CCM yafanya mabadiliko ya sekretarieti, yateua wajumbe kamati kuu

Muktasari:

Safu ya wajumbe saba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) imetangazwa leo baada ya kikao maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).


Dar es Salaam. Safu ya wajumbe saba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) imetangazwa leo baada ya kikao maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kikao hicho kilichofanyika leo Januari 14, 2023 kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.

Akitoa taarifa ya kikao hicho, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema Kamati kuu ya chama iliketi na vikao vyote vilihitimishwa na Halmashauri Kuu chini ya mwenyekiti wake.

“Pamoja na mambo mengine ya kupokea na kufanyia kazi taarifa mbalimbali za chama, kikao kimeteua  safu mpya za wajumbe wa NEC na kuidhinisha sekretarieti,” amesema.

CCM yafanya mabadiliko ya sekretarieti, yateua wajumbe kamati kuu

Amesema mwaka 2022 chama hicho kilikuwa na uchaguzi wa chama ngazi ya shina mpaka taifa na baada ya kumaliza Hamalshauri kuu ya Taifa imefanya uteuzi wa kukamikisha safu ya wajumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi.

“Wajumbe sita wamechaguliwa ambapo watatu wanatoka Tanzania Bara na watatu Zanzibar ili kukamilisha wajumbe wa kamati kuu kufika 24, hawa saba kwa mujibu wa katiba wamechaguliwa na safu,” amesema Shaka.

Amewataja wajumbe kutoka Bara kuwa ni pamoja na Mizengo Pinda (Waziri Mkuu mstaafu), Hassan Wakasuvi (mwenyekiti CCM Tabora), Halima Mamuya ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa umoja wa wanawake Tanzania.

Kwa upande wa Zanzibar amemtaja Mohamed Abood Mohamed, Injinia Nasri Ally na Leyla Burhan Ngozi akisisitiza kuwa kila upande nafasi mbili zilikuwa za wanaume na nafasi mbili wanawake.

Shaka amesema kikao hicho kimeithibitisha sekretariet ya Halmashauri kuu ya taifa na kutaja orodha ya wajumbe waliochaguliwa.

Amesema nafasi ya Katibu Mkuu ameendelea Daniel Chongolo, Naibu Katibu Mkuu Bara Annamringi Macha, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mohemed Said Dimwa.

Amesema nafasi yake ya Katibu Itikadi na Uenezi imechukuliwa na Sophia Edward Mjema, Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha,  Dk Frank Hawasi, Katibu siasa na uhusiano wa kimataifa Mbarouk Nassoro na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Haji Usi Gavu.

Aidha Shaka ametumia fursa hiyo kuaga rasmi akivishukuru vyombo vya habari na Watanzania.

“Nichukue fursa hii kuwashkuru wanahabari tulifanya kazi pamoja na namna ambavyo tulishirikiana  kujenga chama hiki, tuendelee kumpa ushirikiano mwenezi mpya, kwa niaba yangu binafsi niwashkuru kwa mchango wenu mlioutoa kwenye chama hasa kipindi cha uchaguzi tunaendelea kuwaombea Mungu awabariki sana kazi inaendelea,”