Kipanya na viunzi hadi kutimiza ndoto

Mkuu wa kichengo cha uzalishaji wa kampuni ya Kaypee Motors,Rajab Hassan akitengeneza gari katika karakana iliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam jana.Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Siku chache baada ya kulizindua gari lake la umeme, Ally Masoud maarufu ‘Kipanya’ amesema ameshapokea oda za wateja watano anazozifanyia kazi, huku akiendelea kujipanga kwa uzalishaji mkubwa zaidi.


Dar es Salaam. Siku chache baada ya kulizindua gari lake la umeme, Ally Masoud maarufu ‘Kipanya’ amesema ameshapokea oda za wateja watano anazozifanyia kazi, huku akiendelea kujipanga kwa uzalishaji mkubwa zaidi.

Masoud, aliyejizolea umaarufu kwa fani yake ya uchoraji katuni ya Kipanya inayochapishwa kila siku ndani ya gazeti hili, ameiingiza Tanzania katika rekodi za ulimwengu wa teknolojia, baada ya kuunda gari hilo tangu teknolojia hiyo ilipoanzishwa zaidi ya karne moja iliyopita na Mscotland Robert Anderson.

Hatua hiyo ya Masoud imekuja kipindi ambacho kampuni nyingi duniani zinajielekeza katika utengenezaji wa magari ya umeme, ikiwamo Jaguar inayopanga kuyauza magari hayo kuanzia mwaka 2025, Volvo mwaka 2030 na Lotus mwaka 2028.

Kampuni ya General Motors itaanza kufanya hivyo mwaka 2035, Ford mwaka 2030 na Volkswagen mwaka 2030 kwa asilimia 70 ya magari yote itakayoyazalisha.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Masoud alisema anahitaji mtaji wa Sh2 bilioni kuanza uzalishaji mkubwa utakaoiwezesha kampuni yake ya Keypee Motors kuzalisha walau magari 100 kwa mwezi.

“Tunalenga soko la ndani na nje, Tanzania tuna mazoea ya kuagiza bila sisi kupeleka bidhaa zetu nje, hivyo tunaishia kutumia fedha zetu na hatuingizi za kigeni,” alisema.

Kiasi hicho cha fedha, alisema kitawezesha kununua teknolojia zitakazorahisisha uundaji gari, kutoka kutumia saa au siku nzima hadi kuwa tendo la sekunde tu.

Alisema mtaji anaohitaji hatarajii kuupata haraka, bali ni mchakato wa polepole hadi atakapofikia anapotarajia.

“Tukipata fedha hii maana yake tutapata teknolojia zitakazotuwezesha kutengeneza gari 100 kwa mwezi mmoja, kwa sababu leo hii ili kutengeneza boneti, tunakata bati kwa kutumia mkono, lakini kwa teknolojia tutatumia mashine itakayoharakisha zaidi,” alisema.

Hata hivyo, alisema matumizi ya mkono katika kazi nyingi zilizofanyika kuunda gari hilo ndicho kilichosababisha kutumia miezi 21 hadi kukamilika kwake.

“Nilikuwa nachora, nakata napinda mwenyewe kwa namna ninavyotaka, hii inachelewesha ukilinganisha na matumizi ya teknolojia za kisasa,” alisema Masoud.

Kuhusu upatikanaji wa mtaji, Masoud alisema hana haraka ya kutafuta mbia wa kushirikiana naye, bali anakwenda taratibu akiangalia njia sahihi ya kupata kiasi hicho cha fedha.

“Sina haraka kwa sababu najua vitu vikienda polepole kuna raha yake, ndiyo maana huoni nazungumzia mikopo,” alisema.

Lakini, akaongeza kuwa ameshaanza mchakato wa kuzitumia fursa zilizopo Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), kutaka kukuza mtaji wa kampuni yake kwa kuitumia program ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati.

Masuala ya kisera

Ili Tanzania izalishe wabunifu wengi, Masoud anasema ni budi Serikali ibadili mifumo ya elimu ili iwe inatunza na kuvilea vipaji badala ya kuviua.

Akifafanua katika hilo, anasema kuna kazi kubwa inayopaswa kufanywa na Serikali kwa kutengeneza miongozo itakayowawezesha wabunifu kufahamu njia sahihi za kupita ili kufikia malengo yao.

