Kiongozi mbio za Mwenge aonya upandaji miti wa fasheni

Muktasari:

  • Kiongozi huyo amesema kumekuwa na tabia ya upandaji miti sehemu mbalimbali unaofanywa  kama fasheni, viongozi wanapanda miti kwa kujionyesha lakini hawasimamii kuhakikisha inakua.

Hai. Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Godfrey Mzava amezitaka halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kupanda miti kama fasheni kwani zinarudisha nyuma jitihada za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira.

Mzava ametoa wito huo leo Aprili 5, 2024 alipokuwa akikagua  mradi wa ujenzi wa tanki la maji katika kata ya Masama Rundugai lililopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo ametaka mtindo wa kupanda miti kama fasheni uishe badala yake wanaoshiriki kuipanda waisimamie kuhakikisha inakua.

Amesema wengi wanaoipanda kwenye maeneo mbalimbali wamekuwa wakifanya hivyo kujionyesha na si kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

 “Maeneo mengi yamekuwa yakipandwa miti kwa kujirudia, mwaka huu wanapanda miti taasisi fulani, kwa sababu uangalizi hakuna inakufa, mwakani wanakuja wengine wanapanda miti eneo hilohilo, unakuwa ni mchezo, viongozi wapo kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na wilaya sijui wanafanya nini,” amehoji Mzava.

Amesema mambo hayo yamekuwa yakiifanya Serikali kushindwa kufikia malengo iliyojiwekea ya kurudisha miti iliyopotea kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wananchi kwa kukata miti ovyo.

 “Tunapokuja mikoa yote iliyobaki, halmashauri zilizosalia, hizo ndiyo salamu za mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024, tuhakikishe tunapanda miti na tutakuja kuikagua kuhakikisha inakua, tumefanya uharibifu mkubwa sana wa mazingira,” amesema Mzava.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa ameahidi kusimamia maelekezo hayo ili wilaya hiyo ibaki ya kijani na salama. “Mbali na upandaji miti pia tutalinda  vyanzo vya maji ndani ya miti 60 kusifanyike shughuli zozote za kibinadamu.”

“Tumepokea maelekezo tutahakikisha miti tunayoipanda inakua na kufikiwa malengo yetu ya kurejesha kijani,” amesema Mkalipa kwenye uzinduzi wa mradi huo.