Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilowati 100 zaanza kuingizwa gridi ya Taifa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza na ujumbe kutoka Misri ukiongozwa na Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa nchi hiyo, Assem Elgazzar katika kikao kilicholenga kujadili maendeleo ya mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kilichofanyika jijini Dar es Salaam, leo Januari 21, 2024.

Muktasari:

  • Ni katika majaribio ya mwanzo mtambo namba tisa kwenye mradi wa JNHPP.

Dar es Salaam. Kilowati 100 zimeanza kuingizwa kwenye gridi ya Taifa katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), imeelezwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, katika taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa leo Januari 21, 2024 amekaririwa akisema majaribio ya mtambo namba tisa katika mradi wa JNHPP yameleta mafanikio na kilowati 100 zimeanza kuingizwa kwenye gridi hiyo.

Dk Biteko ameeleza kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na wakandarasi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), akisema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa kampuni ya Elsewedy, Injinia Wael Hamdy kuhusu majaribio hayo.

Naibu Waziri Mkuu huyo amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Assem Elgazzar.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam, kuzungumzia maendeleo ya mradi wa JNHPP ambao kwa sasa umefikia asilimia 95.83.

Waziri Elgazzar amefuatana na watendaji wakuu wa kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors wanaotekeleza mradi wa JNHPP.

Kwa upande wa Tanzania, viongozi waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

“Kikao hiki kimejikita kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu mradi wa JNHPP, Waziri Elgazzar ametumwa na Rais wa Misri kuona maendeleo ya mradi huu,” amesema na kuongeza:

“Jambo lililotufurahisha hapa ni majaribio ya mtambo namba tisa yanayoendelea, kwa hatua ya mwanzo ambayo wamejaribu kuzungusha mtambo kwa njia ya maji wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wameingiza kilowati 100 kwenye gridi ya Taifa.”

Amesema mafanikio ya majaribio hayo yanaleta matumaini kwa kuwa ratiba ya kazi inaenda mapema zaidi ya iliyopangwa mwanzo.

Dk Biteko amesema lengo ni kuzalisha megawati 235 kutoka mtambo namba tisa  ifikapo Februari mwaka huu, na kuendelea na mitambo mingine ikiwamo namba nane na saba.

Amesema mradi huo ni wa kipaumbele cha Rais Samia Suluhu Hassan ili Watanzania wapate umeme wa uhakika kwa kuwa mradi huo ukimalizika utaingiza megawati 2,115 kwenye gridi ya Taifa.

Naibu Waziri Mkuu amesema wamezungumzia pia masuala ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii zinazotokana na uwepo wa mradi huo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya mkataba.

Dk Biteko ameomba Watanzania wawe na subira wakati Serikali ikitekeleza miradi itakayoongeza kiasi cha umeme nchini, ukiwemo mradi wa JNHPP.

Amesema mradi huo ni wa kielelezo kwa Afrika kwani unaonyesha nchi za Kiafrika zinaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Waziri Elgazzar amesema nia ya Serikali ya Misri kutoka mwanzo ni kuona mradi huo unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati.

Amewapongeza wakandarasi na Tanesco kwa hatua nzuri ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema Serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwapa ushirikiano wakandarasi katika hatua zote za utekelezaji wa mradi, akisema kukamilika kwake kutatoa fursa kwa kampuni za nchi hizo kuendelea kuaminika kwenye utekelezaji wa miradi mingie ikiwemo ya umeme.