Samia awaonya wasanii matumizi dawa za kulevya

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wasanii nchini wakitaka kujua ubaya wa matumizi ya dawa za kulevya watazame wasanii wenzao waliokuwa wakitumia dawa hizo, akiwemo mwanamuziki,  Whitney Houston

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wasanii nchini wakitaka kujua ubaya wa matumizi ya dawa za kulevya watazame wenzao waliokuwa wakitumia dawa hizo, akiwemo mwanamuziki,  Whitney Houston.

Whitney Huston alifariki dunia Februari 11, 2012 katika Hoteli ya Beverly Hilton jijini Los Angeles, Marekani saa chache kabla ya kufanya onyesho kwenye sherehe za maandalizi ya Tuzo za Grammy.

Mkuu wa Polisi wa Beverly Hills, Luteni Mark Rosen alithibitisha kukutwa kwa aina fulani ya vidonge vya kutuliza maumivu katika chumba alichofia mwanamuziki huyo, huku kukiwa na ushahidi kuwa alikuwa akitumia dawa za kulevya baada ya kushindwa kutumbuiza jukwaani mara kadhaa na kukaa kimya ‘akisikilizia’ kama wafanyavyo mateja.

Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 13, 2019 kwenye kongamano kuhusu tatizo la dawa za kulevya  kwa wasanii lililoandaliwa na Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini (DCEA)  kwa kushirikiana  na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Amewataka wasanii nchini kutoiga kila jambo kutoka kwa wasanii mbalimbali wakubwa duniani, akimtolea mfano Withney aliyesema pamoja na utajiri wake amefariki kwa matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema wakati wasanii hao wakitumia dawa za kulevya zilizopimwa, wasanii nchini wanatumia mataputapu.

"Wenzenu kule wakipatwa hata na kikohozi wana bima kubwa za matibabu, hapa kwetu tutaishia kukupa tangawizi na kumbe ndio tunakumaliza bila kujua,” amesema Samia.

“Wanangu matumizi ya dawa yana athari kubwa kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kwa wale ambao mnazitumia au mnataka kuzitumia acheni kabisa.”