Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yamfuta uanachama aliyekishtaki mahakamani

Muktasari:

  • Hatua ya kufukuzwa kwa Said Issa Mohammed inatokana na ushiriki wake katika kufungua Shauri la Madai Na. 8323 la mwaka 2025 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemfukuza uanachama Said Issa Mohammed kwa kosa la kukiuka katiba, kanuni na miongozo ya chama hicho baada ya kukishtaki mahakamani.

Uamuzi huo umefikiwa na Kamati tendaji ya Kanda ya Pemba katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana Jumamosi, Juni 6, 2026, Chake Chake, Pemba, chini ya uongozi wa mwenyekiti wa kanda hiyo, Omar Nassor.

Hatua ya kufukuzwa kwa Said Issa Mohammed ambaye amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar  inatokana na ushiriki wake katika kufungua Shauri la Madai Na. 8323 la mwaka 2025 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika shauri hilo, yeye pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (sasa marehemu), walidai kuwepo kwa mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hata hivyo, Mei 28, 2026, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitupilia mbali na kufuta kesi hiyo baada ya kubaini hati ya madai ilikuwa na kasoro za kisheria, ikiwemo kushindwa kuainisha bayana tarehe ya kuanza kwa ukiukwaji uliodaiwa. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, Chadema ilikuwa imekata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, hatua iliyopelekea chama hicho kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa Aprili 15, 2026.

Pamoja na ushindi huo wa kisheria, chama kilikuwa kimekaa siku 309 bila kufanya shughuli zozote za kisiasa kutokana na mwenendo wa shauri hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Juni 7, 2026 na Katibu wa Kanda ya Pemba, Abdulla Hassan, Kamati tendaji ilikutana kwa ajenda ya kujadili suala la nidhamu linalomuhusu Said Issa Mohammed na kufanya tathimini kwa kuzingatia masharti ya katiba, kanuni na miongozo ya chama.

“Baada ya kupokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa mbele yake, kamati ilijiridhisha Said Issa Mohammed amekiuka katiba, kanuni na miongozo ya chama. Kutokana na ukiukwaji huo, Kamati tendaji ya Kanda ya Pemba imeazimia kumfukuza uanachama kuanzia Juni 6, 2026,” amesema Hassan.

Amesema kuanzia tarehe hiyo, Said Issa Mohammed hatambuliki tena kama mwanachama, kiongozi wala mwakilishi wa Chadema katika ngazi yoyote ya chama.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika. Jitihada za kumsaka Said zinaendelea.

Chama hicho kimesema kauli, matendo au shughuli zozote atakazozifanya Said Issa Mohammed baada ya kufukuzwa kwake zitakuwa ni za kwake binafsi na hazitahusishwa kwa namna yoyote na Chadema.

Kesi hiyo ndiyo iliyozua mjadala mkubwa, huku baadhi ya wadau na wapenda demokrasia wakiihoji na kuielezea ilikuwa na mwelekeo wa kisiasa uliolenga kukidhoofisha chama hicho.

Kwani katika kipindi hicho, hata viongozi wa chama hawakuruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa na waliojaribu kufanya hata vikao vya ndani walijikuta mikononi mwa Polisi.

Mbali na hilo, kwa muda wa siku 309, mali na ofisi za chama hicho zilifungwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama vilivyokuwa vikitekeleza agizo la Mahakama kwa kuhakikisha shughuli zote za chama zinasitishwa.

Wakati mwingine, baadhi ya viongozi wa chama waliokuwa wakijaribu kufanya mikutano ya ndani walijikuta wakikamatwa na Jeshi la Polisi. Hali hiyo iliwalazimu viongozi hao kubuni utaratibu wa kufanya mikutano kupitia mitandao ya kijamii.

Katika kipindi hicho, viongozi mbalimbali, akiwemo Heche, walilazimika kutumia mitandao ya kijamii kutoa hotuba na kueleza misimamo ya chama kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Pia, bendera za chama hicho hazikupepea katika nguzo za ofisi zake kama ilivyo sasa. Hali hiyo ilishusha morali ya wanachama na wapenda demokrasia wengi ambao hawakuridhishwa na hatua hiyo.