma zake na nafasi ya kujieleza au kujitetea."

"Baada ya hapo ndipo vikao husika vinaweza kufanya uamuzi. Sijaona taratibu hizo zikifuatwa, ndiyo maana nasema kilichofanyika ni uhuni,” amesema.


'Tulimpa siku 14'

Akizungumza na Mwananchi kufafanua madai ya Said,

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pemba, Omar Nassor amesema  alipewa nafasi ya kujitetea kupitia barua ya kutakiwa kutoa maelezo ndani ya siku 14, lakini katika kipindi chote hicho hakuwasilisha majibu yoyote.

“Kamati tendaji ilifanya kikao chake Mei 23, 2026, na baada ya hapo alipewa barua ya kujieleza ndani ya siku 14. Katika kipindi hicho hakutoa majibu yoyote na alibaki kimya. Baada ya muda huo kumalizika, Juni 6, 2026, tulifanya kikao kingine na kufikia uamuzi huo,” amesema.

Nassor amesema kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, si lazima mwanachama aitwe mbele ya kikao kwa kila kosa linalodaiwa kufanywa. Badala yake, anaweza kupewa barua inayoeleza tuhuma zinazomkabili na kupewa nafasi ya kujitetea, kama ilivyofanyika katika suala hilo.

“Tulimpa nafasi ya kujitetea, lakini hakuitumia na alibaki kimya. Baada ya siku 14 kupita, kikao kilifanyika na kufikia uamuzi huo, ambao ni halali kwa mujibu wa kanuni na katiba yetu. Hivyo, kwa sasa si mwanachama wetu tena,” amesema Nassor.

Baada ya majibu haya ya Chadema, Mwananchi limemtafuta tena Saidi kujua barua hiyo aliyopewa lakini amesema atafutwe baadaye.


Taarifa ya Chadema

Kwa mujibu wa taarifa ya umma iliyotolewa jana Juni 7, 2026, na Katibu wa Kanda ya Pemba, Abdulla Hassan, Kamati Tendaji ilifikia uamuzi huo baada ya kujadili suala la nidhamu la Said kwa kuzingatia Katiba, kanuni na miongozo ya chama.

“Baada ya kupokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa mbele yake, Kamati ilijiridhisha kuwa Said Issa Mohammed amekiuka katiba, kanuni na miongozo ya chama. Kutokana na ukiukwaji huo, Kamati tendaji ya Kanda ya Pemba imeazimia kumfukuza uanachama kuanzia Juni 6, 2026,” alisema Hassan.

Alisema kuanzia tarehe hiyo, Said Issa Mohammed hatambuliki tena kama mwanachama, kiongozi wala mwakilishi wa Chadema katika ngazi yoyote ya chama.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika. Chama hicho kimesema kuwa kauli, matendo au shughuli zozote atakazozifanya Said Issa Mohammed baada ya kufukuzwa kwake zitakuwa ni za kwake binafsi na hazitahusishwa kwa namna yoyote na Chadema.