Kilio cha wananchi Ulyankulu bado mfupa mgumu

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Festo Dugange wakati akijibu maswali bungeni leo Ijumaa Novemba 3, 2023.

Muktasari:

  • Imekuwa ni kawaida kwa wabunge kuwasilisha malalamiko yao kwa Serikali, hasa wanapoona wananchi katika majimbo wanayoyaongoza, wamesahaulika katika mambo kadhaa. Hivi ndivyo ilivyotokea bungeni leo ambapo Mbunge wa Ulyankulu (CCM), Rehema Migilla amelalamikia kukosekana kwa vitambulisho vya Taifa na Uchaguzi kwa Wapiga kura wake.

Dodoma. Serikali imetoa sababu za kwa nini haifanyi uchaguzi wa udiwani katika kata tatu za jimbo la Ulyankulu mkoani Tabora.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Festo Dugange amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa muingiliano wa makazi ya wakimbizi na raia, hali ambayo huathiri utekelezaji wa shughuli za uchaguzi ndani ya maeneo hayo.

Dk Dugande ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 3, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu (CCM), Rehema Migilla ambaye ametaka kujua kuna mpango gani kuruhusu Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Udiwani Ulyankulu.

Naibu Waziri amesema Serikali inatambua uwepo wa Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na kwamba inaendelea kushughulikia suala hilo chini ya Ofisi ya Rais – Tamisemi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuhakikisha wananchi wa Kata hizo wanapata haki ya kushiriki kwenye shughuli za uchaguzi.

Kilio cha wananchi wa maeneo hayo kilianza siku nyingi ambapo mbunge aliyemaliza muda wake John Kadutu, wakati wote alikuwa akilalamikia maeneo hayo ikiwemo kilio cha kuwapatia vitambulisho wa Taifa (Nida) lakini majibu yameendelea kuwa ni sababu za “muingiliano.”