Kipindupindu chaua mwingine Geita

Muktasari:

Kufuatia kuibuka kwa ugonjwa huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Marx Kamaoni ameagiza maofisa afya kuendesha msako wa kufunga migahawa yote ya kuuza vyakula.     

Geita. Siku chache baada ya wagonjwa wawili kufariki dunia kati ya 50 waliobainika kuugua ugonjwa wa kipindupindu katika Wilaya ya Geita, mgonjwa mwingine amefariki kwa ugonjwa huo.

Kufuatia kuibuka kwa ugonjwa huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Marx Kamaoni ameagiza maofisa afya kuendesha msako wa kufunga migahawa yote ya kuuza vyakula.

Akizungumza kwenye Kambi ya Kipindupindu Nyankumbu juzi, Ofisa Afya wa halmashauri hiyo, Mabela Mabela alisema ugonjwa huo umegundulika Mji wa Geita Desemba 13, mwaka huu baada ya mwanamke mmoja na watoto wake wawili kuugua.

Mabela alisema siku iliyofuata idara ya afya ilifungua kambi hiyo, lakini kwa bahati mbaya mwanamke huyo mkazi wa Mtaa wa Mbugani alifariki dunia akipatiwa matibabu.

“Mwanzo tulikuwa na kesi tatu kutoka Mtaa wa Mbugani, mmoja alifariki dunia wengine watatu wameruhusiwa baada ya hali zao kuwa vizuri, hadi leo (juzi) wagonjwa waliopo ni wawili na mmoja anasubiri vipimo baada ya kuonekana na kuharisha na kutapika,” alisema.

Mganga wa Kambi hiyo, Dk Jeremiah Nikanory alisema wagonjwa wanaofika wanakuwa na dalili za kuharisha na kutapika mfululizo huku baadhi yao wakiwa wamelegea.

“Kinachotakiwa ni kuzingatia usafi, pia watumie vyoo, kunawa baada ya kutoka chooni na kuepuka kula chakula ovyo, wakifanya hivyo natumaini ugonjwa huu hautawapata,” alisema Dk Nikanory.

Mama mzazi wa mtoto Boniphace Charles ambaye amelazwa katika kambi hiyo, Theresa Enock mkazi wa Nyankumbu alisema mwanawe alianza kuharisha na kutapika lakini alipompeleka hospitali aligundulika ana kipindupindu.

Watu watatu wamefariki dunia kati ya 59 waliogundulika kuugua ugonjwa huo wilayani Geita. Ugonjwa wa kipindupindu umeenea kwa kasi katika mikoa mbalimbali nchini.