Kiongozi mbio za mwenge agoma kuzindua mradi

Askari wa kikosi cha Kuzuia Ghasia ( FFU) mkoa wa Mara akibandua kibao kilichoanadaliwa kwaajili yamradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi nchini (Veta) Butiama baada ya kiongozi wa mbio za mwenge Luteni Josephine Mwambashi kukataa kuweka jiwe la msingi.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Kiongozi wa mbio za mwenge, Luteni Josephine Mwambashi amekataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi nchini (Veta) Wilaya ya Butiama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi makubwa ya fedha yasiyoendana na thamani ya majengo.

Butiama. Kiongozi wa mbio za mwenge, Luteni Josephine Mwambashi amekataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi nchini (Veta) Wilaya ya Butiama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi makubwa ya fedha yasiyoendana na thamani ya majengo.

Amesema banda la walinzi pekee hadi kukamilika litagharimu Sh10 milioni.

Akizungumza leo Jumamosi Juni 26, 2021 baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mwambashi amesema baadhi ya majengo yamejengwa kwa gharama kubwa.

"Hicho kibanda cha walinzi hapo kilipo kimegharimu zaidi ya Sh4 milioni na bado kimeombewa zaidi ya Sh5 milioni eti hadi kukamilika kitagharimu Sh10 milioni, sasa banda hilo pekee ligharimu Sh10 milioni kweli? Inatia shaka,” amesema.

Amesema ujenzi huo unatumia mkataba wa zamani wa Sh1.6 bilioni tofauti na Sh2.2 bilioni zilizobadilishwa huku akishangazwa kuona unaotumika ni mkataba wa zamani wakati kuna majengo yalibadilishwa kutokana na mkataba mpya.

 Alieleza jinsi wasimamizi wa mradi huo walivyoshindwa kuonyesha nyaraka mbalimbali za mradu husika zikiwemo barua za kupokea fedha kutoka serikalini.

Kutokana na dosari hizo ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha hizo.

Awali,  msimamizi wa mradi huo David Benedict akitoa taarifa  amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Januari, 2021 unatarajiwa kukamilika Septemba, 2021 na kwamba hadi sasa wametumia zaidi ya Sh1.4 bilioni.