“Sisi wakati tunatafuta leseni tulikwenda Manispaa hawakutuelewa, tumekwenda wizarani hawakutuelewa, hiyo yote ni sababu hakuna mtu aliyewahi kuomba leseni ya kuunda gari kabisa, leseni nyingi zilizokuwa zinaombwa ni za kuunganisha,” anasema mbunifu huyo.

Hata hivyo, amebainisha kuwa Tanzania imekuwa mlaji zaidi katika masuala ya teknolojia, ndiyo sababu bado hakuna sera zinazosimamia suala hilo.

Katika mazungumzo yake hayo, Masoud alisema tayari ameshakamilisha maelekezo ya Serikali ya kumtaka awasilishe mahitaji yake.

Alianza kuota gari

Masoud anasema wazo la kutengeneza gari alidumu nalo miaka tisa. Licha ya kuwa na wazo pekee, lakini alikwenda mbali zaidi pale alipoamua kukusanya rasilimali mbalimbali alizoona zitasaidia kufanikisha wazo lake hilo.

“Nilikwenda jeshini katika kampuni ya Nyumbu kuona wapi kuna watu wanaofanya kitu ninachotaka kukifanya, nilifika nikazungumza nao wakawa wanasubiri kuona lini nitafanya,” anasema.

Amefanikiwa vipi

Masoud anasema utengenezaji wa gari hilo umehusisha wataalamu wa kada mbalimbali na kila mmoja alimwita kufanya kazi ya utaalamu wake.

Anasema aliwatumia wataalamu wa umeme, kuchomea vyuma, wataalamu wa rangi na hao wote hakuna aliyemtoa kutoka Vyuo vya Ufundi Stadi.

“Usije ukadhani kuwa ili ufanye kitu kama hiki unahitaji vijana ambao wana elimu gani sijui, hapana, inategemea na wewe unataka kutengeneza kitu gani. Hapo ndio utafahamu mahitaji yako,” anasema Masoud.

Teknolojia ikoje

Masoud anasema changamoto ya kukosekana kwa teknolojia ya uhakika, kumemfanya atumie muda mrefu kutengeneza gari hilo lenye uwezo wa kubeba mzigo wa kilo 500 na linalokidhi mahitaji ya Watanzania.

“Watanzania wengi wanataka gari za shughuli angalau iwe inabeba mzigo, wengine ni wakulima watataka kuona gari zinawasaidia kubeba mazao kutoka shambani, ndiyo maana nikatengeneza gari ya aina hii,” anasema.

Bei ya gari sasa

Tofauti na mawazo ya watu wengi, Masoud anasema kuwa licha ya kwamba aliutangazia umma kuwa bei ya gari hilo ni Sh8 milioni, huenda baadaye ikapanda kutokana na gharama za teknolojia.

“Mfumo wa umeme utakaokupa kilomita nyingi za kwenda unahitaji gharama za betri, hivi vitu vyote vipo vinauzwa lakini gharama yake kubwa,” anasema.

Alisema ni vigumu kubainisha sasa kwamba gharama ya gari hiyo itaongezeka kwa kiasi gani, lakini kadri siku zinavyokwenda kila kitu kitakuwa wazi.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa sasa hakujielekeza zaidi katika kupata faida, badala yake anafanya kila awezalo kuthibitisha kwa umma wa Watanzania kuwa magari yanayotengenezwa na kampuni yake yanakuwa bora.

Aliongeza gari zote atakazotengeneza kuanzia sasa zitakuwa na spidi 80.

Mbali na gari alilotengeneza, Masoud alisema mengine mawili ya majaribio yamekamilika kwa asilimia 60 ya utengenezaji na tofauti yake na iliyopo sasa ni ukubwa wa bodi.

Kwa sasa Keypee Motors ina wafanyakazi 13 pamoja naye na kila mmoja amechangia kwa namna yake kufanikisha uundwaji wake.

Kwa mujibu wa Masoud, ubunifu huo hakuuanza leo, amekuwa akiuishi katika uchoraji katuni, lakini hata alivyokuwa mtoto alipenda kutengeneza magari.

“Nilipenda kufanya kitu kifanane na uhalisia, nilikuwa natengeneza gari zinafanana kabisa, kwa hiyo tangu wakati huo nilikuwa napenda vitu hivi,” anasema Masoud.

