Kisutu yawatupa jela Wakenya wawili

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa Kenya, Magreth Ounza (19) kifungo cha miaka mitano jela na kulipa faini ya Sh500, 000 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuingia na kukaa nchini bila kibali.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa Kenya, Magreth Ounza (19) kifungo cha miaka mitano jela na kulipa faini ya Sh500, 000 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuingia na kukaa nchini bila kibali.

Pia, Mahakama hiyo imemhukumu, Mayah Nasimiyu ambaye naye ni rais wa Kenya, kifungo cha mwaka mmoja jela pamoja na kulipa faini ya Sh500, 000 ambavyo vyote vinaenda kwa pamoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuingia na kuishi nchini.

Watuhumiwa hao kwa pamoja Novemba 23, 2021 waliingia na kuishi maeneo ya Mazese bila ya kuwa na kibali huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga ambaye amesema kwa kuwa washtakiwa wamekubali makosa yao yanayowakabili na mahakama hiyo imethibitisha hivyo inawatia hatiani.

Ruboroga amesema mahakama hiyo imezingatia kumbukumbu ya mshtakiwa hasa Ounza amekuwa na kumbukumbu ya makosa mengine na amehukumiwa katika mahakama hiyo hivyo kutokana na hilo inamhukumu kwenda jela miaka mitano na kulipa faini ya Sh500, 000 ambavyo vyote vinaenda pamoja.

Amesema kwa upande wa mshtakiwa, Nasimiyu mahakama hiyo imemuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela na kulipa faini ya Sh500, 000 ambavyo vyote vinaenda kwa pamoja


Awali wakili wa Serikali, Hadija Masoud aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa Ounza alishawahi kutiwa hatiani katika mahakama hiyo kesi namba 53/2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,J aneth Mtega kwa makosa ya kuingia na kuishi nchini bila kibali.

Masoud alidai mshtakiwa huyo alihukumiwa kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kila kosa au kwenda jela miezi mitatu hivyo alishindwa kulipa faini alifungwa gereza la Segerea Aprli 21, 2021.

"Kwa upande wa mshtakiwa Nasimiyu hatuna kumbukumbu ya makosa yake lakini mshtakiwa Ounza alimaliza kifungo chake June 18, 2021 baada ya kutoka gerezani Serikali ya Tanzania ilichukua jukumu la kumsafirisha hadi nchini Kenya kwa makusudi tena amerudia makosa yale yale hivyo naiomba mahakama hii impe adhabu kali,"alidai Masoud