Kina Sabaya wafikishwa mahakamani kusikiliza hukumu

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza leo Juni 10,2022 ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake sita. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambayo leo mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambayo leo mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Leo Ijumaa Juni 10, 2022 Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo saa 3:13 asubuhi.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, Jamhuri ilikuwa na mashahidi 13 huku utetezi wakiwa na mashahidi nane ambapo watuhumiwa hao walikuwa wakitetewa na jopo la mawakili watano huku Mwahomange akijitetea mwenyewe.

Machi 31 mwaka huu Hakimu Kisinda, alisema atatoa hukumu hiyo leo baada ya pande zote kuwasilisha hoja zao za majumuisho.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano, la kwanza wakidaiwa wote saba Januari 22,2021 kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara FrancisĀ  Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh 90 milioni na matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Katika shauri hilo Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi Tarsila Gervas, Felix Kwetukia, Janeth Sekule, Wakili wa Serikali Neema Mbwana na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Jacopiyo Richard.

Watuhumiwa sita walitetewa na Mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Fridolin Bwemelo, Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka.

Mbali na washitakiwa wengine, Mwahomange ambaye ni mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo alijitetea mwenyewe baada ya Wakili Bwemelo kujiondoa kumtetea.

Machi 7, 2022 Bwemelo alisema ameamua kujiondoa kumtetea Mwahomange kwa kile alichodai kuwepo mgongano wa kimaslahi na kulinda maadili yake.

Awali Mei 6, 2022 Sabaya na wenzake wawili, Nyegu na Daniel Mbura waliachiwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania, baada ya kubaini dosari zilizojitokeza katika mwenendo wa kesi ya msingi liyokuwa ikiwakabili katika mahakama ya chini ambapo walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Katika Rufaa hiyo ya jinai namba 129/2021 ilikatwa na Sabaya na wenzake wawili ambao ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wakipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela walichohukumiwa Oktoba 15 mwaka jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Sabaya na wenzake, alisema mahakama inabatilisha mwenendo wa kesi ya msingi na kutengua hatia dhidi ya warufani hao na adhabu iliyotolewa dhidi yao inatupiliwa mbali.

Sabaya na wenzake wawili walihukumiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kuwatia hatiani katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikiwakabili.

Licha ya kuachiwa kwenye rufaa hiyo, Sabaya aliendelea kukaa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo Arusha na watuhumiwa wenzake ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.