Kimeta wadaiwa kuua wawili, 30 walazwa Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai

Muktasari:

  • Watu wawili wakazi wa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia baada ya kula nyama ya ng'ombe anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa kimeta huku wengine zaidi ya watu 30, wakilazwa hospitalini.

Moshi.Watu wawili wakazi wa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia baada ya kula nyama ya ng'ombe anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa kimeta huku wengine zaidi ya watu 30, wakilazwa hospitalini.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kujifanya mtaalamu wa mifugo na kuthibitisha nyama hiyo ni salama, mtu huyo yupo mahututi katika Hospitali ya Ngoyoni Rombo.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 21, 2021 na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, amesema watu hao walikula nyama hiyo Oktoba 6, 2021 baada ya mtu aliyejifanya mtaalamu wa mifugo kuthibitisha nyama hiyo ni salama na kuipiga mihuri feki.

Kagaigai amesema zaidi ya watu 30 waliokula nyama hiyo waliathirika ambapo wawili wamefariki dunia, huku wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Ngoyoni iliyopo Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

"Oktoba 6, 2021, eneo la Mamsera, nyumbani kwa mwananchi mmoja, kulikuwa na Ng'ombe watatu na mmoja alikufa, mtu moja alijitokeza kuwa ni mtaalamu wa mifugo akathibitisha ng'ombe yule alikuwa mzima hana matatizo akagonga na mihuri ambayo nafikiri ilikuwa feki,"amesema RC Kagaigai.

"Baada ya kuchinja, mtu yule alianza kuugua, na waliokula nyama ile wote wakaanza kuugua, ikawekwa mashaka na walipofuatilia ikaonekana kuna dalili za kimeta,"amesema na kuongeza kuwa tayari Serikali imechukua hatua mbalimbali.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuiweka karantini mifugo yote iliyopo kwenye familia hiyo na akaongeza kusema kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta, na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka kula nyama za mizoga kutokana na hofu ya ugonjwa huo.

"Nitoe tahadhari kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro hususani Wilaya ya Rombo, kujiepusha kula nyama ya mizoga, kutokana na tukio hili, lakini Serikali bado tunaendelea na uchunguzi, ili kujua kama ni Kimeta au vinginevyo,"amesema.

Mkuu huyo wa Mkoa, alitumia pia nafasi hiyo, kuwataka wananchi na wale wote wenye mabucha ya nyama mkoani humo, kuhakikisha nyama hizo zimepimwa na mtaalamu wa mifugo aliyethibitishwa.

Imeandikwa na Florah Temba, Fina Lyimo na Ombeni Daniel