Amesema si kila aliyemshirikisha katika safari yake ya kutengeneza gari hilo alimuelewa, kwa sababu wapo ambao hawakumuelewa na sasa wanashangaa kuona amefanikiwa.

Keypee Motors kujengwa wapi

Katika hatua nyingine, Masoud alisema kwa sasa Shirika la Kusaidia Viwanda Vidogo (SIDO) ndipo yalipo makao makuu ya kampuni hiyo na baadaye anatarajia kutafuta eneo kubwa litakalotosheleza uwekezaji atakaofanya.

“Kwa sasa nipo Sido, lakini ni eneo dogo kwa uwekezaji nitakaofanya, nahitaji eneo zaidi, nadhani nitatafuta maeneo ambayo hayatakuwa mbali na Dar es Salaam ila pembezoni mwa mji,” anasema.

Anapofikiria kuwa makao makuu rasmi ya Kaypee Motors, alisema ni Bagamoyo na wakati ukifika atatafuta eneo lenye ukubwa wa kati ya ekari mbili na kuendelea.

Anasema Bagamoyo kwa sababu ni eneo sahihi kwa uwekezaji, pia halipo mbali na Jiji la biashara la Dar es Salaam.

Wataalamu vipi

Mbunifu huyo anasema watu 14 wote kutoka nchini wamehusika katika kutengeneza gari hilo na hakuna mtaalamu aliyekwenda shule kwa shughuli aliyofanya.

“Hawa mafundi mmoja katoka Mwananyamala, mwingine Magomeni, kwa mfano wa kuchomea katokea Magomeni hata VETA panafananaje hafahamu,” amesema.

Anasema kinachohitajika ni usimamizi na uangalizi wa vipimo ambavyo mbunifu anahitaji, hivyo haihitaji fundi mwenye taaluma au uwezo mkubwa kufanya kazi hizo.

Amebainisha kuwa alitumia mafundi wa mtaani, alichozingatia ni kuwasimamia kuhakikisha wanafanya kwa namna anavyohitaji kulingana na vipimo vyake.

Amesisitiza kuwa kila fundi anaweza kufanya chochote chini ya uwezo wake iwapo atasimamiwa na kuelekezwa namna kinavyohitajika.

“Kwenye kutengeneza ile timu ili bati liunganike linahitaji kuchomwa, kwa hiyo hapo nilitafuta fundi wa kuchomea, ametoka zake huko kwa kazi hiyo tu, wewe utamwambia achome nini.

“Kuna mpaka rangi, kuna mtu anaujua umeme, wewe unajua nini kinahitajika ili gari la umeme liwe lakini sio fundi wa umeme, hivyo nimemchukua fundi wa umeme.

“Sio kila unayemuita anakuelewa wengine wanakuona sio, anakuja kwa sababu anajua analipwa basi anafanya kazi yake anaondoka, huo mtazamo unabadilika kadri siku zinavyokwenda na hata ilipofika siku ya uzinduzi na wenyewe walikuwa wanashangilia,” alisema.

Amemtolea mfano fundi wake wa kwanza wa kuchomea aliishia njiani, kwa kuwa hakuamini kama kile alichokuwa akikiwaza Masoud kitatimia.

“Juzi amenipigia simu anataka kuwa sehemu ya safari, watu wengi hawajui nguvu waliyokuwa nayo ndiyo maana mawazo huwa yanaishia njiani,” anasema Masoud.

Kifuatacho...

Baada ya miaka 10, Masoud alisema anatarajia kampuni yake kuwa suluhu ya ajira kwa vijana wengi nchini na iwe miongoni mwa zinazozalisha magari mengi.

Mbali na kuuza magari nchini, baada ya kipindi hicho anatarajia kuuza nje ya nchi na kuiwezesha Tanzania kuongeza vyanzo vyake vya kukusanya mapato na kuingiza fedha za kigeni.

“Katika hili naomba niwaambie Watanzania wenzangu, tusidharau bidhaa zinazozalishwa nchini, tuzinunue kwa nguvu zote, ukinunua kitu kimoja cha Tanzania unatengeneza faida kubwa bila wewe kujua kwa maslahi ya nchi yako.

“Tusiishie kusema vya Tanzania havina ubora, nunua kama kuna changamoto sema ili mtengenezaji aendelee kuboresha, kwa nini sisi tuendelee kuwa mlaji kila siku,” anasema.