Kipanga ahimiza matumizi ya teknolojia kufikia viwanda

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga

Muktasari:

  • Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women) kupitia kampeni yake ya 'binti dijitali 'limetoa mafunzo ya ubunifu katika masuala ya teknolojia kwa wasichana 50 kutoka katika maeneo nchini.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amewataka vijana kutumia maarifa waliyoyapata vyuoni kuleta mabadiliko katika jamii haswa katika uga huo wa teknolojia.

Kipanga ameyasema hayo leo Septemba 29, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwapongeza wahitimu wa mafunzo ya ubunifu katika masuala ya teknolojia kwa wasichana 50 yaliyotolewa na Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women).

Mafunzo hayo ya pili yamefanyika kwa siku 10 kuanzia Septemba 18 hadi 29 mwaka huu, kupitia kampeni ya 'binti dijitali.’

Kipanga amesema mafunzo hayo ni muhimu hasa katika nyakati hizi za mapinduzi ya viwanda ambayo yanaihitaji zaidi teknolojia.

"Hata dira ya maendeleo ya mwaka 2025 inakusudia kujenga uchumi imara na wenye ushindani huku ikisisitiza uendelezaji wa sayansi na teknolojia," amesema.

Amesema marekebisho yanayoendelea ya mtaala wa elimu ya sekondari yamejumuisha masomo ya ufundi stadi katika mitaala ya elimu ya sekondari ya chini ili kuongeza ushiriki wa wavulana na wasichana katika fani zinazohusiana na sayansi na tehama.

 Tanzania pia imekuwa na sera mahususi katika kuhakikisha usawa wa kijinsia na katika masuala mbalimbali ikiwemo yale yanahusu sayansi na teknolojia.

"Juhudi hizi zimesababisha ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wasichana shuleni katika miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo ni muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana.

"Tunaaona wanafunzi wa kike wanaosoma elimu ya juu ya sayansi na teknolojia wakileta tofauti kubwa katika jamii zao, mfano mwanadada kutoka Zanzibar ambaye alikuwa mwanafunzi wa kwanza Afrika Mashariki kuendesha ndege zisizo na rubani," amesema.

Hivyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja na serikali katika kuhakikisha mafunzo kama hayo yanaendelea kutolewa ili kuwafikia wasichana wengi.

Kwa upande wake mmoja kati ya mkufunzi wa mafunzo hayo, Rachel Cornelio amesema katika kambi hiyo maalum ya mafunzo ya teknolojia kwa wasichana ilikuwa ikifundisha mambo mbalimbali ikiwemo ubunifu wa programu mbalimbali za simu janja, tovuti, michezo mbalimbali ya  komputa pamoja na elimu kuhusu soko la kidigitali.

Amesema baada ya mafunzo hayo kuisha wataendelea kuwafatilia wanafunzi hao na kuwasaidia ili waweze kufanya mambo makubwa zaidi kupitia mafunzo hayo.

Mmoja kati ya wahitimu wa mafunzo hayo Matilda Mashauri amesema mafunzo hayo yamempa mwanga wa namna gani anaweza kuitumia teknolojia kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii pia kujitengenezea ajira na hata kuwaajiri wengine.

Mwakilishi kutoka UN-Women Mitra Sadananda amesema utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa asilimia 90 ya kazi zote zinahitaji kuwa na maarifa kuhusu masuala ya teknolojia, hivyo uwepo wa mafunzo hayo ni muhimu kwani utasaidia kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika mapinduzi ya teknolojia nchini.

Naye mwakilishi kutoka balozi wa Ubelgij hapa nchini, Petra Heylen amesema wataendelea kushirkiana na Tanzania kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa na kuimarika hapa nchini.