Kipimo cha wasanii ‘mateja’  mbioni kuanza

Kamishna Jenerali wa (DCEA), Aretas Lyimo

Muktasari:

  • Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kipimo cha wasanii wanaotumia dawa za kulevya kipo mbioni kuanza na tayari baadhi ya vifaa vimeshafungwa maabara.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kipimo cha wasanii wanaotumia dawa za kulevya kipo mbioni na tayari baadhi ya vifaa vimefungwa maabara.

Novemba 14 mwaka jana Kamishna Jenerali wa (DCEA), Aretas Lyimo alisema mamlaka hiyo inakamilisha ujenzi wa maabara mpya ya ukaguzi na sayansi jinai yenye mitambo ya kisasa kwa ajili ya kupima wasanii hususani wa kizazi kipya.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili siku chache zilizopita ofisini kwake, Lyimo alisema tayari baadhi ya vifaa vimeshafungwa katika maabara hiyo kwa ajili ya kuanza huduma za kupima watumia dawa za kulevya. 

“Tumefikia pazuri na tunaendelea nayo, tunasubiri baadhi ya vifaa, kuna vingine vimechelewa bandarini na vingine vimeshafika na kufungwa,” amesema akifafanua:

“Tayari kuna baadhi ya wasanii tumeshafanya nao mahojiano, na orodha tunayo, sasa tuliona tusiweke ‘public’ (kwa umma), tutaweka hadharani pale ambapo tutafanya naye mahojiano, tukamuonya na akaendelea, tutawaita na kuwapima, vifaa hivyo vinaonyesha hata kama unatumia dawa zaidi ya tano.”

Endapo watakutwa na dawa za kulevya, Lyimo amesema sheria inaelekeza kumfungulia mashtaka au kumuonya ili aache.

“Sisi tutaanza na kuwaonya ili waache. Lakini pia tutamfungulia jalada la uchunguzi, atalazimika kuripoti ili kumfuatilia mara kwa mara ili tuone mwenendo wake.”

“Jambo kubwa tutahakikisha kwenye sanaa yake haonyeshi matendo ya kuhamasisha matumizi ya dawa hizo. Au yeye kwa matamshi yake asiwe na ushawishi huo. Endapo ataendelea kufanya hivyo tutampeleka mahakamani moja kwa moja,”amesema.