Kiti cha uenezi CCM moto, miaka mitatu ya Rais Samia

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ambapo aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha. Hatua hiyo itamfanya apendekeze jina la mwenezi mpya atakayeridhiwa na kuteuliwa na halmashauri kuu ya CCM.

Dar es Salaam. Unaweza kusema kuwa miaka mitatu ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa kaa la moto kwa kila aliyeteuliwa kushika nafasi ya kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, kwani wamekuwa wakikaa muda mfupi na kubadilishwa kwa kupangiwa majukumu mengine.

Hadi sasa, makatibu wa itikadi na uenezi wanne wamebadilishwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia na wote wamepangiwa majukumu mengine baada ya kuonekana upungufu walipokalia kiti hicho.

Alipoingia madarakani na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, Rais Samia alifanya kazi na Humphrey Polepole, kama katibu wa itikadi na uenezi aliyemkuta. Polepole aliteuliwa kushika nafasi hiyo Desemba 13, 2016 akijaza nafasi iliyoachwa na Nape Nnauye.

Aprili 30, 2021, halmashauri kuu ya CCM ilimteua Shaka Hamdu Shaka kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo akichukua nafasi ya Polepole ambaye alibaki kuwa mbunge na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na baadaye kuhamishiwa Cuba.

Januari 14, 2023, Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya uteuzi mwingine wa Sophia Mjema kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo akichukua nafasi ya Shaka aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Mjema alifanya kazi hiyo kwa miezi 10 pekee ambapo Oktoba 22, 2023, Paul Makonda aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kujaza nafasi yake baada ya yeye kuteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Masuala ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu.

Safari ya makonda kwenye nafasi hiyo imekuwa ya muda mfupi kwa kuwa amedmu kwa miezi mitano hadi leo Machi 31, 2024 Rais Samia alipofanya mabadiliko kwa kumtoa na kumteua kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha.

Swali lililo vichwani mwa watu ni nani atakayejaza nafasi ya Makonda? Awe na sifa zipi zitakazomfanya adumu kwenye nafasi hiyo? Kipi kipya atakileta kwenye chama hasa wakati huu Taifa likielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025?

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya Rais Samia, sekretarieti ya CCM imekuwa ikipitia mabadiliko makubwa. Itakumbukwa hivi karibuni, Rais Samia alimteua aliyekuwa naibu Katibu Mkuu wa CCM – Bara, Anamringi Macha kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Pia, Novemba 29, 2023, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alijiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai kudhalilishwa mitandaoni. Baadaye Januari 15, 2024, Dk Emmanuel Nchimbi aliteuliwa kujaza nafasi hiyo.

Katika mabadiliko ya leo Machi 31, 2024, mbali na Makonda, Rais Samia amewateua Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Fakii Lulandala kuwa mkuu wa wilaya ya Simanjiro na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Gilbert Kalima kuwa mkuu wa wilaya ya Mkinga.